Meja Jenerali Mstaafu Muhiddin Kimario.
Mwili wa aliyekuwa Waziri mwandamizi kwenye serikali ya awamu ya kwanza na pili Meja Jenerali (mstaafu) Muhiddin Mfaume Kimario umewasili leo mchana kwa ndege ya shirika la Ethiopia kutoka nchini India alikokuwa akipata matibabu tayari kwa mazishi siku ya Jumamosi mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Mwili wa Meja Jenerali Kimario uliwasili jana saa saba mchana kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (JKNIA) na kupokelewa na maafisa wa Jeshi, Serikali na wanafamilia.
Ijumaa tarehe 10 Oktoba, 2014 Jenerali Kimario ataagwa kwa heshima za mwisho kwenye kambi ya Jeshi Lugalo. Watu wote wanaotaka kushiriki kuaga mwili wanakaribishwa. Tukio hilo la dakika 90 linatarajia kuanza saa 4 na kukamilika saa 5:30asubuhi.
Baada ya hapo mwili utapelekwa Msikiti wa Maamur ulioko Upanga kwa ajili ya kuswaliwa wakati wa sala ya Ijumaa na baada ya kukamilika kwa sala hiyo mwili utapelekwa uwanja wa JKNIA kwa ajili ya kwenda Moshi, Kilimanjaro kwa ajili ya maziko siku ya Jumamosi.
Mazishi yake yatafanyika saa 10 jioni kwenye makaburi ya Moshi mjini baada ya kuswaliwa kwenye Msikiti wa Riadha.
Marehemu Meja Jenerali Kimario atakumbukwa kama moja ya Maafisa wa kwanza walioanzisha JWTZ, Kamanda wa vita aliyefanikisha kung’olewa kwa nduli Iddi Amin, mwanasiasa shupavu aliyeshika nyadhifa mbalimbali kama Waziri wa Ulinzi na Mambo ya Ndani pamoja na ukuu wa Mkoa kwa mikoa ya Mwanza na Dar-es-salaam na Mkurugenzi wa CDA.
No comments:
Post a Comment