21 July, 2015

ARUSHA: MADEREVA 6 WALEVI WAFUNGIWA LESENI ZA KUENDESHA MABASI, WAPELEKWA MAHAKAMANI!

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), imefungia kwa miezi sita leseni za udereva za madereva sita wa mabasi wa mkoani Arusha na kuwafikisha mahakamani kwa tuhuma ya ulevi.
Aidha, imewaonya wamiliki wa vyombo mbalimbali vya moto nchini, wasiwaajiri wakati huu wanapotumikia adhabu yao, kuepuka magari yao yasinyang’anywe leseni ya biashara ya usafirishaji abiria kwa kosa la kuajiri walevi.
Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Leo Ngowi, alisema,“Madereva hao walikamatwa wakati wa ukaguzi maalumu, ulioendeshwa na mamlaka yetu Arusha, kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani”.
Aliwataja madereva hao, magari waliyokuwa wakiyaendesha na namba za leseni zao kwenye mabano kuwa ni; Sarikiaeli Mosses Niko  namba za usajili T137BCX lililokuwa likisafiri kati ya Arusha na Ngarenanyuki na dereva mwingine wa gari lenye namba za usajili T586 BWP, Shaaban Daudi Mdoe, lililokuwa linafanya safari kati ya Stendi Kuu na Usa River.
Wengine ni dereva wa gari lenye namba za usajili T107 DCT, ambalo njia zake hazikuelezwa, Prosper Joseph  na wa gari lenye namba T613BSD, Jeremiah Joseph Francis, ambaye gari alilokuwa akiliendesha lina leseni ya kufanya safari kati ya Arusha na Namanga.
Madereva wengine waliofungiwa ni pamoja na Elibariki Wariaeli Kimaro, aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T137 BCX, linalofanya safari kati ya Arusha na Ngarenanyuki na Yohanes Posolo Sanga aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T530AZE, ambalo njia zake hazikuelezwa.
Alisema, kutokana na kukithiri kwa ajali za barabarani, mamlaka hiyo, pamoja na kikosi cha usalama barabarani vilikubaliana kuendesha ukaguzi maalumu wa kushitukiza katika maeneo mbalimbali, wakianzia na Arusha ambapo Mei 2, mwaka huu, madereva watano walikutwa wakiendesha magari ya abiria wakiwa wamelewa pombe.
Kutokana na maelezo yake, wameamua kuchukua hatua ya kinidhamu na kisheria, kuwafungia leseni zao, kuzuia wasiajiriwe mahali kokote na mmiliki yoyote ndani ya Tanzania, iwe fundisho kwa madereva wengine wenye tabia hiyo.
“Madereva hao hawatapaswa kuajiriwa na mmiliki wa chombo chochote cha moto kwa sababu leseni zao tumezifungia kwa miezi sita, kuanzia Mei 2 hadi Novemba 2, mwaka huu. Atakayekamatwa kwa kuwaajiri atakuwa amepoteza sifa ya kufanya biashara ya kusafirisha abiria”, Ngowi alisema.

No comments:

Post a Comment

UKIONDOA DIPLOMA, DEGREE AU PHD ULIYONAYO, KICHWA CHAKO KINABAKI NA NINI?

Horace Mann - Binadamu wa kwanza kugundua wazo la elimu Albert Einstein aliwahi kuulizwa akili ni nini? What is intellect? Akasema akili ni ...