1.
Utangulizi
i. Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe
20 - 22 Novemba 2013, Kamati
Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia kunivua nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. Kwa
mujibu wa taarifa ya chama iliyotolewa
katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi
mimi na Dk Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na
waraka unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013. Ukweli ni kwamba waraka
uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa
nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati
Kuu . Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu
ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama.
Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi
nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa. Nitazianisha tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo
nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vyama.
ii.
Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika
wakati mgumu sana sasa hivi.
Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo
cha CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha hivi nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu
atakapokuwa mtu mzima na atakapoamua
kujiunga na siasa aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na chama changu
na ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi
jana, leo
na kesho.
Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu
Zipo
tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu. Tuhuma
hizi zinalenga kuonyesha kwamba
mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili kukihujumu chama changu. Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu
kama ambavyo nimekuwa
nikizijibu
katika vikao mbalimbali vya chama.i) Tuhuma
kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais katika uchaguzi
wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:● Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika
Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.● Pamoja na kuwa
mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam,
Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa
juu aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea
urais.● Kote
nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.● Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais
katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane
ya Mkoa wa Kigoma.ii) Tuhuma kwamba katika
Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia kampeni wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye
niliyeshinda katika uchaguzi huo. Ukweli
ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo ndivyo wapiga kura
wa Kigoma walivyoamua.iii) Tuhuma kwamba nilishiriki
kuwashawishi wagombea wetu katika baadhi ya majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa
CCM wapite bila kupingwa kwa
njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni pamoja na Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini. Kama
nilivyokwisha kueleza katika vikao
mbalimbali vya chama jambo hili si la kweli na hakuna popote ambapo watoa tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi kwamba nilifanya
jambo hili. Nipo tayari kwa uchunguzi
ndani ya chama na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi
kila mara tangu mwaka 2010 bila uchunguzi wowote kufanyika na jambo
hili lifikie mwisho.iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni
mbalimbali za chama: Ukweli ni kwamba
nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni
kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda
katika mikoa yote tuliyotembelea. Mwaka 2012
baada ya hoja ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa
Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa
na operesheni kubwa moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi. Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa
nchini Marekani kufungua matawi kwa mwaliko wa Watanzania wanaoishi
huko.v)
Tuhuma
kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG):
Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu nilipaswa
kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya'
ili wajiandae. Kwamba kutokuwatonya
kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM na nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika
taarifa yangu nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo ningependa kuyakariri
hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:● Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti
wa PAC kulinda chama changu na kuonea vyama
vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na
ambazo tunapigania kuzibadilisha● Napenda kusisitiza
kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
Natambua kwamba mahesabu ya chama
changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea.
Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya
siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa
hili ni la nani.
vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu
kuchukua Posho za Vikao
Mtakumbuka
kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa
kupinga posho za kukaa na matumizi
mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu ya mwaka 2010-2015. Mtakumbuka kwamba hivi
karibuni Mheshimiwa Lema amenishutumu
kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya
umma ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza
yafuatayo kuhusu jambo hili:● Sipokei posho yeyote
ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu
mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za
Bunge ninavyohudhuria. Mtu yeyote
mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.● Swala la kukataa
posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na kwangu ni swala la
kimisingi
zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye
ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa huduma kwa sababu ya
bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi ya Serikali katika
Ilani, na kuondoa posho za
wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa, kungesaidia sana
kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.
● Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa
Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.3
.
Usambazaji
wa Ripoti
ya Siri kuhusu Zitto Kabwe
Hivi
karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi ukibeba lundo
la tuhuma kwamba nimehongwa fedha
nyingi ili kukihujumu chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu ya
CHADEMA. Jambo hili pia lilijadiliwa
katika kikao cha juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka huu haukuandaliwa wala kusambazwa na
makao makuu. Katika mchango wangu nililalamikia mambo matatu
yafuatayo:i. Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza
waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini
kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa
taratibu za chama chetu.ii. Kwa kuwa chama
kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za kisheria ili kuhakikisha kwamba wote
waliohusika kutengeneza hekaya ile wanachukuliwa hatua stahiki za
kisheria.
4.
Hitimisho
a) Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu
mapigo na ningewazodoa
watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za Tanzania. Natambua
pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya siasa
hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi magumu'.
Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya
kuendelea kutumia
suala hili katika harakati zao za kudhoofisha mapambano ya demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani
nchini mwetu.
Napenda wanachama
wa CHADEMA nawapenda
demokrasia na siasa safi wote nchini
watambue kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu
wa chama hiki na nitakuwa wa
mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote
ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.b)
Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia ninapopigwa. Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na
zinanikwaza. Tuache siasa za uzushi
ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania wenye
matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.
c) Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda
sasa yapo mengi mazuri
nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa na yapo makosa niliyofanya
kisiasa katika maisha yangu ya siasa.
d) Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya
kukuza demokrasia. Ni mapambano
baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa
safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka.
Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu inayohitaji uongozi shupavu kuikabili. Nitasimama daima upande wa
demokrasia. Kama alivyopata kunena mmoja ya wanasiasa maarufu,
'kiwango cha juu kabisa cha uzalendo katika nchi ni kukubali kutofautiana
kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni wa chama chetu.
Kabwe
Zuberi Zitto, Mb
Dar
es Salaam.24 Novemba, 2013
No comments:
Post a Comment