Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka.
WAKATI Rais
Jakaya Kikwete akiwa amemuwajibisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka kufuatia kumegewa mgawo wa fedha za
Tegeta Escrow, binti anayedaiwa kuwa mwanaye, amejikuta akipata wakati
mgumu baada ya kumtetea mama yake kupitia mitandao ya kijamii.
Katika Mtandao wa Twitter, binti huyo aliyejitambulisha kwa jina la
Kagem Tibaijuka, alimtetea mama yake akisema fedha zilizowekwa kwenye
akaunti yake zilikuwa ni safi na halali na kwamba ziliwekwa kwa nia
njema ya kuwasaidia kielimu watoto wa kike.
“My mum did nothing wrong except wanting to help young girls get an
education. A school built with my late father. Accepted a donation,”
(Mama yangu hakufanya kosa lolote isipokuwa alitaka kuwasaidia wasichana
kupata elimu. Shule ilijengwa na marehemu baba yangu. Mchango
ukakubaliwa)yalikuwa ni moja ya maneno yake katika mtandao huo wa
Twitter.
Aidha, aliwashambulia wanawake walioonekana kushangilia wakati Rais
Kikwete alipotangaza kumuwajibisha mama yake, akiwaambia kuwa
anawashangaa kushangilia anguko la mwanamke mwenzao na kwamba hata wao
iko siku yatawakuta ya kuwakuta.
Lakini katika mitandao mingine ya kijamii, ikiwemo Facebook na Jamii
Forum inayotembelewa na watanzania wengi, walimshambulia binti huyo kwa
kumwelezea kama mtu aliyelewa fedha na kwamba mama yake alistahili
kuondolewa kwenye nafasi yake, ikiwa ni pamoja na kushtakiwa.
Wachangiaji walioonekana kuchukizwa na utetezi wa binti huyo kwa mama
yake, walisema licha ya Profesa Tibaijuka kuondolewa, pia watu wote
waliotajwa, wakiwemo Waziri Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu, Eliakim
Maswi nao walistahili kuondolewa katika nafasi zao.
Gazeti hili lilimtafuta mama Tibaijuka kupitia simu zake mbili za
mkononi, ili kuzungumzia maoni yake baada ya kukutwa na ajali hiyo ya
kisiasa pamoja na kumuuliza kama Kagem ni bintiye, lakini moja
iliyopatikana, iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa. Hata hivyo baadaye
simu hiyo ilipopigwa, ilionekana imezimwa.
Aidha Kagem mwenyewe, ambaye ofisi zake zinadaiwa kuwa eneo la
Kijitonyama jijini Dar es Salaam, naye hakupokea simu yake ya mkononi
aliyopigiwa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno, hakujibu.
Jumatatu iliyopita, Rais Kikwete alizungumzia suala hilo la fedha
zilizodaiwa na Bunge kuwa ni za umma, kuchukuliwa isivyo halali katika
akaunti iliyofunguliwa Benki Kuu ya Tanzania. Wakati Mwanasheria Mkuu,
Jaji Frederick Werema alijiuzulu mwenyewe na mama Tibaijuka
kuwajibishwa, viongozi wengine waliodaiwa kuhusika na fedha hizo
wanaendelea kuchunguzwa na hatua stahiki dhidi yao zitachukuliwa.
No comments:
Post a Comment