Padri John Wootherspoon (kulia) akizungumza na mama wa mmoja wa wafungwa wa Kitanzania walioko Hong Kong katika hoteli moja jijini Dar es Salaam.
Padri John Wootherspoon, raia wa Australia ameeleza mikasa na visa mbalimbali vinavyohusiana na biashara ya dawa za kulevya, vikiwamo vitisho na jinsi alivyozungumza na familia za wafungwa wa Kitanzania waliokamatwa na dawa za kulevya na kufungwa Hong Kong. Hong Kong inatumiwa na Watanzania kama njia ya kupitisha dawa za kulevya kwenda China na nchi nyingine za mashariki ya mbali. Wootherspoon, Padri wa Kanisa Katoliki ambaye kazi yake ni kuwatembelea wafungwa katika magereza, kuwafariji na kueneza neno la Mungu, amesema tangu alipofika nchini amekuwa akiwatahadharishwa kuwa makini na watu wanaofanyabiashara ya dawa za kulevya. “Nimeambiwa mara nyingi kuwa wanaweza kunitafuta na kunidhuru, lakini sijaona chochote mpaka sasa na siogopi kwa kuwa Mungu ananilinda,” alisema. Mwandishi wa Mwananchi alikutana na Padri Wootherspoon wakati anazitafuta familia zaidi ya 30 za Watanzania waliofungwa Hong Kong baada ya kuwasiliana naye kwa njia ya barua pepe tangu Novemba mwaka jana alipokuwa akipanga safari ya kuja nchini. Padri huyo alizungumza na wanafamilia wa wafungwa hao ambao waliandika ujumbe mfupi kwa ndugu zao kwa kuwa kila mfungwa aliyeandika ujumbe aliweka namba ya simu ya ndugu yake. “Niliwapa kitabu kidogo hiki kila mmoja alikitumia kuandika ujumbe mfupi na namba ya simu, wafungwa wote hawakupata nafasi ya kuandika kwa sababu wapo zaidi ya 130. Padri huyo alifafanua kuwa ili kusafirisha dawa hizo Watanzania hao humeza kete hizo na mtu mmoja anaweza kumeza hadi 90 za heroini (sawa na kilo 1.5). Miongoni mwa wafungwa walioleta ujumbe wao ni pamoja na msichana maarufu katika muziki wa Bongo Flevya, Binti Kiziwa au Sandra Khan. Sababu kubwa ya kusafirisha dawa za kulevya ambayo wafungwa hao walimweleza Padri Wootherspoon ni umaskini na tamaa ya fedha za haraka. “Nilichogundua ni kuwa wengi wameshawishiwa bila kujua madhara, walidanganywa kuwa ni rahisi zaidi kupenya katika mipaka,” alisema. Kadhalika alieleza kuwa wapo Watanzania wengi China ambao ameshindwa kuonana nao kwa kuwa mtu aliyekamatwa na dawa za kulevya nchi hiyo huhukumiwa kunyongwa. “Niliwaruhusu kuandika barua ili wawakanye Watanzania wengine wasibebe dawa za kulevya na hizo,” alisema huku akionyesha barua hizo. Agawa fedha kwa familia Baada ya kukutana na familia za wafungwa hao, Padre Wootherspoon aligundua kuwa nyingi zinaishi katika hali ya umaskini, jambo ambalo lilimlazimu kutoa fedha zake ili kuzisaidia. Katika ziara hiyo, Padri huyo alitoa zaidi ya Sh6 milioni alizokuwa nazo na nyingine kutoka kwa wasamaria wanaoishi Hong Kong. Familia zilizosaidiwa fedha nyingi zaidi ni za watoto wa wafungwa wenye mahitaji ya ada, wazazi wanaoumwa na wake wenye watoto wachanga. Kwa mfano, mfungwa ambaye alikiri kuwa anaishi na Virusi vya Ukimwi aliandika katika barua kuwa mama yake naye anaishi na VVU wakati amemwachia mtoto mdogo. Akutana na Nzowa Akiwa nchini, Padri Wootherspoon alikutana na Kamishna wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, ACP Godfrey Nzowa na kuzungumza naye kuhusu vita ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi. Katika mazungumzo yao, Wootherspoon alimtaka Nzowa aende kuonana na wafungwa hao ili wamweleze siri nzito za biashara hiyo. “Ni vyema ukaonane nao kwa sababu wanahitaji faraja na watakupa mengi wanayoyajua kuhusu biashara hii. Kwa sasa wanajutia walichokifanya, hivyo watakuwa radhi kukupa ushirikiano,” alisema Padri Wootherspoon. Hata hivyo, Nzowa alipinga uamuzi wa wafungwa hao kutaja majina ya magwiji wa biashara ya dawa za kulevya katika barua na kuweka katika tovuti kwa kuwa wanahatarisha maisha yao badala yake wangewasiliana naye. Padri Wootherspoon alizaliwa miaka 68 iliyopita, baada ya kupata upadri alihamia Hong Kong ambako amefanya kazi kwa miaka 25 akiwahudumia wafungwa.
No comments:
Post a Comment