
Hakuna kati yetu ambaye hata sasa
anaweza kukataa kuwa hatukupendana. Ndio. Yeye alilijua hilo na hata
mimi nililijua hilo. Lakini mwisho wa siku unajua tumeishia wapi?
Tumeishia kwa kila mmoja kuchukua njia yake. Yes…tulipendana sana lakini
tukaishia kwa kila mmoja kuamua kuangalia upande tofauti na alipo
mwenzake. Unataka kujua ni kwanini hasa ilitokea hivi? hebu subiri…….
Wakati Mungu alipoamua kumuumba
mwanadamu, kwa makusudi kabisa aliona kuna umuhimu wa kumpa kila mtu
kipaji, uwezo, akili na vitu vingine vya namna hiyo kwa namna ya upekee
kabisa ambayo ni tofauti kabisa na wengine. Ndio maana duniani kuna
msemo wa kuwa “wewe ni mtu maalum, hakuna mwingine kama wewe dunia nzima, hata kama mnafanana majina na maumbo“. Ni kutokana na ukweli huo basi, ambapo binadamu tumekuwa tukitofautiana kimitizamo, kiakili, kimaumbile, nk.
Bahati mbaya sana binadamu tunapofikia
umri wa kuingia kwenye mahusiano, ukweli huu tumekuwa tukijitahidi sana
kuukwepa. Tumekuwa tunaukwepa ama kwa makusudi kabisa, au kwa bahati
mbaya pengine kwa kutokujua. Wengi wetu tumekuwa tukiamini kuwa tunaweza
kabisa kuwapata watu wenye kila tunachokihitaji katika maisha yetu.
Lakini hebu ona, ni wangapi ambao wameshawahi kuwapata watu wenye kila
walichokuwa wakikihitaji?
Ukweli ni kuwa, hata pale ambapo
tunawaona watu wakisherehekea Jubilee za miaka kibao ya ndoa zao,
haimaanishi kuwa kudumu kwao huko kumetokana na mwanaume au mwanamke
husika kuwa alipata kile alichokuwa akikihitaji na ndio maana akadumu
nacho.
Ukweli ni kwamba, hata hawa wamepitia
milima na mabonde mengi mno. Tena mengi kuliko wale wanaoshindwa
mwanzomwanzo wa safari yenyewe ya mahusiano. Na kuthibitisha hili ndio
maana kuna msemo wa “Wagombanao ndio wapatanao“….Taarifa za
kitaalamu kabisa zinaonyesha kuwa ndoa/mahusiano yale ambayo yamekuwa na
migongano ya fikra ya mara kwa mara ndio ambazo zimeweza kudumu kwa
muda mrefu.
Muujiza!! Hapana, si muujiza bali ndio
uhalisia wenyewe huo. Lakini unajua ni kwanini basi ikawa hivi? Ni
kwanini wale wenye kukwaruzana mara kwa mara ndio wenye kudumu zaidi?
Lakini kwanini pia wapo wenye kukwaruzana kidogo tu na kila kitu kikawa
kimesambaratika? Jibu ni rahisi sana tu…….
Meeting Point.
Wakati fulani nilipokuwa mdogo,
nakumbuka tulipokuwa tukicheza mchezo wa kupigana na kila mmoja akawa
anamuogopa mwenzake, basi tulikuwa tunachora mstari chini kisha tunasema
anayejiamini anatakiwa kuvuka upande wa mwenzake, na hapo ndipo ngumi
zingeanza. Wengi wetu tulicheza mchezo huu, hasa wale tuliokulia
vijijini. Je, mchezo ule unatufundisha nini tunapokuwa ni wakubwa hivi
sasa? Unatufundisha nini kwenye suala la mahusiano?
Mahusiano kama kitu chochote ambacho
huwakutanisha watu wawili, ambao kila mmoja ameumbwa tofauti sana na
mwenzake, ni kitu kigumu sana. Ni kitu kigumu sana maana ni kitu chenye
kumfanya mtu abadilike kwa kila hali.
Mahusiano yaliyo bora kabisa ni yale
ambayo hayaendi kwa mtindo wa hisia zangu, au hisia zake, bali hisia
zetu. Lakini tunazipataje hisia zetu ilhali kila mmoja ana zake. Je,
hisia ni kemikali ambayo unaweza kwenda maabara ukachanganya yako na ya
mwenzako mkapata kompaundi moja ambayo inakuwa hisia zenu? Bilashaka
jibu ni HAPANA, na kama jibu ni hapana, ni nini basi kinatokea ili kuwa
na hisia zenu na sio zako au zake? Subiri nikupe mkasa mmoja:
Siku moja isiyo na jina, nililazimika
kukesha kwa kukosa usingizi baada ya kukwaruzana na mtu niliyekuwa
nampenda. Ilikuwa baada ya kupishana kauli siku kadhaa kabla ya hapo,
ambapo kwenye maongezi yetu niliongea jambo ambalo mwishowe alilitafsiri
vibaya. Haikusaidia mimi kujieleza, na baada ya siku kadhaa ndio
ikafikia siku hii ambayo aliniambia ni bora asiwasiliane nami kwani
nimekuwa nikimuumiza kwa kauli zangu.
Katika usiku huo, nilijiuliza mambo
mengi sana, kubwa likiwa ni wapi hasa nilikosea? Cha ajabu sana ni kuwa
ndani kabisa ya nafsi yangu, kuna kitu kilikuwa kikiniambia look,
hakuna lolote baya ulilolifanya. Ulikuwa na haki kabisa ya kufanya
hivyo…tatizo haliko hapo”. sauti hii ilinichanganya sana, lakini mwisho
wa siku ilinifanya nizidi kuumiza kichwa zaidi na kwakuwa usiku ulikuwa
mrefu sana haikuwa shida baadae kujua tatizo lilikuwa nini.
Chini ya mfumo ule ule wa tofauti za
hisia za mwanadamu, nilibaini kuwa licha ya kwamba tulipendana, lakini
hatukuwahi kuwa na mahali ambapo hisia zetu zilikuwa zinakutana. Ndio…we
never identified the need for a place where our feelings could have
been meeting…….
Nilijibaini kuwa kihulka zile zile za
hisia za kiuanadamu, mimi nilkuwa ni mtu wa KUSOMA MATENDO YAKE, wakati
ambapo yeye alikuwa ameumbwa katika hisia za KUTAFSIRI KAULI ZANGU
ZAIDI. Unaona hapo….mmoja msomaji mwingine mfasiri….mmoja
maneno…mwingine matendo. Tungeweza kuelewana kweli? Hapana ilikuwa
vigumu sana. Ilikuwa ni lazima tupate mahali ambapo hisia zetu zingeweza
kukutana. Mahali ambapo fikra zetu zingeweza kukutana. Ilitakiwa tuwe
na Meeting Point.
Ndio…hapa ni mahali muhimu sana ambapo
tulishindwa kupaandaa…ni mahali ambako tulitakiwa toka mwanzo tuwe
tumeshapaandaa kwani hapa ni mahali ambako pangemaanisha kila kitu
kuhusu maisha yetu ya mahusiano.
Ni mahali ambapo ningeweza kumwambia
Hakuna kwenda disco, na akaelewa kuwa simaanishi akienda anafanya
umalaya, bali nina hamu ya kuwa naye ubavuni mwangu kwa muda huo. Hapa
ni mahali ambako ningemuuliza kwanini umekawia kurudi nyumbani na
akaelewa kuwa nilitamani sana nikute yuko nyumbani anipokee na sio kuwa
nilimaanisha kuwa amepitia mahali pabaya. Ndio…hapa ni mahali ambako
angeniambia nataka kwenda kwa rafiki yangu nami nikaelewa kuwa anaona
nimechoka anataka nipumzike kwa utulivi kwakuwa akiwepo hawezi kuvumilia
kunisemesha……Kifupi, hapa ni mahali ambako pangekuwa kila kitu.
Ni katika usiku huo huo nilipowaza na
kujua kuwa kumbe tulifanya makosa makubwa sana kutokukubaliana katika
hili. Tulikosea sana kuamini kuwa ningeweza kumpenda naye akaonyesha
kunipenda wakati hatupendani. Ni usiku huo nilipobaini kuwa kumbe
tulichokuwa tukifanya ni sawa na mimi kuuvuta moyo wake, huku yeye naye
akiuvuta wangu..kumbe tulitakiwa tusivute moyo wa kila mmoja bali
tuunganishe nyoyo zetu. Lakini tungefanyaje ilhali hatukuwa na meeting
point? Sikuwa napita katikati ya mistari ya kile alichokuwa akitenda.
Hakuwa akipita katikati ya mistari ya kile nilichokuwa
nikikisema………….Hatukuwa na mahali tulipokuwa tunakutanisha hisia
zetu…huyu akajua ni kwanini yule alifanya vile na kwanini huyu akasema
hivi……..
No comments:
Post a Comment