Dar es Salaam. Ndivyo alivyosema na bila shaka ndivyo anavyoamini Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, lakini kauli ambazo amekuwa akizitoa
tangu kuanza kwa mbio za urais zinamuweka katika hali ngumu Mwenyekiti
wake, Rais Jakaya Kikwete.
Lowassa alirudia moja ya kauli hizo juzi alipokuwa Dar es Salaam
kuendelea na kazi ya kutafuta wadhamini aliposisitiza kauli ya Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa “Watanzania wanataka mabadiliko,
wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje,” akisisitiza kuwa yeye ndiye
anayeweza kuleta mabadiliko hayo.
Mbunge huyo wa Monduli ametoa kauli hizo kabla ya vikao vya juu vya
kufanya uamuzi wa mgombea urais wa CCM vitakavyoongozwa na Rais Kikwete.
Vikao hivyo vitaanza Julai 8.
Tayari makada 42 wamejitokeza kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya chama
hicho kikongwe kugombea urais na kutoa ahadi mbalimbali, lakini Lowassa,
ambaye amekuwa akipata wadhamini wengi kuliko makada wengine, ndiye
ambaye ametoa kauli zinazomuweka Kikwete kwenye hali ngumu.
Tangu alipoanza kuzungumzia urais kwenye kikao cha kwanza na wahariri
Mei 25 mjini Dodoma, Lowassa amekuwa akitoa kauli kadhaa katika mikoa
mbalimbali nchini, akianzia Arusha ambako alitangaza nia ya kugombea
urais kwa tiketi ya CCM na baadaye kwenye harakati za kusaka wadhamini.
Asiyenipenda ahame CCM
Akijibu swali kwamba anaweza kuhama chama iwapo jina lake litakatwa
kwenye mchakato wa ndani ya CCM, Lowassa alieleza jinsi alivyokitumikia
chama na imani yake.
“Sina mpango wa kuhama chama changu, sina Plan B. Mimi ni Plan A tu.
Tangu nimalize chuo kikuu mwaka 1977, nimekuwa mwana-CCM. Sijafanya kazi
nje ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na
nilipohamishiwa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha. Maisha yangu
yote ni CCM,” alisema Lowassa.
“Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiyo ahame, siyo mimi.”
Safari hii JK ataniunga mkono
Akihutubia maelfu ya wananchi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mei 30
wakati akitiania, Lowassa alielezea tukio la kuchukua fomu za kuomba
ridhaa ya CCM kuwania urais mwaka 1995 wakati alipofanya mkutano na
waandishi wa habari akiwa pamoja na Kikwete, ambaye pia alichukua fomu
hizo.
“Wakati ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Pamoja tulikwenda kuchukua
fomu na baadaye kwa pamoja tukazungumza na waandishi wa habari. Tulileta
hamasa kubwa pale tulipofanya jambo ambalo halikuzoeleka kwa Watanzania
kwa kutangaza kwamba yeyote atakayepita kati yetu, mwenzake ambaye
hangefanikiwa angemuunga mkono mwingine,” alisema Lowassa na kuongeza
kuwa wakati ule alimuunga mkono Kikwete...“Natarajia safari hii, Kikwete
ataniunga mkono.”
waka huo, Kikwete alishindwa na Benjamin Mkapa ambaye baadaye akawa Rais
wa Serikali ya Awamu ya Tatu. Mwaka 2005, Lowassa hakuchukua fomu na
badala yake alimuunga mkono Kikwete aliyeshinda na mbunge huyo wa
Monduli kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Pengine kauli hiyo ya Lowassa kutaka amuunge mkono ndiyo iliyosababisha
Rais Kikwete kutupiwa swali na mwanadiplomasia wa Marekani Juni 9 wakati
akizungumza na Jumuiya ya Watanzania waishio Uholanzi katika hoteli ya
Chawnie Plaza. Rais Kikwete alijibu kuwa hana mtu wake na kwamba wote ni
wagombea wake, na kama ni suala la kuchagua, ana kura moja tu kama
wajumbe wengine.
Mabadiliko aliyotabiri Nyerere
Akiwa mjini Iringa Juni 20, Lowassa alitumia kauli hiyo ya Nyerere kuhusu mabadiliko ndani na nje ya CCM.
“Baba wa Taifa alisema kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko na
wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” alisema Lowassa.
“Huu ni wakati wa mabadiliko. CCM ikijipanga inaweza kuleta mabadiliko
na mtu wa kuleta mabadiliko hayo ni mimi,” alisema Lowassa kwenye Uwanja
wa Samora mjini Iringa.
Pia aliwaambia wahariri mjini Dodoma kuwa hawezi kuondoka CCM na kama
kuna watu wanadhani hivyo, waondoke wao. Alikuwa akijibu swali kama
atakuwa tayari kuondoka CCM iwapo ataenguliwa kwenye mchujo wa wagombea
urais.
Hakuna wa kumkata jina
Juni 22, akizungumza mara baada ya kuwasili mkoani Ruvuma alisema
hatarajii jina lake kukatwa katika vikao vya CCM vitakavyoketi kumteua
mwanasiasa atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro
cha urais.
“Nimekuwa mwanaCCM tangu mwaka 1977 nilipomaliza chuo kikuu, sijawahi
kufanya kazi nje ya CCM hivyo nakijua chama na hakuna mgombea
atakayeweza kuvunja rekodi ya utendaji wangu katika chama, sasa leo
anayetaka kukata jina langu anatoka wapi? Anakata kwa sababu gani? Sioni
kosa la kukatwa jina na Watanzania hawaoni, kwa hiyo msiwe na wasiwasi
jina litarudi tu,” alisema Lowassa.
Anayemtuhumu kwa ufisadi amtaje
Siku ya kuchukua fomu Juni 5, Lowassa alijibu kwa kifupi maswali ya
wanahabari na kusema kama kuna mtu ana ushahidi wa tuhuma za ufisadi
dhidi yake amtaje jina.
“Kama hawakunitaja hawakunihusisha… Mtu anayejiamini aseme na anitaje.
Nachoka na siasa za tuhuma, hatupimi viongozi kwa rekodi za matusi ila
tu zijengwe hoja.
CCM ikijipanga itashinda
Juni 25, akiwa mjini Babati kutafuta wadhamini, Lowassa alisema iwapo
CCM itajipanga vizuri, ikamaliza migogoro na kujiamini, itashinda mapema
katika uchaguzi.
“Tukijipanga vizuri, tukajiamini tukaacha magomvi katika umoja wetu huu, tutashinda uchaguzi mapema dhidi ya watani wetu.”
Kwa kujipanga, Lowassa alikuwa akimaanisha kumteua yeye kugombea urais
kwa tiketi ya CCM, akisema kufanya hivyo kutamaliza uchaguzi mapema.
Alichokisema Dar
Akiwa Dar es Salaam juzi kusaka wadhamini alirejea kauli ya Mwalimu
Nyerere ya mwaka 1995 kwamba mabadiliko yasipopatikana ndani ya CCM,
yatatafutwa nje ya chama hicho.
Kutokana na kauli hizo ni wazi kuwa rais Kikwete atakuwa katika mtihani
mzito wakati atakapokuwa akiendesha vikao vya chama hicho vya kupata
mgombea urais.
Kwa mujibu wa ratiba za CCM, kikao kitakachoanza kitakuwa na Usalama na
Maadili kitakachofanyika Julai 8 na kufuatiwa na Kamati Kuu Julai 9
ambayo itawachuja wagombea hao 42 na kubaki watano ambao majina yao
yatawasilishwa Halmashauri Kuu (NEC) Julai 10 kuchuja wagombea hao na
kubaki watatu watakaopigiwa kura na mkutano mkuu kumpata mmoja. Mkutano
mkuu utafanyika Julai 11 na 12.
Vikao vyote isipokuwa cha Usalama na Maadili vitaongozwa na Rais Kikwete.
Jambo jingine linaloonekana kukitesa chama hicho katika kupitisha
mgombea ni idadi kubwa ya wana-CCM wanaojitokeza kumdhamini waziri mkuu
huyo wa zamani.
Kwa mujibu wa taratibu za chama hicho kila mgombea urais anatakiwa
kudhaminiwa na wanachama 30 katika mikoa 15 nchini ili kufikisha idadi
ya wadhamini 450, lakini Lowassa amekuwa akipata wanachama hadi 50,000
wanaotaka kumdhamini katika baadhi ya mikoa.
Makada, wasomi wazungumzia kauli
Pius Msekwa alisema chama kikongwe kama CCM hakiwezi kutishika kwa kauli
kama hizo ambazo zinaweza kuwa na tafsiri tofauti kwa wananchi wa
kawaida ambao hawafahamu taratibu za chama wanaoweza kuamini kuna watu
wanaonewa.
Alisema kwa taratibu za chama, mgombea anatakiwa kueleza sera zake
atakachowafanyia wananchi, lakini akiwa anatoa kauli za vitisho anakuwa
kero kwa wanaomsikiliza kwani haziwasaidii.
“Sidhani kama ni kauli nzuri, kinachotakiwa wagombea wanadi sera zao na
wasubiri kupitishwa na kamati itakayokaa kwa ajili hiyo badala ya
kutamka kauli zisizokuwa na tija wala faida kwa mwananchi wa kawaida,
”alisema Msekwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Frank Tilya alisema
ameshangazwa na tabia hiyo ya wagombea wa CCM iliyoibuka kabla ya
taratibu za uchaguzi kutangazwa kwani huko nyuma haikuwapo.
Alisema anachofahamu CCM ina taratibu zake za kupata wagombea kwa
kuwachuja, hivyo kauli hizo zinaonyesha kuingilia mamlaka hizo na
wanaozisimamia.
Alisema ameshangazwa na kinachojitokeza katika uchaguzi wa mwaka huu
wagombea wa CCM badala ya kutangaza nia na kuomba wadhamini wao
wanafanya kampeni kabisa utafikiri wameshapitishwa.
“Hii ni hatari kwa siasa, watu kufanya mambo kwa kutokuzingatia taratibu
siyo jambo jema, nahisi kuna kitu hakipo sawa huko, wanapaswa
wajichunguze na kuacha wahusika wafanye kazi yao badala ya wao kuwa
majaji,” alisema Dk Tily.
Mhadhiri wa UDSM, Dk Benson Bana alisema anayachukulia hayo kama
majigambo ya wanachama kutafuta nguvu na kujiamini na kwamba haoni kama
kuna shida, kwa sababu mwisho wa siku watajulikana nani anabaki na nani
anaondoka katika kinyang’anyiro hicho.
“Ninachoomba kifanyike hapa ni kamati kufanya kazi yake bila
kupindapinda wala kumuogopa mtu, kwani inaonekana wazi kuna ambao
wanajinadi wakiwa na lengo la kutafuta nafasi huko mbele ya safari ili
wasiachwe na atakayeshinda, kutengeneza historia katika maisha yao, pia
wapo wenye nia ya kweli,” alisema Dk Bana.
No comments:
Post a Comment