17 October, 2014

WERAAAWERAAAA.....WAPINZANI WANUIA KUSIMAMISHA MGOMBEA MMOJA WA URAIS 2015


MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa. Ibrahimu Lipumba, amevitaka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kumsimamisha mgombea mmoja wa urais ambaye atakishinda Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi mkuu mwakani.
 
Lipumba alitoa kauli hiyo juzi wakati akiwahutubia maelfu ya wananchi wa mkoa wa Mtwara na vitongoji vyake waliohudhuria mkutano huo uliofanyika kwenye uwanja wa Mashujaa, mkoani hapa.
 
Alisema ili kuishinda CCM, lazima waungane katika uchaguzi mkuu mwakani na kusisitiza kama kweli wanahitaji mabadiliko, suala la mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais, ubunge, udiwani hadi vitongoji, haliepukiki.
 
“Sisi tunaounda UKAWA lazima tushirikiane ili tuweze kumsimamisha mgombea mmoja wa urais ambaye atakubalika na wananchi wa kada zote. Tukiungana ninaamini tunaweza kuishindwa CCM kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao.
 
“….Wananchi wa Mtwara na Tanzania kwa ujumla wakati umefika sasa wa kusema basi tunataka mabadiliko ya kweli na wenye kufanya mabadiliko hayo ni nyinyi wenyewe,” alisema Lipumba huku akishangiliwa na malfu ya wananchi waliohudhuria.
 
Aliwataka watanzania kuonyesha mapinduzi ya kweli katika kuwatetea wananchi ambao alisema wamechoka kuonewa, kupigwa, kuteswa, kunyanyaswa kwenye nchi yao na hata kuporwa mali zao na kuwapa kipaumbele wawekezaji badala ya wazawa.
 
Alisema UKAWA lazima ichukue nchi kutoka mikononi mwa mafisadi wasiowajali wapiga kura wao na badala yake wamekuwa wabinafsi wa kujali maslahi yao.
 
Lipumba, alienda mbali zaidi kwa kusema UKAWA wanahitaji kuungana pia hata kwenye majimbo kwa kumsimamisha mgombea ubunge mmoja.
 
“Viongozi wenzangu, lazima tuingie katika mapambano ya kuwatetea wananchi wetu kutoka katika mikono ya mafisadi, katika utaratibu wa kuweka wabunge pia na hili tuungane, kwa mfano kama CUF wanapendwa Mtwara Mjini, basi waweke mgombea wa CUF na vyama vingine waunge mkono au CHADEMA ina nguvu Arusha basi wasimamishe mgombe ubunge wa CHADEMA na vyama vingine viunge mkono katika kumpigia kampeni mgombea mbunge wa CHADEMA,” alisema Lipumba na kuongeza.
 
“Na hata NCCR-Mageuzi kama ina nguvu Kasulu, basi vyama vingine vifanye hivyo hivyo katika kumpigia kampeni mgombea huyo wa NCCR-Mageuzi na vyama vingine vya upinzani kama vina nguvu sehemu nyingine lazima tushirikiane kwa pamoja, lengo likiwa kuleta mabadiliko ya kweli katika kushika dola,” alisema.
 
Aliwataka wananchi wa Mtwara na vitongoji vyake kujiandikisha kwa wingi kwenye Daftari la Kudumu la wapiga kura ili waweze kushiriki kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao unatarajia kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
 
“Kama kweli Mtwara mna uchungu na mlichofanyiwa na serikali ya CCM ya kupigwa na wanajeshi hadi wengine kupelekwa Naliendele kuteswa, nawaomba mfanye mapinduzi ya kweli na tunaanza na uchaguzi za serikali za mitaa kwa kuwaonyesha kwamba hamkutendewa haki.
 
Kwa upande wake, Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Baruani (CUF), aliwapa pole wananchi wa Mtwara kwa yote yaliyotokea mwaka jana wakati wakidai haki yao ya kutaka kujua faida watakayopata kutokana na gesi iliyogundulika mkoani humo.
 
“Ila wananchi nawaomba hasira yenu ionyesheni katika kupiga kura, msikichague chama ambacho akithamini wananchi wake na mwisho wa siku kinawatesa na kuwanyanyasa kwenye nchi yenu. Uonyesheni mabadiliko ya kweli kwenye uchaguzi,” alisema Baruani.

No comments:

Post a Comment

UKIONDOA DIPLOMA, DEGREE AU PHD ULIYONAYO, KICHWA CHAKO KINABAKI NA NINI?

Horace Mann - Binadamu wa kwanza kugundua wazo la elimu Albert Einstein aliwahi kuulizwa akili ni nini? What is intellect? Akasema akili ni ...