10 October, 2014

MBUNGE WA CHADEMA AAPA KUZUNGUKA NCHI NZIMA



Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini ameapa kuzunguka nchi nzima kuwahamasisha Watanzania kudai kufufuliwa kwa Taifa la Tanganyika na kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa.

Selasini alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki katika sherehe za uzinduzi wa tawi la Chadema katika Kijiji cha Mande wilayani Moshi Vijijini lililozinduliwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya (Chadema).
Katiba inayopendekezwa ilipitishwa bungeni Oktoba 3, mwaka huu bila ya kuwapo kwa wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Tutazunguka nchi nzima na kitakachotuzungusha ni kuwaomba nyinyi Watanzania kila mmoja awe mhubiri kwamba tunataka Tanganyika yetu na Katiba yetu,” alisema Selasini na kuongeza:
“Katiba iliyopo siyo yetu, haibebi maoni yetu na ikija kwetu kura yetu sisi itakuwa ni hapana kwa sababu katika Katiba ile hakuna maoni yetu. Nawaomba sana tuhubiri hili”.
Selasini alisema tangu walipoamua kutoka katika Bunge la Katiba Aprili 16, mwaka huu baada ya kuona maoni ya wananchi yanafinyangwa, wamekuwa wakitaka maridhiano lakini wenzao Chama cha Mapinduzi (CCM) hawakutaka.
“Tangu tumetoka tumekuwa tukishauri kwa sababu Katiba siyo jambo la kulazimishana ni jambo la maridhiano. Tukawaomba maridhiano lakini hawataki,” alisema na kuongeza:
“Nasema nchi hii wanaitumbukiza kwenye fujo na fujo zote duniani zimesababishwa na ubovu wa Katiba,” alisema Selasini.
Owenya alitumia ufunguzi huo kulaani tukio la kukamatwa na kudhalilishwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee.
Alisema kila Mtanzania anayo haki ya kuonyesha kutoridhishwa na jambo fulani ambalo uamuzi wake ni wa kisiasa na moja ya mambo hayo ni Katiba ambayo ni sheria mama ya nchi.
Mwishoni mwa wiki mwenyekiti huyo alitiwa nguvuni na polisi baada ya kuandamana bila kibali.

No comments:

Post a Comment

UKIONDOA DIPLOMA, DEGREE AU PHD ULIYONAYO, KICHWA CHAKO KINABAKI NA NINI?

Horace Mann - Binadamu wa kwanza kugundua wazo la elimu Albert Einstein aliwahi kuulizwa akili ni nini? What is intellect? Akasema akili ni ...