Dodoma. Bunge
Maalumu la Katiba linaanza vikao vyake tena leo mjini Dodoma, huku
kukiwa na jitihada kubwa za kujaribu kuweka udhibiti wa mjadala
utakavyoendeshwa miongoni mwa wabunge, wengi wao wakiwa ni kutoka chama
tawala CCM.
Kuna hofu
ndani ya chama hicho kwamba mgawanyiko uliojitokeza wakati wa vikao vya
kamati utahamia kwenye Bunge zima ambako mbali na waandishi wa habari
kuruhusiwa kushiriki, pia huonyeshwa moja kwa moja na vituo kadhaa vya
televisheni.
Msigano
unaotabiriwa kutokea ni ule uliojengwa katika mambo yaliyozua mvutano
ndani ya kamati kiasi cha wajumbe wenye itikadi moja kusigana kwa
misingi tofauti lakini kubwa likiwa ni lile la Uzanzibari na Ubara.
Tofauti hizo
za kimaeneo zilionekana dhahiri wakati wa mjadala wa Sura ya Tisa na 10
ambazo zinahusu muundo wa Bunge na mambo mengine ya utawala, pia katika
Sura ya 14 hususan mgawanyo wa mapato.
Mwishoni mwa
wiki iliyopita, baadhi ya wenyeviti wa Kamati za Bunge hilo walitabiri
mvutano mkali bungeni, wakirejea hali ilivyokuwa ndani ya kamati zao
ambako baadhi ya wajumbe hawakuridhika na baadhi ya uamuzi.
Mwenyekiti
wa Kamati Namba Nne, Christopher Ole Sendeka alisema mjadala katika
kamati yake ulikuwa mkali na kwamba hali itakuwa ni ngumu zaidi
watakapoingia bungeni.
Mwenyekiti
wa Kamati Namba Tatu, Dk Francis Michael alisema suala la ardhi linaweza
kuzua mvutano mkali kwani ni moja ya mambo muhimu katika Katiba.
Makamu
Mwenyekiti wa kamati Namba Kumi na Moja, Hamadi Yusufu Masauni alisema
jambo pekee analotarajia kuwa litasumbua ni muundo wa Bunge la Muungano.
Alisema unapotajwa muundo wa Bunge ndipo unapotajwa mfumo wa Muungano ambao umekuwa ni kero ya muda mrefu.
Mwenyekiti
wa Kamati Namba Moja, Ummy Mwalimu alisema hofu yake iko kwenye suala la
mgawanyo wa mapato ambalo kamati yake ilisita kulijadili hadi
walipoitwa wataalamu kutoka Benki Kuu ya Tanzania na Wizara ya Fedha za
Muungano na ile ya Zanzibar.
Kwa msingi
huo, wakati kamati zikianza safari ya siku tano kuwasilisha taarifa zake
kuanzia leo hadi Septemba 8, mwaka huu, kutakuwa na maoni ya wachache
katika baadhi ya kamati suala ambalo linatoa picha ya kuwapo kwa mawazo
tofauti katika mambo kadhaa.
Uchunguzi wa
gazeti hili umebaini kuwa mengi ya mambo hayo ni yale yaliyobadilishwa
kinyume na yalivyokuwa kwenye Rasimu ya Katiba iliyotungwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba au mambo mapya yaliyoingizwa kwenye rasimu hiyo.
Mambo yaliyobadilika
Kamati za Bunge Maalumu katika uchambuzi wake wa rasimu zimefanya mabadiliko makubwa tofauti na ilivyokuwa awali.
Mabadiliko
yaliyofanywa yameondoa mambo makubwa yaliyokuwa yakiifanya rasimu hiyo
kuonekana mpya, kiasi cha baadhi ya wachambuzi kuiona kama ‘Katiba ya
1977 iliyofanyiwa marekebisho’.
Mwelekeo wa
kubadili karibu misingi yote muhimu iliyojengwa na Tume ya Jaji Joseph
Warioba, ilianza baada ya kuwekwa kando kwa mfumo wa muungano wa
Serikali tatu uliopendekezwa na badala yake kurejea katika muundo wa
sasa wa serikali mbili.
Uamuzi huo
uliathiri mtiririko na muundo mzima wa sura na ibara za rasimu hiyo,
kwani sasa wajumbe wa Bunge Maalumu walilazimika kutengeneza Katiba
yenye mwelekeo wa Serikali mbili na siyo tatu tena zilizokuwa
zimependekezwa na tume.
CREDIT: MWANANCHI: PINDUAPINDUA YA RASIMU YA KATIBA
No comments:
Post a Comment