Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais asiye na Wizara Maalumu,
Profesa Mark Mwandosya amesema kutumia lugha ya kejeli dhidi ya
mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba ilikuwa mbinu ya kupata ushindi katika majadiliano wakati wa
Bunge Maalumu la Katiba.
Mwandosya alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na
waandishi wa habari nje ya ofisi za CCM baada ya kuhudhuria kikao cha
Halmashauri Kuu ya chama hicho ya Mkoa wa Mbeya.
“Katika eneo kama lile ni lazima utumie lugha
ambayo ilikuwa siyo nzuri kwa Tume ya Warioba ili kuweza kusisitiza
jambo fulani au ni njia ya ushawishi ili kuweza kupata ushindi,” alisema
Mwandosya.
“Hivyo tunapaswa kuachana na maneno na maudhi
yaliyofanyika wakati ule na kufuata misingi katika kuhakikisha tunapata
katiba mpya kwa masilahi ya wananchi wetu.”
Alipoulizwa kuhusu Bunge hilo kutozingatia maoni
ya wananchi kwa kuondoa vipengele vilivyokuwa katika Rasimu ya Katiba,
alisema kuwa maoni ya wananchi yaliyotolewa, hayakuwa kura ya maoni.
Mwandosya alitetea kuwa katika vikao vya Bunge
hilo hawakuwa na rasimu yoyote ambayo waliitumia katika kutafuta Katiba
Mpya, zaidi ya ile iliyoandaliwa na Tume ya Warioba.
“Hapa naomba nifafanue vizuri kuwa hatukuwa na
Rasimu yoyote ambayo tuliitumia nje ya Rasimu ya Jaji Warioba na ndiyo
hiyo itakuja kwa wananchi kwa ajili ya kuipigia kura ya ndiyo au
hapana,” alisema.
Kuhusu kuondolewa kwa vipengele ambavyo vinawapa
wananchi nguvu ya kuwawajibisha viongozi wao, Mwandosya alisema
wamefuatilia katiba zote duniani na kugundua kuwa wananchi wana haki ya
kuwawajibisha wabunge wakati wa uchaguzi mkuu. Alisema wabunge wengi
wamekuwa wakishindwa kwenye chaguzi kwa kuwajibishwa na wananchi.
No comments:
Post a Comment