24 January, 2014

CHADEMA YAWASILISHA PINGAMIZI DHIDI YA ZITTO

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewasilisha majibu na pingamizi la awali dhidi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuhusu Kamati Kuu ya Chama hicho akiitaka mahakama kuzuia uanachama wake usijadiliwe hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.
Kadhalika, chama hicho kimejibu barua ya Zitto pamoja na kuwasilisha mwenendo wa shauri lililopelekea kuvuliwa nyadhifa za uongozi katika chama hicho kama mlalamikaji alivyoomba.
Majibu hayo yaliwasilishwa jana Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Mawakili wa chama hicho, Tundu Lissu na Peter Kibatala, katika pingamizi hilo kuna hoja sita na wakiitaka Mahakama kutupilia mbali kesi hiyo kwamba haina mashiko ya kisheria.

Hoja hizo ni shauri hilo halina msingi kwa sababu halikuwasilishwa katika Mahakama ya chini kusikilizwa na kutolewa maamuzi kwa mujibu wa kifungu cha 13 cha Mwenendo wa Mashauri ya Madai.
Limewasilishwa masijala Kuu ya Mahakama Kuu badala ya masijala ya Wilaya kinyume cha sheria na taratibu za masijala za Mahakama.
Mlalamikaji hajaomba maoni ya Mahakama Kuu kuhusiana na suala linalohusiana na uanchama wake Chadema.
Nyingine ni shauri halina msingi kwa sababu Zitto anaendesha mashauri mawili, Mahakama Kuu na rufaa ya kwenye Baraza Kuu la chama.
Pia Mahakama Kuu siyo mahali pake kwa sababu Zitto hajatumia nafasi zilizopo ndani ya Chadema.
Mahakama Kuu haina mamlaka ya kutoa maamuzi ya maombi ya kuzuia Zitto asijadiliwe uanachama wake kwa sababu ni mambo ya yanayohusu Chadema.
Chadema wakijibu maombi ya msingi ya Zitto kupitia hati iliyosainiwa na Sylvester Masinde na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa, wamedai kwamba hawana ubishi kwamba mlalamikaji alivuliwa uongozi Novemba 22, mwaka 2013.
Pia, inaeleza kwamba Zitto alishiriki katika Mkutano wa Kamati Kuu na alijua kinachoendelea kuhusu tuhuma zake.
Chadema inaomba Mahakama kutupilia mbali maombi ya mlalamikaji kwa kuwa hayana mashiko ya kisheria.
Mapema Januari 2, mwaka huu Zitto kupitia Wakili Albert Msando, alifungua kesi mahakamani hapo dhidi ya Baraza la Wadhamini la Chama hicho na Katibu Mkuu, Dk. Slaa, akiiomba Mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu kutojadili suala la uanachama wake hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.
Mahakama iliyokaa chini ya Jaji John Utamwa ilikubali na kutoa zuio la muda hadi kesi ya msingi itakapoisha.

No comments:

Post a Comment

UKIONDOA DIPLOMA, DEGREE AU PHD ULIYONAYO, KICHWA CHAKO KINABAKI NA NINI?

Horace Mann - Binadamu wa kwanza kugundua wazo la elimu Albert Einstein aliwahi kuulizwa akili ni nini? What is intellect? Akasema akili ni ...