Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhh Dkt. Jakaya Mrisho kikwete.
Steve, aliyepanda jukwaani kuwakilisha wasanii, alitumia dakika zisizozidi tano kumsifu Rais Kikwete kwa mchango wake mkubwa kwa wasanii, akidai ndiye amewafungulia milango ya mafanikio na kwamba watamkumbuka kwa kitendo cha kutambuliwa kwao kikatiba.
Baada ya hapo, mchekeshaji huyo maarufu wa kuiga sauti za watu mbalimbali, alianza kwa kuigiza sauti ya Rais Barack Obama wa Marekani, akimuigiza kumsifu Rais Kikwete kwa kutengeneza katiba mpya na kisha kuwasifu Watanzania na nchi yao kisha akawashukuru kwa kuwaambia asante.
“Mbona hamuitikii jamani Watanzania, au Kiingereza not reachable, naona mna-vibrate tu,” maneno hayo licha ya kuwachekesha mamia ya waliomsikiliza, pia walimfanya Rais Kikwete na Dk. Shein, kuvunjika mbavu hadi kulazimika kulalia meza zao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhh Dkt. Jakaya Mrisho kikwete na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhh Dkt. Mohamed Ali Shein, kwa pamoja wakionyesha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
Alipomaliza kuiga sauti ya Obama, akaendelea kwa kumuiga Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akimnukuu akielezea jinsi Rais Kikwete alivyokwenda kwake na kumuambia kuhusu nia yake ya kutaka kuwa Rais wa Tanzania.
Baada ya kumaliza kumuiga Mwalimu, Steve Nyerere alimgeukia JK na kuiga sauti yake na jinsi anavyofanya baadhi ya mambo katika hotuba. Aliiga staili ya Rais anapowasalimia watu walio mbali, anavyojishika kichwani na maneno yake, hali ambayo kwa muda wote ilimchekesha Rais na viongozi wengine wengi waliokuwepo meza kuu, akiwemo Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Shein, Rais Mstaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Makamu wa Rais Mohamed Bilal na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta.
Mchekeshaji Steven Mengere ‘Steve Nyerere’.
Kabla ya Rais kukabidhiwa Katiba hiyo inayopendekezwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Bunge Maalum la Katiba, Andrew Chenge, alitoa muhtasari wa kilichomo ndani ya Katiba hiyo mpya, ambayo hatua itakayofuata ni kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni kabla ya kuthibitishwa na kuanza kutumika rasmi.
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, ndiye aliyekabidhi katiba hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete aliyeasisi mchakato huo, akizima ajenda ya muda mrefu ya vyama vya upinzani.
No comments:
Post a Comment