Dodoma/Dar. Wakati wowote wiki hii, Rais Jakaya Kikwete anatarajia
kukutana na viongozi wa Vyama vya Siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD) ili kuzungumzia mchakato wa Katiba.
Katika mkutano huo, Rais Kikwete atakutaka ‘kiaina’ na wajumbe wa Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao unaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi,
Chadema na CUF.
Aprili 16, mwaka huu wajumbe wa Ukawa na baadhi kutoka Kundi la 201,
walisusia vikao vya Bunge hilo wakitaka msingi wa mapendekezo ya Rasimu
ya Katiba usibadilishwe, wakipinga uamuzi wa CCM kutaka kuingiza mfumo
wa serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa katika Rasimu.
TCD inaundwa na vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni ambavyo ni
CCM, CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi, UDP na TLP, huku vyama visivyo na
uwakilishi bungeni vikiwakilishwa na UPDP kinachoongozwa na Fahmi
Dovutwa.
Jana, kwa nyakati tofauti wenyeviti wenza wa Ukawa, Freeman Mbowe
(Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR
Mageuzi), walisema wako tayari kukutana na Rais, ila msimamo wao wa
kutaka ijadiliwe rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kimekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa Ukawa kuomba wakutane na Rais
Kikwete kwa ajili ya kujadiliana namna bora ya kuendesha mchakato wa
kupata Katiba Mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari bungeni Dodoma jana, Mwenyekiti wa
TCD, John Cheyo alisema Rais atafanya kikao hicho wakati wowote ndani ya
wiki hii na kwamba viongozi wa vyama wakiwamo wa Ukawa, wamethibitisha
kushiriki.
Cheyo alisema, katika kikao walichokutana Dar es Salaam Agosti 23,
wanachama wa TCD walikubaliana kwamba upo umuhimu wa kukutana na Rais
Kikwete kwa mazungumzo na maridhiano.
Kukutana kwa viongozi hao, kunakuja huku wajumbe wa Bunge Maalumu wakiwa
wamemaliza kujadili sura zote 15 zilizokuwa zimesalia na tayari baadhi
ya kamati zimemaliza kupiga kura wakisubiri kuingia bungeni Septemba 2
kwa kazi ya kupigia kura sura kwa sura.
Kuhusu viongozi wa Ukawa, alisema wanazo taarifa na baadhi yao
walikuwapo katika kikao cha kujadili kukutana na kiongozi huyo wa nchi,
hivyo akasema lazima watashiriki wakati wowote wakiitwa.
Lipumba
Akizungumzia mkutano huo na Rais, Profesa Lipumba alisema: “Tunakutana
na Rais Kikwete kwa sababu sisi ni wanachama wa TCD.” Alipoulizwa juu ya
msimamo wa Ukawa, alisema lengo ni kutafuta mwafaka ili mchakato wa
kupata Katiba Mpya uendeshwe kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
“Kikubwa tunachokitaka ni maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya
Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Warioba kuheshimiwa na siyo
kuchukuliwa maoni mengine kama inavyofanyika sasa huko bungeni,” alisema
Profesa Lipumba.
Mbowe
Mbowe alisema Katiba Mpya ni kwa masilahi ya Watanzania wote na Taifa
lao, hivyo inapotokea mikutano kama hiyo na kwa hali ilivyo sasa, hakuna
mtu mwenye nia njema atakayekataa kushiriki. Kikubwa ni kwamba hatuwezi
kubadili msimamo wetu na huo ndiyo ukweli,” alisema.
Kuhusu Bunge hilo kupokea maoni ya makundi mbalimbali wakati tayari
ukusanyaji wa maoni umeshafanywa na Tume ya Jaji Warioba, Mbowe alisema,
“Ndiyo maana tulisusia vikao vya Bunge la Katiba, nadhani sasa
Watanzania wamejua kwa nini tulitoka nje.”
Mbowe alisema kuwa mchakato wa Katiba unaendeshwa kwa mujibu wa sheria,
lakini hivi sasa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samwel Sitta analiendesha
Bunge hilo kinyume na sheria hiyo... “Ukusanyaji wa maoni unaofanyika
sasa ni fedheha kwa CCM na Serikali, ni utoto na aibu wa CCM. Kwa sasa
Ukawa tumetulia tunatazama hali inavyokwenda na tuna mipango yetu ambayo
tunapanga. Kama hali ikiendelea kuwa hivi tutachukua uamuzi mgumu ili
dunia nzima ijue.”
James Mbatia
Alisema wako tayari kukutana na Rais Kikwete kwa ushauriano kwa sababu
suala la maridhiano ni la msingi na viongozi wote wa TCD walikubaliana
Agosti 23.
“Mwaliko tumeupata na tutashiriki. Bunge linaweza kuendelea kwa taratibu
zake za kisheria, lakini suala la mashauriano, lazima tukae tuangalie
ni jinsi gani Taifa letu linaweza likavuka kwa maridhiano kwa amani na
utulivu,” alisema.
Kauli ya Ikulu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu alisema Rais Kikwete
yuko tayari kukutana na viongozi wa vyama vya siasa muda wowote... “Wao
wafuate utaratibu tu, Rais hawezi kukataa kukutana nao na hilo amekuwa
akilisema mara nyingi tu.
http://www.mwananchi.co.tz/
No comments:
Post a Comment