Iringa. Waraka
uliotolewa juzi na Jukwaa la Wakristo Tanzania wakitaka mchakato wa
Katiba Mpya usitishwe, jana ulisomwa katika baadhi ya makanisa na sasa
utasambazwa katika jumuiya ndogo za Kanisa Katoliki.
Akizungumzia
waraka huo katika Ibada ya Jumapili, Paroko wa Parokia ya Mkwawa ya
Kanisa Katoliki Jimbo la Iringa, Padri Oscar Rutechura alisema amechukua
uamuzi huo ili kuwawezesha waumini kuelewa vizuri tamko la viongozi wao
wa dini kuhusu mchakato wa katiba unaoendelea.
“Katika
ibada hii ya leo nitatoa mahubiri kwa muda mfupi, nitafanya hivyo ili
niweze kufanya mambo mengi yaliyoko mbele yangu,” alisema Padri
Rutechura kabla ya kusoma waraka huo.
Waraka huo
ulitolewa kwa pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste
Tanzania (FPCT) na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA).
Padri
Rutechura alitaja mapendekezo sita yaliyomo kwenye waraka huo ambayo ni:
Kuitaka Serikali irudishe tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
kulitaka Bunge kuboresha maoni ya wananchi yaliyomo kwenye rasimu ya
Katiba na kuacha kuyadharau na kuyapuuza.
Mengine ni
kutaka mchakato wa Katiba usitishwe, Bunge la Katiba liendeshwe kwa
mujibu wa kanuni, wananchi waendelee kusoma na kufuatilia mchakato na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihusishwe na kupewa mamlaka ya kujibu
maswali yanayojitokeza.
Padri
Rutechura alisisitiza kuwa ametumiwa waraka huo na Askofu wa Jimbo la
Iringa, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa ambaye kwa sasa ndiye Rais TEC
kwa ajili ya kuusoma kwa waumini wote.
Alisema
baada ya kuusoma angetoa nakala na kuzigawa kwa viongozi wa jumuiya
ndogondogo ili waumini wote wa parokia hiyo wapate fursa ya kuusoma na
kuuelewa na watoe uamuzi sahihi.
Padri
Rutechura aliwataka waumini kuhakikisha wanajiandikisha kwa wingi kwenye
daftari la kudumu la wapigakura pindi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
itakapotangaza kuanza kuandikisha upya wapigakura.
Alisema
hatua hiyo itawasaidia waumini hao kushiriki kikamilifu katika mchakato
wa kupiga kura ya maoni kupata Katiba Mpya au kuipinga, kuchagua
viongozi wanaofaa katika uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu
wa mwakani.
Wakati
huohuo, polisi wilaya mpya ya kipolisi, Mbalizi mkoani Mbeya
wamewakamata waumini 16 wa Kanisa la Katoliki, Parokia ya Songwe kwa
madai ya kutaka kufanya vurugu kwenye kanisa lao.
Paroko wa Parokia hiyo, Ernest Mwashiuya alisema waumini hao walikamatwa jana na kwamba taarifa zaidi zitatolewa na polisi.
Baadhi ya
waliokamatwa walisema tukio hilo lilitokea Jumamosi saa 12 jioni wakati
wanajadili sehemu ya kusalia ibada ya Jumapili baada ya kutokuwa na
imani na paroko wao. Walisema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Paroko
Mwashiuya, Jumapili ya Agosti 24 kutamka kwamba waumini wasio na imani
naye wasifike kanisani hapo tena.
“Polisi
walifika nyumbani kwa Emmanuel Kalomba tulikokuwa tukisali na
kutukamata,” alisema mmoja wa waumini waliokamatwa na kuachiwa kwa
dhamana.
No comments:
Post a Comment