Dodoma. Kuna dalili hali si shwari ndani ya Bunge Maalumu la Katiba baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kujiuzulu ujumbe wa Kamati ya Uandishi wa Katiba inayopendekezwa.
Habari za uhakika zilizopatikana jana bungeni mjini Dodoma, zinaeleza
kuwa kigogo huyo wa SMZ amemwandikia barua Mwenyekiti wa Bunge hilo,
Samuel Sitta akimwarifu juu ya uamuzi wake huo.
Kamati hiyo ndiyo moyo wa Bunge hilo katika kuandika vifungu, ibara na
sura za rasimu kulingana na mapendekezo ya kila kamati na baada ya
majadiliano na mwisho inawajibika kuandika Katiba itakayopendekezwa kwa
wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.
Kujiengua kwake ni pigo kwa Bunge Maalumu, kwani kunapunguza uhalali wa
Katiba itakayopendekezwa kwani Othman akiwa Mwanasheria Mkuu wa upande
huo wa Muungano ndiye anayepaswa kuwa kinara wa kulinda masilahi ya
Zanzibar wakati wa uandishi wa Katiba inayopendekezwa.
Jana Othman alilithibitisha kuhusu kujiuzulu kutoka kwenye
kamati hiyo, lakini akakataa kueleza sababu zilizomsukuma kuchukua
uamuzi huo akitaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu atafutwe kwani barua yake
ya kujiuzulu ameikabidhi kwake.
“Ni sahihi kwamba nimejiuzulu…hizo sababu ndiyo siwezi kukutajia maana
kwa mujibu wa taratibu za Bunge Maalumu zinapaswa kuzungumzwa na
Mwenyekiti maana barua yangu ya kujiuzulu anayo yeye,”alisema jana.
Hata hivyo, Sitta alipotafutwa jana, alikataa kuzungumza lolote juu ya
taarifa hizo akisema hawezi kufanya mahojiano na mwandishi asiyemfahamu
kwa njia ya simu.
“Kwanza sikujui halafu unataka nifanye mahojiano kwenye simu? Mimi sipo
(Dodoma), nipo Dar es Salaam ninarudi Jumatatu niliondoka huko (Dodoma)
mara tu baada ya kipindi cha asubuhi,” alisema Sitta.
Kwa upande wake, Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad,
alipotafutwa alisema hajaiona barua hiyo ya Othman, lakini kwa
utaratibu, mjumbe anayetaka kuchukua uamuzi kama huo humwandikia barua
mwenyekiti ndipo ishuke chini.
“Mimi bado sijapata taarifa hiyo, labda atakuwa amewasilisha kwa
mwenyekiti akishaipata ndiyo inaletwa huku kwangu,”alisema Hamad.
Alisema kwa sababu nafasi hizo ni uteuzi unaofanywa na mwenyekiti na
kanuni ziko kimya kuhusiana na idadi ya wajumbe katika kamati,
mwenyekiti ndiye mwenye uamuzi wa kuteua mtu mwingine ama kuacha.
No comments:
Post a Comment