Mhudumu wa afya akiandaa dawa kuweka katika bomba la sindano tayari kumchoma mgonjwa.Picha ya Maktaba.
Mwili wa mtoto Imran Mwerangi aliyefariki dunia katika Hospitali ya Apollo, India alikokuwa amepelekwa kwa matibabu, unatarajiwa kuwasili leo.
Imran (6), ambaye alipooza mwili mzima na kupata mtindio wa ubongo baada ya kudungwa sindano katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alifariki dunia saa 11.45 alfajiri ya Mei 8.
Mtoto huyo ambaye alikuwa akipelekwa katika hospitali hiyo, kila baada ya miezi sita kwa ajili ya uchunguzi wa maendeleo ya afya yake kutokana na athari za sindani hiyo, alifikishwa huko Jumatano iliyopita baada ya hali ya afya yake kubadilika na kuvimba mwili mzima. Alifariki dunia wakati madaktari wakihangaika kupata mishipa ya damu kwa ajili ya vipimo.
Baba wa marehemu, Iddy Mwerangi alisema jana kuwa taratibu za kuurudisha mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi zimefanywa na Ubalozi wa Tanzania nchini India na kwamba mwili huo unatarajiwa kuwasili.
Mwerangi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), alisema wakati mwili wa marehemu ukitarajiwa kuwasili jioni, mama wa marehemu, Amina Machuro, atawasili mchana. “Baada ya mwili huo kuwasili nchini muda huo, moja kwa moja tutaanza safari kuelekea Mdaula, (Morogoro) kwa ajili ya mazishi,” alisema Mwerangi.
Imran alidungwa sindano hiyo, Julai 29, 2011 alipopelekwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu ya upasuaji mdogo wa nyama zilizokuwa zimeota katika njia ya hewa, puani.
Baada ya kudungwa alitelekezwa ICU bila matibabu kwa zaidi ya miezi sita, akipumua kwa msaada wa mashine, huku ikimlazimu mama yake kumgeuzageuza kila baada ya saa mbili kwa kipindi chote hicho.
Licha ya kutokupata matibabu kwa muda wote huo, juhudi za wazazi wake kuomba rufaa ili apelekwe nje kwa uchunguzi zaidi hazikuzaa matunda hadi gazeti hili lilipoibua taarifa za mkasa wa mtoto huyo Februari 2012 na kuulazimu uongozi wa hospitali hiyo kuunda jopo la madaktari bingwa kuchunguza tukio hilo.
Baada ya ripoti ya uchunguzi huo, ndipo mtoto huyo aliposafirishwa kwenda kutibiwa India.
Aliruhusiwa kurejea nyumbani baada ya madaktari kuridhishwa na maendeleo ya afya yake, akitakiwa kurudi Appolo kila baada ya miezi sita kwa ajili ya uchunguzi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment