26 August, 2011

TANZANIA KUNA UGONJWA

Nimepata msukumo mkubwa kuandika hichi ninachokiandika baada ya kusikiliza mahubiri ya Mchungaji Josephat Mwingira kupitia kituo chake cha luninnga TRENET.

Watanzania na Afrika kwa ujumla tunaumizwa na yale tuliyozoea kuyasikia... Mara nyingi tumesikia wenzetu wa Marekeni, Ufaransa, Uarabuni, Ujerumani  wakisema "HATUWEZI". Neno hili limetufanya hata pale tunapotaka kujaribu jambo tunarudishwa nyuma kwasababu tu neno hatuwezi limeshaingia akilini mwetu.

Imani ni kuwa na uhakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana (Waebrania 11:1) Hii ina maana kwamba kwakua tuliambiwa hatuwezi imani yetu nayo imepokea kile tulichozoea kukisikia kwamba hatuwezi! 

Si hilo tu bali ni mara nyingi pia tumezoea kusikia Tanzania ni miongoni mwa nchi maskini Duniani!! Kwasababu hiyo kile tulichosikia tunakiamini hata kama ukweli juu ya utajiri na rasilimali zote tulizonazo hatuzioni.
                                           Masikio kiungo tunachotumia kusikia

Ni kichekesho kwa mtu aliyeamua kuoa na kuwa na familia kwenda kuomba unga ili apeleke nyumbani kwake ale na familia yake. Ndio maana mtu anapoamua kuingia kwenye jukumu la kuanzisha familia hujitahidi kufanya kazi kwa bidii ili familia yake isikose riziki. Hivyo basi badala ya kwenda kuomba unga atachukua jembe na kwenda kulima.   

Huu ni mfano halisi wa Tanzania yetu kuwa na uthubutu wa kuomba misaada nchi za nje licha ya kuwepo kwa ardhi yenye rutuba ya kuweza kufanya kilimo cha kuzalisha mazao ya kutosha kulisha Dunia nzima. Madini ya kufanya barabara zote za mijini na vijijini nchini Tanzania kujengwa, Wanyama mbugani na vivutio vingine vingi vya kuwezesha Tanzania kujiendesha bila kuomba msaada wowote. Lakini wapi!? Hii yote ni kwasababu tumesikia na kuamini kwamba Tanzania hatuwezi, Tanzania ni maskini na mambo mengine kama hayo.

Hatuhitaji  shule wala vyuo vikuu zaidi, wala hatuhitaji  wasomi zaidi bali tunahitaji watu wanaojitambua! Shuleni tulifundishwa kwamba babu zetu ni nyani! Hivyo sisi Waafrika tumetokana na nyani yaani sokwe watu. Tukafanya mitihani na tukafaulu kwa kujibu kwamba  kweli tumetokana na nyani! Kwasababu tuliamini kile tulichofundishwa! Ndio maana leo hii mhitimu yeyote wa Tanzania  pale tu anapomaliza masomo / mafunzo yake kikubwa anachokiwaza na kukitamani  ni kutafuta kazi aajiriwe ili alipwe mshahara utakaomsaidia kujikimu kimaisha. Kwasababu  hata waliomtangulia walifanya vivyo hivyo. Kwamba walipohitimu walitafuta kazi! Si kweli ndugu zangu? Au naongopa jamani?!

                                                                    Ramani ya Tanzania  

Mungu isamehe Tanzania. Kusikia kunatutesa; Neno hatuwezi linatutesa. Na maisha haya ndio tunayoyaishi siku zote. Mali zetu zinachukuliwa huku tunaona na tunanyamaza. Ni LAZIMA tukubali kusikia habari mpya kwani mafanikio hayawezi kuja mpaka pale tutakapo pona ugonjwa wa kuamini kwamba Tanzania hatuwezi, na tutakapo pona ugonjwa wa kuamini kwamba Tanzania ni nchi maskini.


No comments:

Post a Comment

UKIONDOA DIPLOMA, DEGREE AU PHD ULIYONAYO, KICHWA CHAKO KINABAKI NA NINI?

Horace Mann - Binadamu wa kwanza kugundua wazo la elimu Albert Einstein aliwahi kuulizwa akili ni nini? What is intellect? Akasema akili ni ...