Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
amesema hatua ya viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), kuingia katika makubaliano ya kushirikiana “ni kaburi
la vyama hivyo.”
Wakati Nape akisema hayo, baadhi ya wasomi
wamesema ni hatua kubwa lakini yenye kuhitaji kuwa na sera na itikadi ya
pamoja. Akizungumza kwa simu jana, Nape alisema Ukawa ni kaburi la
vyama vya upinzani vilivyoungana kwa kuwa vitapoteza utambulisho wao.
“Huu ni mwanzo wa kumomonyoka kwa vyama vya
upinzani, moja vyama hivyo vitapoteza identity (utambulisho) zao na kama
mkutano wenyewe ndiyo umehudhuriwa na watu kidogo vile, basi hali yao
ni ngumu sana,” alisema Nape.
Alisema kutakuwa na mgogoro mkubwa hasa kwenye
nafasi za kugombea kwa kuwa hasa katika majimbo akitolea mfano wa Jimbo
la Ubungo ambalo alisema Julius Mtatiro wa CUF anataka kugombea huku
John Mnyika wa Chadema naye akitaka kutetea nafasi yake.
“Ukawa ni bomu ambalo litawalipukia na kwangu sijaona jambo jema kwa ushirikiano huo,” alisema Nape.
Hata hivyo, Nape alisema jambo moja ambalo vyama
hivyo vimelifanya ni kuunganisha nguvu kupambana na CCM ambayo misuli
yake ni mikubwa.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Kitila Mkumbo alisema ushirikiano huo ni hatua kubwa kwa kuwa angalau
umeweza kuainisha mambo ambayo watashirikiana.
Hata hivyo, Profesa Mkumbo alisema hiyo iwe ni
hatua ya kwanza kushirikiana na hatua ya pili iwe ni kwa vyama vya
upinzani kuungana kabisa na kuwa chama kimoja kiitikadi na kifalsafa ili
kuweza kuwa na vyama viwili vikubwa nchini.
“Nilidhani wangekuwa na sera ya kuweza kuchambua
tofauti za kiitikadi ndani ya vyama na kuja na vipaumbele vya msingi
katika nchi, lakini ushirikiano huo unaonekana ni wa kimadaraka zaidi,”
alisema Profesa Mkumbo.
Alisema itikadi za vyama ni muhimu kuzingatiwa kwa
kuwa ni jambo la msingi katika kuunda Serikali. “Ukiangalia Chadema wao
itikadi yao ni ya kibepari, CUF ni kiliberali na NCCR-Mageuzi ni
ujamaa, sasa wakiunda serikali itakuwa ya itikadi gani? Hili ni jambo la
kujiuliza,” alisema.
Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, Dk Benson Bana
alisema si jambo baya lakini kinachohitajika ni kujulikana wamejenga
ushirikiano huo kwa msingi gani.
“Hamuwezi kuungana kwa sababu ya kwenda Ikulu.
Tunahitaji wawe na itikadi ya aina moja na sera za mbadala ingekuwa ni
jambo jema zaidi,” alisema Dk Bana na kuongeza: “Wakubaliane sera za
mambo mbalimbali ambayo yataweza kuing’oa CCM na si kujiwekea mkakati wa
kugawana madaraka.”
No comments:
Post a Comment