KWENU mastaa wa kike ndani ya Bongo Movies. Nianze kwa kuwasalimia wote kwa ujumla, asalaam aleikum waungwana na poleni kwa swaumu.
Binafsi niko poa, niko nanyi kiroho kuhakikisha swaumu inapanda hadi pale tutakapomaliza mfungo, ishallah Mungu awafanyie wepesi, muumalize mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani salama.
Bila kuwataja majina, (najua mnajijua) nimewakumbuka leo kwa barua. Nina jambo ndugu zangu nataka kuzungumza katika kipindi hiki cha mfungo. Natambua wapo baadhi yenu wanafunga kweli lakini wapo wengine hawafungi. Wanafanya maigizo kama ilivyo sanaa yao. Hao ndiyo nimewaandikia barua hii.
Najua wapo ambao wanajifanya swaumu imewabana kweli kumbe moyoni hawana lolote. Wanawadanganya Watanzania kwa kuweka picha za ushungi mitandaoni ili waonekane wamefunga kumbe wana majanga kibao wanayafanya nyuma ya pazia. Hata nafsi zao zinawasuta.
Ndugu zangu Mungu hadanganywi. Anajua matendo yetu yote ya kila siku. Hakuna haja ya kujificha. Eti unakula mchana, unafanya matukio yako ya ajabu na watu wanayaona lakini ndiyo unakuwa wa kwanza kuweka picha mitandaoni umevaa ushungi kuashiria umebanwa na swaumu.
Unawadanganya wanadamu wakati Mungu wako anakuona mpaka rohoni, kuna faida gani? Mnatakiwa kubadilika, hakuna haja ya kujitangaza uko safi wakati unafanya madhambi ‘chungu mbovu’ gizani, tena ndani ya mwezi huu mtukufu.
Mfungo huu uwe wa mfano. Wale ambao mmekuwa mkifuturisha kwa mbwembwe pia safari hii inabidi mbadilishe staili. Jaribuni kuwakumbuka watu wenye mahitaji na si kuitana mastaa na kuonesha ufahari wa kuwa na ‘madikodiko’ ya kumwaga.
Ili thawabu zako ziwe maradufu kwa Mungu, ni vyema katika kipindi hiki ukawakumbuka watu ambao wana shida kuliko wale ambao za kubadilishia mboga wanazo.Unawasaidia ambao wanakuja na magari kufuturu, wamesafiri umbali mrefu, wameweka mafuta kwa fedha zao, ina maana gani?
Unawaacha wale ambao hawajui hata kula yao ya siku moja, ‘haiswihi’ hata kidogo. Kuna watu ambao si kwa ridhaa yao wamejikuta wanaombaomba barabarani, kwa nini usiwasaidie?
Kuna watu wanaumwa, hawana msaada wowote mahospitalini, kwa nini usiende hata kuwajulia hali katika kipindi hiki na wao wakafarijika?
Mungu aliyekupa wewe utajiri, ndiye aliyewanyima wengine na ipo siku kibao kitageuka. Akakunyang’anya na ukarudi kule waliko wenye hali ya chini.
Niwasihi ndugu zangu tuoneshe kwa vitendo. Kufunga si kuacha kula pekee bali kunaambatana na matendo mema sanjari na kusaidia wenye matatizo. Vinginevyo funga yako inakosa mashiko. Una shinda na njaa.
Ni matumaini yangu mtakuwa mmenielewa, naomba mfanyie kazi mawazo yangu.
Ramadhani Kareem!
No comments:
Post a Comment