Askari wa Kenya wakiwa wamejipanga kwa ajili ya kuwadhibiti watuhumiwa
waliovamia na kuteka watu kwenye Jengo la Westgate Mall mjini Nairobi
jana.
Mwanamke mmoja raia wa Uingereza ametajwa na gazeti moja la nchi
yake kuwa ndiye aliyeongoza shambulizi la kigaidi lililofanywa katika
eneo la maduka la Westgate jijini Nairobi, Jumamosi iliyopita.
Gazeti la Daily Mail la Uingereza lilikariri
vyanzo vyake ndani ya duru za usalama za Kenya ambavyo vilieleza kuwa
magaidi hao wanaoaminika kuwa ni wafuasi wa Kundi la kigaidi la
Al-Shabaab la Somalia waliongozwa na mwanamke anayeitwa Samantha
Lewthwaite maarufu kwa jina la White Widow (Mjane Mweupe).
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya,
Joseph Ole Lenku amesema wanaamini kuwa magaidi waliovamia jengo hilo la
Westgate wote ni wanaume.
Ole Lenku alisema baadhi ya watekaji hao walivalia
nguo za kike ili kuwachanganya watu na kwamba tayari wawili kati yao
wameshauawa na vikosi vya usalama.
Wakati Ole Lenku akisema hayo, Mkuu wa Majeshi ya
Kenya, Jenerali Julius Karangi alisema kuwa wanajua magaidi hao wanatoka
wapi lakini hakutaka kueleza zaidi.
Lewthwaite anayeaminika kuwa na umri wa miaka 29,
alifiwa na mumewe, Jermaine Lindsay baada ya kulipua bomu la kujitoa
muhanga Julai 7, 2005 jijini London, Uingereza.
Kundi la Al-Shabaab ambalo limekiri kuhusika na
shambulizi hilo, kupitia mtando wa Twitter lilitoa taarifa jana
likimsifia Lewthwaite, ambaye siku hizi anatumia jina la Sherafiyah.
“Sherafiyah Lewthwaite a.k.a Samantha ni mwanamke
shujaa na tunajivunia kuwa naye. Askari wetu wa Mujahideen wamejitolea
kufa katika operesheni hii.”
Milio ya silaha nzito na mabomu ilisikika kwenye eneo hilo la Westgate wakati wa mapambano kati ya polisi na magaidi hao.
Awali askari wa Kenya walieleza kuwa mwanamke
aliyevalia hijab ndiye aliyeongoza kati ya watu 10-15 wenye silaha
kuvamia jengo hilo.
Maofisa wa usalama wa Kenya ambao hawakupenda
kutajwa majina walikaririwa wakisema kuwa watu wengi waliokuwa
wameshikiliwa na magaidi hao walikuwa wameachiliwa na bado jitihada
zilikuwa zinafanyika kuwaokoa mateka waliobakia.
Kwa mujibu wa Daily Mail, mbali ya Lewthwaite,
raia wengine wa Uingereza wanaohusishwa na tukio hilo ni Liban Adam (23)
na Ahmed Nasir Shirdoon (24), ambao pia wametajwa kwenye taarifa ya
Al-Shabaab.
Chanzo: Mwananchi.com
Chanzo: Mwananchi.com


No comments:
Post a Comment