Itakumbukwa
Kamati Kuu iliyopita ya tarehe 13/01/2015, iliyoketi Kisiwandui
Zanzibar ilipitisha ratiba ya shughuli za kawaida za Chama kwa mwaka
2015 na kupanga kushughulikia ratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea
wa CCM vikao vijavyo.
Pamoja
na kutotolewa kwa ratiba hiyo, bado zimekuwepo harakati nyingi za
wanaotaka kuteuliwa na CCM kugombea nafasi mbalimbali hasa ya urais wa
Jamhuri ya Muungano. Harakati hizo baadhi halali, nyingi haramu.
Pamoja
na kutaadharishwa mara nyingi juu ya madhara ya harakati hizo kwa umoja
na mshikamano wa Chama bado baadhi yao wamekuwa wakiendelea na harakati
hizo.
Kwa
muda sasa kumekuwepo na uzushi mwingi juu ya baadhi ya wanaotaka kuwania
nafasi hizo kujadiliwa na hata kuchukuliwa hatua na vikao vya chama.
Maneno haya kwa sehemu kubwa yamekuwa yakisambazwa na wagombea wenyewe
au wapambe wao.
Uzushi
huu, hauna nia njema kwa CCM, unalengo la kukigawa Chama na kuonyesha
kama vile Chama hakina kazi nyingine ila kujadili na kushughulika na
watu hao. Kwa mara nyingine CCM inapenda kuwataadharisha wagombea hao na
wapambe wao kujiepusha na kusambaza taarifa zisizokuwa za kweli. Kwa
kuwa vitendo hivi vinakigawa Chama chetu.
CCM
haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaosambaza taarifa hizi.
Ni vyema wagombea wakawadhibiti wapambe wao na wakajichunga wenyewe
dhidi ya hujuma hizi kwa Chama kwani zitawapotezea sifa ya kugombea.
Wengi
wa wanaosambaza taarifa hizi ni wagombea au wapambe wasiojiamini
kutokana na matendo yao, ambayo hata wao wana mashaka na uadilifu wao.
Hatuoni sababu ya mgombea anayefuata sheria, kanuni na taratibu za Chama
kuhofia kuchukuliwa hatua kila vikao vya Chama vinapofanyika.
Ukitenda kwa haki huna haja ya kuogopa vikao na kuzusha uongo na uzushi usio na ukweli. CCM inaamini matendo haya hayatajirudia.
Aidha
Chama Cha Mapinduzi kinawaomba wanachama na wananchi kuzipuuza taarifa
zinazosambazwa kwa kuvinukuu vyanzo visivyo rasmi, kama kuna hatua au
taarifa kwa umma juu ya hatua yoyote katika mchakato huu basi itatolewa
na wasemaji halali wa Chama na si kutoka vyanzo vya barabarani.
Itakumbukwa
pia baada ya Kamati Kuu iliyopita kukutana tulitangaza kufanyika kwa
kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili kwa ajili ya kushughulikia masuala ya
kimaadili kwenye sakata la Escrow kwa viongozi wa Chama walioko kwenye
vikao vya Chama vya maamuzi.
Jana
kumekuwepo na harakati nyingi za vyombo vya habari na watu binafsi
kujaribu kupata taarifa ya nini kimetokea kwenye kikao hicho cha
Maadili.
Tunapenda
kuwakumbusha kuwa kwa mujibu wa taratibu taarifa za kilichotokea kwenye
kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili huwa hazitolewi kwa umma mpaka baada
ya kufikishwa kwenye Kamati Kuu. Hivyo basi tunawaomba kutulia na
kusubiri taarifa rasmi baada ya kufikishwa kwenye Kamati Kuu kuliko
kuhangaika sasa hivi, jambo linaloweza kusababisha kuokotwa kwa habari
za barabarani ambazo nyingi si za kweli. Tulieni subirini taarifa rasmi.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na;-
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Itikadi na Uenezi.
20/01/2015
Imetolewa na;-
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Itikadi na Uenezi.
20/01/2015
No comments:
Post a Comment