
Wakati nilipofanya jambo na akaniambia
limemkwaa, nilihakikisha kuwa naongea naye kuhusu suala husika na
kuhakikisha kuwa tunalipatia ufumbuzi. Sikuwa natumia ubabe kwa
kumlazimisha labda kuwa bwana eee…ndio imekuwa hivyo basi sasa unasemaje
au kauli zingine kama hizo. Lahasha!! nilitumia lugha ambayo mwishowe
iliturejesha katika furaha yetu ya awali.
Tatizo ni kwamba alipofanya yeye jambo
lililonikwaza, ninapomuuliza tu, huo ndio ungekuwa mwisho wa furaha yetu
kwa siku kadhaa. Hakupenda tujadili kitu pale aliponikosea. Na daima
alipenda kuangalia zaidi lugha niliyotumia kuuliza badala ya mantiki ya
nilichokuwa nauliza.
Ningeweza kumuuliza “Unadhani mie siumii unapofanya hivyo?”
na badala ya kunipa ufafanuzi, akaelewa kuwa hizo ndio hisia zangu na
kunipa maelezo ya kunitoa katika hisia hizo mbaya, yeye angekimbilia
kusema “Kwahiyo unataka kuniambia kuwa huko nilikokuwa nilikuwa na wanaume sio?” Na hali hii haikuwa mara moja wala mara mbili.
Nilijitahidi sana kuizoea lakini
ilinishinda. Ilinishinda maana ilikuwa inaniuliza. Mara nyingi
nilijiuliza maswali mengi sana kuliko majibu.
- Je, hanipendi ndio maana anafanya hivyo makusudi na nikiuliza anakwepa kunijibu ili aniumize?
- Je, anathamini sana kazi, shughuli na hata marafiki zake kuliko mimi? Yaani mimi sio kipaumbele chake cha kwanza?
- Ni kwanini hasa ninapoeleza hisia zangu anakuwa mkali badala ya kunijibu kama ninavyomfanyia mimi?
Kwa ujumla mlolongo wa maswali ulikuwa
mengi zaidi ya majibu. Sikujua hali hii inatokana na nini. Nilikuwa
nafanya kila niwezalo kuhakikisha kuwa simuumizi. Nikimkosea nampa
maelezo anielewe ili awe na amani. Nami sikutaka akinifanyia jambo
nikwazike milele. Nilipenda sana awe ananipa maelezo ya kutosha badala
ya kunifanya niishi kwa vinyongo na kumdhania kuwa hanipendi. lakini
haikuwa rahisi namna hii. Ilishindikana.
Nahofia kukaa na kitu kinachonikwaza
moyoni maana najua wazi kitanifanya nianze kujenga chuki na yeye.
Nitakuwa namshuku vibaya hata kama hanitendei ubaya. Lakini nitafanyaje
ilhali hataki pia kunipa nafasi ya kumuuliza? Kila nikimuuliza ananijia
juu na tunaishia kugombana? Je, nianze kujadili matatizo ya mpenzi wangu
na majirani au watu wengine badala ya yeye? Na je, hao nitakaokuwa
nikijadili nao matatizo ya mwenzangu watatupeleka wapi hasa? Si nao
watafungua vinywa kuongea na wengine zaidi na mwishowe tutaishia
kuanikwa mtaa mzima?
Credit: R. Msangi Via Jukwaa Huru Media Inc.
No comments:
Post a Comment