15 January, 2015

UKATILI NA UNYANYASAJI HUU NI AIBU KWA TAIFA!



Katika kipindi cha hivi karibuni, kumejitokeza vitendo vingi vya kuwadhalilisha watoto kwa kuwabaka, kuwanajisi, kuwalawiti, kuwatesa, kuwaua bila hatia kutokana tu na sababu zisizo na msingi zikiwemo za ushirikina na kutafuta utajiri, vitendo ambavyo ni vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Miaka minne iliyopita, kulijitokeza wimbi la vitendo vya mauaji kwa walemavu wa ngozi, hasa kwa mikoa ya Kaskazini, mauaji ambayo yalishinikizwa na imani za kishirikina. Kutokana na jitihada za polisi pamoja na jamii iliyokasirishwa na vitendo hivyo, ilisaidia kupunguza kasi ya mauaji ya albino hao, ingawa matukio kama hayo yameripotiwa kutokea tena hivi karibuni mkoani Katavi, na pia mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino) Pendo Immanuel aliibwa na watu wasiojulikana katika kijiji cha Ndami wilayani Kwimba mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana. Mwaka jana, mtoto Nasra Rashid mwenye umri wa miaka minne, aligundulika kufichwa katika boksi katika mtaa mmoja mjini Morogoro, ameishi ndani ya boksi hilo tangu akiwa na umri wa miezi tisa, taarifa za kuwepo kwa mateso ya aina hiyo kwa mtoto huyo ziliibuliwa na wasamaria wema baada ya kupewa taarifa kuwa ndani ya nyumba ya Mariam Said kulikuwa na mtoto aliyefichwa ndani ya boksi. Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari (TAMWA), Valerie Msoka aliwahi kuvipongeza vyombo vya habari kwa kutoa ushirikiano na uandishi wa habari za ukatili wa kijinsia ambao umeonesha mafanikio kwa sasa. Mama Msoka alitoa kauli hiyo wakati akiwasilisha taarifa ya matokeo ya utafiti wa mradi wa kutokomeza ukatili na unyanyasaji kwa wanawake na watoto jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi wa TAMWA alisema kumekuwepo na ongezeko la habari za unyanyasaji kuandikwa kwenye magazeti mbalimbali, akatoa wito nakuwaomba waandishi wa habari waongeze juhudi za uandishi wa habari za ukatili unaoathiri ustawi wa jamii yetu. Mashirika na taasisi mbalimbali za haki za watoto zimeguswa sana na tukio la mateso aliyoyapata mtoto aliyeishi ndani ya boksi kwa muda wote huo, hali iliyomsababishia ulemavu wa mikono pamoja na miguu. Mkurugenzi wa Wildaf nchini, Dk. Judith Odunga alitoa maagizo kwa mwakilishi wa kituo cha Morogoro Flora Masoyi kufuatilia tukio la mtoto huyo, ingawa kwa bahati mbaya baadaye mtoto alifariki dunia. Tukio jingine la kusikitisha lililotokea kwa mganga wa jadi Mujingwa John aliyemkata mtoto sehemu za siri na kuzibanika, tukio hilo la kutisha lilitokea kijiji cha Matera, kata ya Nyangunge wilaya ya Magu mkoani Mwanza ambako lilimkumba mwanafunzi wa darasa la kwanza, Fausta Geofrey mwenye umri wa miaka minane. Mtoto huyo alikatwa mikono yote, masikio, sehemu za siri, na mganga huyo, ambapo viungo hivyo alivibanika ili vikauke aweze kutengenezea dawa za kienyeji kwa wateja wake. Vitendo vya kikatili viliendelea kushamiri ambapo wakati mmoja, Jeshi la Polisi mkoani Morogoro lilimshikilia mlinzi mmoja Mohamed Mgende mwenye umri wa miaka 59, anayeishi maeneo ya Msamvu kwa tuhuma za kumbaka binti wa miaka 12, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano, ilidhihirika kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa na tabia ya kumdhalilisha binti huyo kwa kumbaka kila mara kwa ujira wa chips na kumpa 200/-. Yapo matukio mengi mengine ambayo yanahusu udhalilishwaji watoto ambayo huishia katika suluhu za kifamilia kwa misingi ya kukwepa aibu katika jamii. Watoto wamekuwa wakitendewa vitendo vibaya bila ya jamii kuchukua hatua za kisheria kwa visingizio vya kulinda heshima ya wazazi pamoja na kujenga mahusiano mema miongoni mwa familia zinazotuhumiana, suala hilo kwa hakika limerudisha nyuma jitihada za kukomesha ukatili dhidi ya watoto nchini. Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) kimekuwa kikiwahamasisha wananchi kutoa habari za unyanyasaji katika ngazi mbalimbali ili jamii ielewe namna ya kutumia sheria zilizopo za kupambana na watuhumiwa wa vitendo hivyo. Umaskini uliokithiri miongoni mwa jamii yetu ni moja ya vyanzo vinavyorudisha nyuma jitihada za kupambana na unyanyasaji na ukatili kwa watoto, mzazi anapotambua kuwa mtoto wake katendewa vitendo vibaya, na akaahidiwa malipo kufidia udhalilishwaji aliofanyiwa mtoto, huwa radhi kuliko kufuatilia hatua za kisheria. Zipo sheria za mwaka 2009, Sura ya pili kipengele cha 5 (1), 5 (2) na 13 zinazolinda haki za watoto ambapo pamoja na mambo mengine vinatetea kwa undani haki na ustawi wa mtoto na kumueleza mtoto ni nani na mambo gani anapaswa kufanyiwa. Kutokana na kitendo cha kumficha mtoto ndani ya boksi, Chama cha Wanahabari Tanzania (Tamwa) kilisema serikali inapaswa kukishughulikia kwa kuangalia sheria zinazomlinda mtoto za mwaka 2009.

No comments:

Post a Comment

UKIONDOA DIPLOMA, DEGREE AU PHD ULIYONAYO, KICHWA CHAKO KINABAKI NA NINI?

Horace Mann - Binadamu wa kwanza kugundua wazo la elimu Albert Einstein aliwahi kuulizwa akili ni nini? What is intellect? Akasema akili ni ...