27 June, 2014

MAELEZO YA MH. ZITTO KABWE KUHUSU KAZI ZA KIGOMA ALL STARS/ LEGADUTIGITE KWA NSSF NA TANAPA

Maelezo yangu kuhusu kazi za Kigoma AllStars/LEKADUTIGITE kwa NSSF na TANAPA.
Leo tarehe 29 Mei, 2014 Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu Habari, Michezo, Vijana na Utamaduni amenituhumu kuhusika na kinachoitwa ufisadi katika Shirika la TANAPA na NSSF.
Nasikitika kwamba katika hali niliyonayo ya kumwuguza mama yangu naingizwa kwenye siasa za majitaka. Kwa sasa nitatoa maelezo kwa ufupi ili kuondoa upotoshaji.
Kampuni ya LekaDutigite inamilikiwa na wasanii 15 ambapo kila mmoja ana hisa 5% ambazo niliwalipia ili waweze kushirikiana katika kazi zao. Hisa 25% zilizobakia zinamilikiwa na kampuni ya Gombe Advisors ambayo ni kampuni isiyofanya faida (Company limited by guarantee) na haina maslahi yeyote ya kibiashara (not for profit company). Hivyo Mimi binafsi sina maslahi yeyote ya kifedha zaidi ya kuwasaidia wasanii hawa katika kazi zao mbalimbali.
Wasanii wa Kigoma AllStars wamefanya kazi na TANAPA na NSSF, kazi ambazo zinajulikana na zipo. Kwa upande wa TANAPA wasanii hawa waliandaa kazi ya kuitangaza Hifadhi ya Saadani na walilipwa. Kwa upande wa NSSF wasanii hao walitunga wimbo na video yake (http://m.youtube.com/watch?v=sMl8T-RkIdM ) na wimbo huo unatumika katika Shirika hilo.
Vile vile walifanya matamasha mbalimbali ya kuhamasisha watu kujiunga na NSSF. Wasanii wa Kigoma All Stars wote ni wanachama wa Mfuko huo.
Katika kazi zote hizi Mimi binafsi sijafaidika kwa namna yeyote ile kifedha. Kauli yeyote ya kujaribu kuonyesha kazi hizi za wasanii ni ufisadi ni kauli za kusikitisha na kukatisha tamaa kwa mtu ambaye anajaribu kusaidia wasanii kufaidika na kazi zao za sanaa.
Toka mwaka 2012 nilipoanza kujitokeza kusemea wasanii watu kadhaa wenye maslahi na tasnia hii wamekuwa wakinikatisha tamaa na hata wengine kuona nimewaingilia kazi zao.
Hivi sasa wasanii wa Kigoma AllStars ni wanahisa katika kampuni ya PERA Africa limited ili kufaidika na biashara ya miito ya simu. Yote haya nilifanya kwa uchungu nilionao kwa vijana wetu na sio kwa kutaka kufaidika kifedha. Nimeumizwa sana na tuhuma hizi za kuokoteza okoteza.
Inaniumiza zaidi kutokana na ukweli kwamba ninamwuguza mama yangu mzazi, kipindi ninachohitaji kutiwa moyo na kuombewa hata na maadui zangu kisiasa. Kipindi ambacho mama yangu yupo mahututi, tena mjumbe wa kamati kuu ya chama ambacho watoa tuhuma wanatoka, pole ninayopewa ndio hiyo. Hakuna namna ya kukosa ubinaadamu zaidi ya hivi.
Najua wajibu wangu ni kusimamia Mashirika ya Umma na nikiwa mpigania uwajibikaji nipo makini sana kuhakikisha sina mgongano wa maslahi katika mambo yangu. Ndio maana sina biashara yeyote ile ili kuhakikisha natimiza wajibu wangu kwa uadilifu mkubwa. Napata 'moral authority' ya kutaka uwajibikaji kwa sababu nafanya kazi zangu kwa misingi hiyo 'at arms length'.
Hivyo ninataka mara moja CAG afanye ukaguzi wa kazi za wasanii hao kwenye NSSF na TANAPA. Pia achunguze kama Gombe Advisors ( company limited by guarantee) ina maslahi yeyote ya kifedha katika kazi hizo za wasanii. Nataka pia Shirika la NSSF na TANAPA waweke wazi mchakato wa kazi zao na wasanii hawa kupitia LEKADUTIGITE Limited.
Zitto Kabwe
Mei 29, 2014
Dar Es Salaam.

No comments:

Post a Comment

UKIONDOA DIPLOMA, DEGREE AU PHD ULIYONAYO, KICHWA CHAKO KINABAKI NA NINI?

Horace Mann - Binadamu wa kwanza kugundua wazo la elimu Albert Einstein aliwahi kuulizwa akili ni nini? What is intellect? Akasema akili ni ...