Mdau wa Sanaa
Henry Mdimu (Kulia) akisisitiza umuhimu wa kuwa na mitandao ya kijamii kwa
wasanii (hawapo pichani) katika Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA). Kushoto ni Afisa Sanaa wa BASATA, Augustino Makame.
Afisa Habari wa
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Aristides Kwizela (Kulia) akisisitiza jambo
kwa Wasanii (Hawako pichani) wakati wa Jukwaa la Sanaa lililofanyika mapema
wiki kwenye Ukumbi wa Baraza hilo ulioko Ilala, Sharif Shamba jijini Dar es
Salaam. Katikati ni mdau wa Sanaa Henry Mdimu na Afisa Sanaa wa Baraza hilo
Augustino Makame.
Wadau wa Sanaa
pamoja na Wasanii wakipata elimu kuhusu Nafasi ya Mitandao ya Kijamii katika
Kukuza Sekta ya Sanaa kwenye mapema wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA.
Wasanii
wamesisitizwa juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwani waandaaji wa
matamasha na matukio mbalimbali ya kisanaa sehemu mbalimbali duniani wamekuwa
wakiitumia katika kuwapa kazi.
Akizungumza
kwenye Jukwaa la Sanaa lililofanyika mapema wiki hii kwenye Ukumbi wa Baraza la
Sanaa la Taifa (BASATA) ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam, mdau
wa Sanaa Henry Mdimu alisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona wasanii
wakitumia kurasa zao kuonesha mambo binafsi kama ya mapenzi na matusi wakati
zinapaswa kutumika kwa ajili ya kazi zao za Sanaa na kuwasiliana na mashabiki wao.
Alisisitiza
kwamba si kila kitu kinapaswa kuwekwa kwenye kurasa za kijamii za wasanii na kwamba
lazima wasanii wajifunze kutenganisha maslahi au masuala yao binafsi dhidi ya
yale ya wapenzi wao na kwamba Sanaa iko kwa ajili ya walaji na si wasanii
pekee.
“Wasanii
hawana budi kuelewa kuwa hawatengenezi sanaa au kurasa za mitandao ya kijamii
kwa ajili yao. Wanaitengeneza ili kuwasiliana na mashabiki wao kuhusu kazi
wazifanyazo na kutafuta fursa za masoko na kazi nje. Lazima waelewe mapromota
wa kimataifa hutumia sana kurasa hizi katika kutoa fursa” alisisitiza Mdimu.
Aliongeza
kwamba, msanii yeyote anayefanya kazi ya Sanaa kama kazi yake lazima afikirie
kutumia mitandao hii ya kijamii kiweledi katika kujitangaza kwani kutokufanya
hivyo ni bora kufanya kazi nyingine maana hiyo ndiyo njia kuu kwa sasa ya
kujitangaza na kupata fursa za maonesho mbalimbali ya kimataifa kwa gharama
nafuu.
Kwa
upande wake Afisa Sanaa kutoka BASATA, Augustino Makame alisema kwamba Baraza
limekuwa mstari wa mbele kusisitiza matumizi sahihi ya teknolojia za kupashana
habari muiongoni mwa wasanii na kwamba sasa ni muda wa wasanii kuona umuhimu wa
mitandao hii ya kijamii na kuitumia ipasavyo katika kukuza Sanaa zao.
No comments:
Post a Comment