Wanamgambo wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria, ambao chanzo chake kinatajwa kuwa ni ukosefu wa ajira na ujinga.
Rais mstaafu wa Nigeria, Jenerali Olusegun Obasanjo (aliyeinama) akimuonyesha kitu Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin William Mkapa, katika mkutano wa marais wastaafu uliofanyika jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.
SIRI ya kuanza kwa kundi la ugaidi la Boko Haram
linaloendesha vitendo vyake vya kigaidi nchini Nigeria, iliyofichuliwa
wiki iliyopita na aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Olusegun Obasanjo, sasa
inaweza kuiathiri Tanzania.
Obasanjo, akiwa katika kikao na viongozi wenzake wastaafu
jijini Dar es Salaam, alisema ukosefu wa elimu na ajira kwa vijana wa
nchi hiyo ndiyo chimbuko la Boko Haram.
Onyo hilo la Obasanjo kwa serikali za Afrika kujikita
katika kutatua tatizo la ukosefu wa ajira na elimu linaweza kuwa chachu
kwa viongozi wa Tanzania kutafuta ufumbuzi badala ya kushambulia
wanasiasa.
Obasanjo aliongeza kuwa kundi la Boko Haram ambalo
linatokea kusini mwa Nigeria, limekusanya wapiganaji wengi ambao hawana
ajira, huku wengi wao wakiwa hawajapata elimu na ajira.
Akitoa ushauri kwa nchi za Afrika kuondoa tatizo hilo ili
kuhakikisha uchumi wake unakua na kuondoa uwepo wa makundi kama hayo
yanayosababisha kushusha uchumi, ni lazima wahakikishe wanatoa elimu na
kutengeneza ajira kwa vijana wa mataifa yao.
Wito kama huo umewahi pia kutolewa na viongozi kadhaa
nchini, akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, waliotaka
kutafutwa kwa ufumbuzi wa tatizo la vijana wasiokuwa na ajira.
Lowassa, amekuwa akielezea namna ambavyo ukosefu wa ajira
unavyotengeneza bomu kwa vijana linalosubiri kulipuka muda wowote,
akitolea mfano wa kujitokeza kwa vijana 10,000 Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam wakiwania nafasi 70 pekee za kazi Idara ya Uhamiaji.
Katika mazungumzo yake, Lowassa aliwaeleza wanahabari
kwamba ili kuepusha ongezeko hilo linalokua kwa kasi, serikali ni lazima
ihakikishe inatengeneza ajira kwa kuwa kila mwaka zaidi ya vijana
30,000 wanahitimu katika vyuo mbalimbali nchini.
Lowassa aliyejiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008,
amekuwa akiishauri serikali kuchukua hatua kukabiliana na tatizo la
ajira, ambalo limemsababishia malumbano na Waziri wa Kazi na Ajira,
Gaudensia Kabaka aliyejibu mapigo Machi 21, 2012 bungeni kwa kutoa
takwimu zinazoonyesha namna serikali ilivyotengeneza ajira.
Kwa upande wake, Mbowe alilalamikia serikali kwa kutokuwa
makini kwa kushindwa kulitafutia ufumbuzi tatizo la ajira kwa vijana
ambalo aliomba liwe hoja maalum bungeni, serikali kuu, halmashauri na
katika baraza la mawaziri kwani ni janga la taifa.
Wakati Mbowe akichangia hotuba ya Waziri wa Fedha bungeni
kuhusu mapendekezo ya serikali ya makadirio ya mapato na matumizi kwa
mwaka 2014/15, alisema ajira ni mkakati na siyo suala la kufumania.
Akielezea njia za kuondoa tatizo hilo, aliishauri serikali
kubadili mfumo uliopo wa kurundika kila kitu serikali kuu katika
kutengeneza ajira kwani haiwezi kufanikiwa na badala yake alitaka kuwe
na mkakati wa kutengeneza ajira katika halmashauri zote 133.
Mbowe alisema kuwa haoni sababu ya kuwa na wakurugenzi na
wataalam wa uchumi katika halmashauri wasiokuwa na uwezo wa kutengeneza
ajira.
Aliishauri serikali kuanzisha Mamlaka ya Majengo (Real
Estate Authority – REA) itakayohusika kusimamia majengo mijini na
kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia kujenga ajira kwani bila ya
kufanya hivyo, vijana watalazimika kukimbilia mijini kwa sababu vijijini
hakuna maendeleo wala mwelekeo.
Alisema ni aibu kwa halmashauri za Kinondoni na Ilala
kutegemea ruzuku toka serikali kuu wakati zina vyanzo vingi vya mapato
ambavyo vinaweza kusaidia kutengeneza fedha na ajira kwa vijana.
Aliongeza kuwa idadi ya Watanzania kwa sasa wanafikia
milioni 50 na kila mwaka wahitimu wa vyuo vikuu wanafikia zaidi ya
40,000 huku kukiwa hakuna ajira.
Tanzania Daima Jumapili, imedokezwa kuwa kutovalia njuga
kupuuza ushauri huo kunaweza kuchangia kushamiri kwa makundi ya kihalifu
kama Boko Haram aliyoitaja Obasanjo.
Tayari hapa nchini kumezuka makundi ya kihalifu ambayo
baadhi yao ni Watoto wa Mbwa, Panya Road na Badface ambayo yalitikisa
maeneo mbalimbali kwa uhalifu uliozimwa na vyombo vya dola, lakini
unaweza kuzuka tena siku za usoni.
Vijana hawa wamekuwa wakienda kupora wakiwa kundi kubwa
lenye watu 30 hadi 100 wakiwa wamebeba silaha za jadi ambazo huzitumia
kuwashambulia wanaowapora.
Zipo taarifa nyingine zinasema kwamba vijana hao hutumia
njia ya kuimba kwa sauti kubwa wimbo huu; “Tunatakaa… pesa zetuu..!”
huku wakiingia ndani kuchukua vitu vya thamani na kuwaacha baadhi ya
majirani wakiduwaa kwa kudhani mtu anadaiwa kumbe anaibiwa.
Makundi ya vijana hawa yanaelezwa kuwa maskani yao yapo maeneo ya Manzese, Kigogo, Mburahati, Kigogo Luhanga na viunga vyake.
Vijana wanaofanya uhalifu kama huo, pia wamekuwa
wakipatikana katika Mkoa wa Mara wakitumia majina ya Jamaica Mob, Mbio
za Vijiti na Midomo ya Furu ambao mara kadhaa wamekuwa wakiwasumbua
wakazi wa mkoa huo kwa kuwaibia na baadaye kuwajeruhi kwa silaha za
jadi.
Mkoani Kilimanjaro pia liliibuka kundi la vijana lililokuwa likifanya uhalifu lijulikanalo kwa jina la Kunguru Hafugiki.
Tanzania Daima Jumapili, limekuwa likifuatilia baadhi ya
nyendo za viongozi wa serikali katika kutatua kero za ajira, ambao wengi
wao wamekuwa wakitoa zawadi za fedha na ahadi kwa vijana wakati wa
uchaguzi badala ya kujikita kwenye miradi itakayokuwa endelevu.
Ahadi hizo na fedha hizo ndizo zinadaiwa kuwajenga chuki
vijana pindi zinaposhindwa kutekelezwa na kujikuta wakishiriki kwenye
vitendo vya kihalifu.
No comments:
Post a Comment