
Mjumbe wa Bunge la Katiba, Mchungaji Peter Msigwa.
Ni vita ya maneno ya hoja kati ya Mchungaji Peter Msigwa na Askofu Mstaafu Donald Mtetemela Mjumbe
wa Bunge la Katiba, Mchungaji Petaer Msigwa amemvaa Askofu Donald
Mtetemela na kumtaka avae rasmi magwanda ya Chama cha Mapinduzi (CCM).Akizungumza
na gazeti hili, Msigwa ambaye pia ni Mbunge kupitia Chadema alisema
Askofu Mtetemela alionyesha upendeleo wa wazi kwa CCM alipokuwa
akichangia bungeni mjini Dodoma Alhamisi iliyopita.Katika
mchango wake, Askofu Mtetemela alikemea tabia ya wajumbe wa Bunge hilo
kuwakashifu waasisi wa Taifa aliosema wana heshima kubwa kwa jamii na
mbele za Mungu.
Hata
hivyo, Msigwa alisema:“ Askofu ameonyesha upendeleo wa wazi wazi
japokuwa anasema anasimamia katikati (hana upande kisiasa). Hakuona
kejeli, ubaguzi na matusi yaliyokuwa yakiendelea ndani ya Bunge?”
Mchungaji
Msigwa alisema yeye ni mchungaji lakini amejitokeza wazi kusimamia
Chadema tofauti na askofu huyo ambaye ameonyesha wazi upande
anaousimamia wa CCM, wakati awali walidhani ni mtu mwenye msimamo wa
kati.
“Mimi
sina ugomvi kama ameamua kuwa mwanasiasa kama mimi lakini awe wazi kwa
kusimama na kujionyesha wazi upande aliopo,”alisema.
Kauli ya Askofu Mtetemela
Katika
mchango wake, Askofu Mtetemela alilieleza kukerwa na kauli ya Profesa
Lipumba kuliita Bunge la Maalum la Katiba kuwa linafanana na kundi ovu
la Italahamwe.
“Nasikitika
kwamba sijaweza kumuona yeye binafsi Profesa Lipumba ili niweze
kumwambia masikitiko yangu, na naamini ni masikitiko ya wengine. Mshtuko
wangu ni kwamba alilinganisha Bunge hili na kundi la Intarahamwe la
Rwanda,” alisema.
Alibainisha
kwamba kihistoria inajulikana Intarahamwe ni wauaji, hivyo sio busara
kabisa kuwafananisha wajumbe wa Bunge Maalumu na kundi hilo.
“Hatuko
hapa kumuua mtu yeyote, kutuita sisi wauaji si jambo jema, ni baya
lakini pia kauli hiyo inaweza kufufua maumivu ya wenzetu wa Rwanda ambao
hawataki hali hiyo ijirudie tena katika nchi yao,” alisema.
Alieleza
kuwa kauli hiyo pia inaweza kuibua hisia tofauti hata kwa Serikali ya
Rwanda inayoweza kufikiri kuwa Tanzania inalifanyia mzaha jambo
lililowaumiza kwa kiasi kikubwa.