Story ya wanawake wa Rombo kukodi wanaume Kenya kuwaridhisha kimapenzi yatinga bungeni, wanaume wataka waombwe radhi
Habari iliyoandikwa kwenye gazeti la
Mwananchi juzi yenye kichwa cha habari ‘Wanawake wa Rombo wakodi wanaume
kutoka Kenya’ imeibukia bungeni leo.
Habari hiyo iliandikwa kutokana na kauli
aliyoitoa mkuu wa wilaya ya Rombo, Lembris Kipuyo, aliyedai kuwa
kutokana na wanaume wa wilaya hiyo kuwa walevi wa kutupa, wake zao
wamekuwa wakikodi wanaume kutoka Kenya ili kuwaridhisha kimapenzi.
“Tatizo la ulevi wilayani Rombo na
matumizi ya pombe zisizokuwa na viwango ni kubwa sana na linahitaji
nguvu kulikabili,” alisema mkuu huyo wa wilaya. “Imefikia wakati wanaume
wengi wanashindwa kumudu kufanya tendo la ndoa na kuwalazimu kukodi
wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya kwaajili ya tendo hilo.”
Akiuliza swali kwa Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA), amesema habari hiyo
imesababisha madhara makubwa katika jimbo lake.
Selesani amesema habari hiyo imewadhalilisha wanaume wa Rombo na wanaiomba serikali iwaombe radhi kwa kilichoandikwa.
Amesema kutokana na habari hiyo wanaume
wengi wameanza kuwatilia mashaka wake zao kuwa huenda ‘wamekuwa
wakichepuka’ na wakenya na hivyo kusababisha maelewano hafifu ndani ya
ndoa.
Akijibu swali hilo, mheshimiwa Pinda alisema binafsi hajaisikia taarifa hiyo kwahiyo hatoweza kuomba radhi hadi pale
atakapolifuatilia.
No comments:
Post a Comment