Mbeya. Aprili 6, mwaka huu ni siku ambayo mkazi wa Kijiji cha Kibanda wilayani Kyela, Mboka Mwakikagile (20) haitaisahau.
Ni siku ambayo aliibiwa mtoto mchanga wa kiume aliyekuwa na umri wa siku saba tu.
Akisimulia tukio hilo, Mboka anasema alijifungua
salama Machi 30 akiwa nyumbani kwa wazazi wake ambao ni Lupalo
Mwakikagile (90) na mkewe Nelly Kyusa (49).
Anasema akiwa katika siku ya saba, alipigiwa simu
na mzazi mwenzake (jina linahifadhiwa) kwamba mama yake mkubwa atafika
nyumbani kumwona mtoto.
Anasema baada muda mfupi mwanamke huyo alifika
kwa pikipiki akiwa na mkoba uliokuwa na nguo za mtoto, sabuni na vifaa
vingine. “Baada ya kumkaribisha na kusalimiana na wote , mwanamke
huyo alimchukua mtoto na baadaye alinishauri twende Zahanati ya Njisi
akatibiwe jicho ambalo lilikuwa linamsumbua kidogo,’’anasema.
Mboka na mwanamke huyo waliondoka kwenda kwenye
zahanati hiyo kwa pikipiki na kwamba baada ya kufika hapo, daktari
aliwataka wanunue daftari na mwanamke huyo alitoa Sh2,000 na kumtaka
akanunue.
‘’Nilipokea fedha hizo na kumwachia mtoto pamoja
na simu yangu wakati mimi nikielekea kununua daftari kwenye duka lililo
mbali na zahanati hiyo,’’ anasema.
Anasema mara baada ya kurudi dukani alishtuka kutomwona mwanamke na mtoto wake.
Anaongeza kuwa alimwomba daktari simu na
kumpigia mzazi mwenzake ambaye alimjibu kwamba asiwe na wasiwasi kwani
inawezekana alitoka mara moja.
‘’Nilikwenda eneo la bodaboda na kuwauliza
madereva kama walimwona mwanamke akiwa na mtoto. Walikiri kumwona akiwa
na wasiwasi na kwamba alipanda pikipiki na kuondoa,’’ anasema.
Anasema baada ya kuambiwa hivyo, aliangua kilio jambo lililowafanya majirani wa eneo hilo kutaharuki na kufika kumpa pole.
Mboka anasema alikwenda kutoa taarifa Kituo cha
Polisi Kasumulu , lakini cha ajabu alipofika alimkuta mzazi mwenzake
akiwa kituoni hapo.
No comments:
Post a Comment