Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umemtaka Rais Jakaya Kikwete kusitisha
Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini Dodoma na iwapo hatafanya
hivyo utaongoza maandamano nchi nzima.
Umoja
huo pia umeeleza kuwa kuendelea kwa Bunge hilo ni sawa na kuvuruga
mchakato wa kupata Katiba Mpya, kuiweka nchi rehani, kufuja fedha za
walipakodi, kuwahadaa Watanzania kwa kupitisha Katiba isiyotokana na
maoni yao, huku kanuni zikibadilishwa na kuingizwa mambo ya Tanganyika
katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kadhalika,
umemtaka Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya
ukaguzi maalumu wa matumizi ya fedha za Bunge hilo kwa maelezo kuwa
zinatumika bila maelezo sahihi.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, mwenyekiti mwenza wa umoja
huo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) akiwa na wenyeviti wenzake, Freeman
Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), alisema hawatataja
muda lakini wanataka jambo hilo lifanyike haraka iwezekanavyo.
“Iwapo
Rais Kikwete hatatumia mamlaka yake kusitisha Bunge na kukubali
liendelee kinyume na matakwa ya wananchi, Ukawa tutawaongoza Watanzania
kupaza sauti kupinga najisi inayotiwa kwenye maoni yao, kupitia
maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima,” alisema Mbatia.
Akizungumzia
iwapo Rais anayo mamlaka ya kusitisha vikao vya Bunge hilo, Wakili na
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jesse James alisema
anaweza kufanya hivyo kwa kutumia dhamana ya uongozi aliyonayo, lakini
kisheria hawezi kutokana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kutokuwa na
ibara inayompa mamlaka hayo.
“Rais
ni Amiri Jeshi Mkuu, Mkuu wa nchi na Serikali. Majukumu hayo ndiyo
yanayomfanya awe na uwezo wa kusitisha shughuli za Bunge hilo, hasa
akiona theluthi mbili ya wajumbe kutoka kila upande kwa ajili ya kufanya
uamuzi haitapatikana.”
Aprili
16, mwaka huu wajumbe wanaotokana na vyama vya siasa vinavyounda Ukawa
na baadhi kutoka Kundi la 201, walisusia vikao vya Bunge hilo wakitaka
msingi wa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba usibadilishwe, wakipinga
uamuzi wa CCM kutaka kuingiza mfumo wa serikali mbili badala ya tatu
zilizopendekezwa katika rasimu.
Mbatia
alisema Ukawa imechukua uamuzi wa kuandamana kutokana na wajumbe wa CCM
pamoja na wengine 166 walioteuliwa kupitia kundi la wajumbe 201,
kuendelea na vikao vya Bunge hilo na kuingiza mambo yao katika Rasimu ya
Katiba, huku wakilipwa fedha za walipakodi.
“Mambo
wanayoyajadili na kuyachomeka kinyemela kwenye rasimu kama ardhi,
elimu, maji, kilimo, uvuvi, mifugo na serikali za mitaa ni masuala
yanayopaswa kuandikwa kwa kina ndani ya Katiba ya Tanganyika siyo Katiba
ya Jamhuri ya Muungano,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Zanzibar
walijadili wenyewe mambo yao ya ndani na kutengeneza Katiba yao, hivyo
hatuoni mantiki ya wajumbe kutoka Zanzibar kujadili na kuamua mambo ya
Tanganyika. Bunge la Katiba halina sifa za kujadili mambo yasiyo ya
muungano. Hii inaonyesha CCM wamelewa madaraka.”
Alisema
ili Bunge hilo lipate uhalali wa kuendelea yanatakiwa kufanyika
maridhiano ya pande zote zinazovutana na kusisitiza kuwa kinachoendelea
sasa kinatokana na kukosekana kwa uongozi wa kisiasa.
“Wakati
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisema kuwa suala la muundo wa serikali
lilitakiwa kupigiwa kura, Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samwel Sitta
anaendelea kuongoza Bunge kama mchakato ni mali yake binafsi. Baadhi ya
viongozi wa chama hicho wanataka mchakato usitishwe, wengine wanataka
uendelee,” alisema.
Profesa Lipumba alisema: “Wapo
wanaosema kuwa Ukawa tumegawanyika. Hilo siyo kweli kwa sababu
waliotusaliti na kuhudhuria vikao vya Bunge hata asilimia tano hawafiki.
Zaidi ya asilimia 95 hatujakwenda bungeni,” alisema.
Alisema
kuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba alitenga masuala ya ardhi, maliasili na Serikali za Mitaa ili
yaingizwe katika Katiba ya Tanganyika, hivyo kuyajadili mambo hayo
katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano si sahihi.
Mbowe alisema: “Viongozi wanaiacha nchi ijiendeshe yenyewe. Ni kama ndege ambayo rubani yupo lakini ameweka ‘auto pilot’, yaani wameiruhusu ndege ijiendeshe yenyewe.”
Mbowe alisema: “Viongozi wanaiacha nchi ijiendeshe yenyewe. Ni kama ndege ambayo rubani yupo lakini ameweka ‘auto pilot’, yaani wameiruhusu ndege ijiendeshe yenyewe.”
CAG achunguze
Kuhusu
suala la ukaguzi wa hesabu, Mbatia alisema katika vikao vya Bunge la
Bajeti, baadhi ya wabunge walihoji zinakopatikana fedha za kuendesha
Bunge la Katiba na kusema kutokana na hali hiyo, ni vyema CAG
akachunguza kwa undani suala hilo.
Hoja
kutaka Bunge hilo lisitishwe inaungwa mkono na makundi mbalimbali
pamoja na baadhi ya wabunge wa CCM, akiwamo Naibu Katibu Mkuu wa CCM,
Mwigulu Nchemba (Iramba-Magharibi) aliyesema likiendelea bila uhakika wa
kupata akidi ya uamuzi itakuwa ni kupoteza zaidi ya Sh20 bilioni za
walipa kodi na wananchi hawataelewa.
Hata
hivyo, uongozi wa Bunge umesisitiza kuwa vikao hivyo ambavyo awali
vilifanyika kwa siku 67, vitaendelea kwa siku 60 za kazi zilizoongezwa
na Rais Jakaya Kikwete, bila kuhusisha siku za Jumamosi na Jumapili
ambazo zinaongeza muda wa wajumbe kukaa Dodoma kuwa 84.
No comments:
Post a Comment