Moja ya malengo ya serikali yetu tangu baada ya Uhuru ni kupambana na janga la Umaskini. Tangu enzi za Mwalimu Nyerere, Alhaji Mwinyi, Mh. Mkapa na hata Kikwete mapambano dhidi ya umaskini yanaendelezwa tena sasa kwa kile kinachodaiwa kuwa Ari, kasi na Nguvu Mpya. Ni wazi pia kuwa mapambano hayo sasa yameelekezwa katika kuboresha na kuinua hali za kimaisha za makundi dhaifu na yaliyo katika hali mbaya zaidi ya umaskini. Makundi hayo ni kama vile Wazee, Walemavu, Watoto na hasa Yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, pamoja na WANAWAKE. Leo nitazungumzia zaidi kundi hili la mwisho.
Lengo la kuinua maisha ya wanawake ambao wameishi katika umaskini wa kutupwa kwa karne nyingi ni sambamba na kuwawezesha kumiliki mali na hasa Ardhi, na kushirikishwa katika maamuzi katika ngazi za uongozi serikalini, katika jamii na familia.
Kuna mifano kadhaa ambayo inathibitisha juhudi hizo za Serikali ikiwa ni pamoja na kuwapa nafasi za viti maalum bungeni kwa wastani wa karibu asilimia 30 sasa, kuteuliwa kushika ngazi tofauti za uongozi serikalini, kupanua wigo wa idadi yao mashuleni na vyuoni, kuanzishwa kwa vyama mbalimbali vinavyoundwa na kuongozwa na wanawake kama TAMWA, TAULA, MEWATA, TGNP n.k, na kubwa zaidi kwa sasa ni kuanzishwa kwa vyama vya kuweka na kukopa(SACCOS), na taasisi lukuki zinazotoa mikopo kama FINCA, PRIDE, na hivi karibuni kuanzishwa kwa benki ya wanawake. Hizi zote ni juhudi nzuri.
Swali la kujiuliza pamoja na juhudi hizi zote, ni kwanini maisha ya wanawake wengi yanaendelea kuwa duni nap engine kuzolota? Ni lazima sababu ipo.Nikupe tu mfano wa wa Taasisi hizi za kutoa mikopo kwa wanawake. Sasa hivi wanawake wengi na hasa sehemu za mijini wamekuwa na mwamko mkubwa wa kujiunga katika vikundi vidogovidogo kwaajili ya mikopo. Na ni wengi wamechukua mikopo hiyo ila ni wangapi wamenufaika na mikopo hiyo ni wazi kuwa ni wachache mno. Wengi wameendelea kupiga “makitaim” na wengine hali zao kawa mbaya zaidi kuliko awali huku wakopeshaji wakiendelea kunawili na kuneemeka. Ndio maana nimeuita utumwa.
Mikopo wanayopewa ni midogo sana ambayo haiwezi kuwawezesha kumudu ushindani wa sasa wa kibiashara. Kutokana na kutokuwa na msingi wa biashara wegi wao wamekuwa wakipata kati ya shilingi elfu hamsini na laki moja na hamsini. Kutokana na kiasi hiki kidogo cha mikopo inawalazimu kujishughulisha na biashara ndogo ndogo kama uuzaji wa mbogamboga, matunda, mama lishe, kuuza nazi, mihogo na samaki. Biashara zao nyingi ni za kuigana, za msimu na zinazooza mapema hali inayofanya wasiwe na soko la uhakika, watumie muda mrefu na kupata faida ndogo.
Nilibahatika kukutana na mwanamke mmoja wa Tabata-Kisukuru, Dar-es-Salaam anaefanya kazi ya kukaanga na kuuza mihogo kwa mtaji wa pesa ya mkopo. Yeye huanza kuandaa biashara hiyo jioni kwa kufuata mihogo hiyo kwenye soko la Tandika au Buguruni. Kesho yake hukaanga na kuiuza na anasema hupata faida kati ya shilingi elfu mbili hadi nne soko likiwa zuri. “Huwa Napata elfu mbili hivi, na wakati mwingine elfu tatu au nne wateja wakiwa wengi” Faida hiyo ndogo anayopata inambidi atumie kidogo na sehemu nyingine aweke akiba kwa ajili ya marejesho ya mkopo. Ana watoto wawili wanaomtegemea pamoja na mume wake ambaye ni mgonjwa.
Mbali ya kupata mikopo midogo, akinamama hawa wanakabiliwa na changamoto nyingine kama ukosefu wa elimu ya biashara, utegemezi mkubwa katika familia zao, pamoja na RIBA kubwa ya mikopo hiyo midogo ambayo ni kati ya asilimia kumi na tano na ishirini kutegemeana na aina ya Taasisi husika. Wanapewa juma moja au mawili waanze kurejesha tangu siku wanayopewa mikopo hiyo. Ukilinganisha na aina ya biashara wanazofanya, muda huo ni mfupi sana kuanza kurejesha mkopo.
Hali hiyo huwalazimu wakinamama hao kuanza kurejesha pesa ile ile waliyokopeshwa. Na kutokana na makali ya maisha kwa walala hoi hawa sehemu nyingine ya mkopo huitumia kuhudumia familia zao. Katika mazingira haya wakina mama hukosa pesa za kurudisha mikopo yao baada ya muda mfupi. Lakini kwasababu pesa mkopo sio zao na ni lazima zirudishwe, wengi wamepambana na dhahama kubwa na kuishia kufilisiwa zaidi. Wengi wamenyang’anywa mali zao kama Luninga(TV), vitanda, magodoro, kabati, friji, sofa na nyingine nyingi. Maisha ya mama aliyeporwa mali hizi huwa mbaya kuliko awali. Je! hii ni kuboresha maisha yao?
Ni wazi kuwa hali za kimaisha za akinamama waliowengi zimezidi kudorora huku wengi wao wakikimbia makazi yao kwa kushindwa kurudisha mikopo, wengine wamekuwa na madeni lukuki kwa majirani, marafiki na ndugu zao eti kwasababu ya mikopo iliyolenga kuwanufaisha. Wengi wamegombana na waume zao hivyo kuhatarisha ndoa zao, na hayo yote kwa pamoja ni kukosa heshima, kuhatarisha usalama, amani na utulivu katika jamii wanayoishi. Labda niulize tena, hili ndio lengo lililokusudiwa? Jibu lipo wazi.
Tafakuri ya kina na hatua mahususi za lazima na za haraka ni sharti zichukuliwe kama kweli tunataka kuboresha maisha ya wanawake. Taasisi za mikopo hutoa elimu ya kurudisha mikopo ni si elimu ya ujariamali, hivyo kuna haja ya dhati kabisa ya kutoa elimu hiyo. Lakini pia mikopo iwe mikubwa inayokidhi mahitaji ya biashara shindani na endelevu. Pamoja na hayo yote swala kubwa na la msingi litabaki kuwa,
“NI NINI DHAMANA YA MIKOPO YA WANAWAKE HAWA WASIO NA MILKI YOYOTE?” Hilo ni la kutazamwa kwa macho yote.
No comments:
Post a Comment