14 August, 2014

MWALIMU NYERERE ANAJIGEUZA KABURINI KWAKE!


Na Daniel Mbega
BABA wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere atakuwa anajigeuza kaburini kwake. Ndivyo tunavyoweza kusema katika kipindi hiki cha miaka 15 ya kifo chake wakati tunaposhuhudia wanasiasa wanavyobishana namna ya ‘kuua’ Muungano – mwanawe pekee aliyesalia – huku tayari wakiwa wameigeuza Ikulu mahali pa biashara na ufisadi ukitamalaki.
Tangu tuliposhuhudia Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Ben Mkapa na mkewe wakianzisha ujasiriamali wakiwa Ikulu na kujiuzia mashirika ya umma huku mengi yakiuzwa ama kubinafsishwa, hali imekuwa mbaya kila sekta na watendaji wengi wameamua ‘kuchukua vyao mapema’, hivyo kuifanya Tanzania inuke rushwa na ufisadi.
Ni mageuzi, lakini vikumbo hivi havikuwa na kasi namna hii, na hata kama ilikuwepo, basi ilikuwa na staha. Kinashuhudiwa hivi sasa ni ubabe, jeuri na mambo mengine kama hayo katika kuidai Tanganyika ndani ya Muungano na wakati huo huo wengine wakipinga muundo wa serikali tatu.
Wapo wenye nia ya dhati kulizungumzia suala hili: Wale wanaotaka muundo wa serikali tatu (ikiwemo ya Tanganyika) wana mambo yao - wengine wanataka ziwepo serikali nyingi ili waweze kupata vyeo vya kisiasa. Wananchi wanatumiwa kama daraja tu la 'kuhalalisha' hoja zao, hakuna kingine!
Wanaong'ang'ana na serikali mbili - hasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) - nao wanahofia kuwepo kwa serikali tatu kwa vile nguvu ya kulishika dola itapungua. Tena yawezekana wasirudi madarakani katika mfumo mpya.
Kikubwa zaidi ni kwamba, hofu ya kuvunjika kwa Muungano iko dhahiri kwa sababu hata Wazanzibari wenyewe - ambao kimsingi waliukataa Muungano tangu mwaka 1992 - wamesimama kidete wakiidai Tanganyika na wanapinga mbinja kweli kweli kuhakikisha serikali ya Tanganyika inarejea - halafu waingie kwenye Muungano wa Mkataba!
Lakini tunapoelekea kuazimisha miaka 15 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, ni dhahiri makundi mengi yamejitokeza na maono tofauti katika suala zima la Muungano – ambao yeye aliamua kuingilia kati na kuizima hoja ya Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano iliyotolewa na Njelula Mulugale Kasaka mwaka 1993.
Tuliokuwepo tunakumbuka mambo yaliyotokea, na kwa vijana wa sasa ni vyema kuwakumbusha tu kwamba Mwalimu alilipinga wazo hilo kwa nguvu zake zote na kusema Serikali Tatu siyo sera za chama.
Hata alipowauliza viongozi waliokuwa wakidai serikali tatu, walishindwa kujibu. Yeye akasema katika utenzi wake:
Ati kuuliza watu
"Serikali ziwe tatu?"
Ni swali gumu ajabu,
Wanashindwa kulijibu

Tena ati wanasema
Walihofia gharama
Ila serikali tatu
Gharama zake si kitu

Baadhi ya waliopata ujasiri walisema kwamba walikuwa tayari kuunga mkono serikali tatu kwa sababu ni Azimio la Bunge, na kamwe hawawezi kulipinga Bunge la chama chao. Lakini Mwalimu akasema:
Sasa wana hoja nyemi,
Ya kutaka kujihami,
Ni hoja ya kudanganya,
Na kutaka kujiponya

Wanasema viongozi,
Ati Chama hakiwezi,
Kukataa sera hino,
Ya kuvunja Muungano.

Ati serikali mbili,
Sasa ni sera batili;
Maana bunge la watu,
Limetaka ziwe tatu

Chama kisipobadili,
Hiyo ni sera batili,
Kitapinga Bunge lake
Pia Serikali yake.

Na hilo, wanatwambia,
Ni kinyume na kinyume cha sharia,
Siyo halali kwa chama,
Kupinga Bunge la Umma!

Kale twali tukiimba,
Wimbo huu wa kasumba;
Furaha kuu, furaha kuu!
Mikono chini, miguu juu
Twaenda machi, twaenda machi
Twaenda machi, furaha kuu

Hizo ni hoja za wakuu,
Za miguu kuwa juu,
Na vichwa vikawa chini,
Wabunge tahadharini.

Siyo zenu hoja hizi,
Ni hoja za viongozi,
Msizipe uhalali,
Kwani ni hoja batili

Wabunge wa umma,
asili yao ni chama,
wale wa kuchaguliwa,
na walioteuliwa

Sera zao Bungeni,
Zatokana na ilani,
Ya uchaguzi wa nyuma,
Ulofanywa na kauma,
Na wala si sera zao,
Ni sera za chama chao,
Na sababu ya ilani,
Ni kutafuta idhini,
Ya wananchi wenzenu,
Wakubali sera zenu.

Mkishapata kibali,
Mtaunda serikali,
Mtekeleze Bungeni,
Sera zenu, kwa idhini;
Na wale walowatuma,
Ni chama pamwe na Umma.

Lakini tangu mchakato wa kutafuta Katiba Mpya umeanza mwaka 2012, tumeshuhudia mambo mengi yakitokea. Makundi kadhaa yametoa maoni yao na ndipo ilipoibuka hoja ya kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, ambayo Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba iliyachukua na kuyaweka kwenye Rasimu zote mbili.
Jinsi ilivyopata nguvu hoja hiyo tangu awali, na jinsi wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba – hasa wa vyama vya upinzani walivyojitenga kwa kusisitiza kwamba lazima serikali ya Tanganyika ipite kama ilivyopendekezwa, huku wale wa Chama cha Mapinduzi wakipigania kwa nguvu zote kuhakikisha zinabaki serikali mbili – ni wao pekee ndio wanaojua.
Naam, tumeshuhudia matusi, kejeli, na bezo nyingi kwa kila upande, wajumbe hao wakitaka kutetea hoja zao kwa nguvu hali iliyowafanya wale wanaotaka serikali tatu, ambao waliunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakaamua kususia Bunge hilo.
Wajumbe kutoka Kundi la Walio Wengi (CCM & Co.) bado wanasimama kwenye maneno ya Mwalimu Nyerere pale aliposema:
Ndiyo ma’na na ikasemwa,
Wabunge wakishatumwa,
Wana kauli ya mwisho,
Wasikubali vitisho.

Wameshatumwa na chama,
Kwa idhini ya kauma,
Atowapinga ni nani,
Ila chama pinzani?

Na kwa chama kipinzani,
Kiloshindwa uwanjani,
Kupitisha sera zake,
Kupinga ni haki yake.

Lakini vikumbo vyote hivi vinaleta tafsiri moja tu; kwamba yawezekana Mwalimu Nyerere anageuka kaburini kwake, ndiyo maana kuna mtikisiko mkubwa huko bungeni na mitaani.
Je, Katiba Mpya itapatikana kama ilivyopangwa? Nini hatma ya mvutano huu unaoendelea? Itakuwa aibu kwa Tanzania iliyosaidia harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika kushindwa kutatua matatizo yake yenyewe, hasa suala nyeti kama Katiba.
Iringa,
0656-331974

No comments:

Post a Comment

UKIONDOA DIPLOMA, DEGREE AU PHD ULIYONAYO, KICHWA CHAKO KINABAKI NA NINI?

Horace Mann - Binadamu wa kwanza kugundua wazo la elimu Albert Einstein aliwahi kuulizwa akili ni nini? What is intellect? Akasema akili ni ...