Wapinzani wamekusudia kuikwamisha Katiba
Inayopendekezwa huku wakielekeza nguvu zao kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka
huu kwa lengo la kukiangusha chama tawala.
Mwaka huu una matukio makuu mawili ambayo
yanasubiriwa kwa hamu kubwa na Watanzania wengi ili kuandika historia;
upigaji kura wa kukubali au kuikataa Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi
Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
Mambo hayo yanasababisha wanasiasa na vyama vyao
kuwa katika hekaheka kubwa ili kuhakikisha wanashinda katika matukio
hayo kulingana na msimamo wao.
Kumekuwapo na mgawanyiko katika suala la kuikubali
au kuikataa katiba hiyo na mvutano mkubwa upo kati ya Serikali kwa
maana chama tawala cha CCM na wapinzani chini ya muungano wao wa vyama
vitatu, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi ambavyo vinaunda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa).
Silaha kubwa wanayoitumia Ukawa kwa sasa katika
kuikabili CCM ni kashfa ya ufisadi ya Akaunti Tegeta Escrow na msimamo
kwamba hawaiungi mkono Katiba Inayopendekezwa.
Kutokana na hali hiyo, CUF imefanya mkutano mkubwa
wa hadhara kwenye uwanja wa Mashujaa mkoani Mtwara ambako ilitumia
silaha hizo katika kushawishi wananchi kuiunga mkono.
Katika mkutano huo, mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba alimwalika mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Zitto Kabwe ambaye kamati yake ndiyo ilishughulikia
sakata hilo kwa kutumia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG).
Ulikuwa ni mkutano uliopambwa na shangwe na
nderemo za kila aina kutoka kwa wafuasi wa CUF waliojitokeza kuwalaki
kwenye Daraja za Mikindani na kufanya maandamano ya zaidi ya magari 30,
pikipiki 300 na bajaji 40 na pikipiki huku wananchi wakiwa wamejipanga
kwenye mistari barabarani.
Baadhi walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali,
zikiwemo zilizokuwa na kibwagizo cha “tunataka fedha zetu za Escrow
zirudi... Mtumbwi wa Chenge umetoboka”. Andrew Change ndiye aliyekuwa
mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba.
Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF) alitumia
mkutano huo kuwaomba wananchi wa mkoa huo kupiga kura ya ‘hapana’ kwa
Katiba Inayopendekezwa wakati muda utakapofika.
Alisema Chenge na wabunge wenzake wa CCM
wametengeneza Katiba inayoendelea kulinda maslahi ya wachache badala ya
Watanzania wote.
“Fanyeni hivyo kwa maana maoni yenu yametupwa. Nanyi itupeni Katiba yao kwa kupiga kura ya hapana kwa wingi.
“Lakini hilo litaanza na ninyi kujitokeza kwa
wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura litakapoanza, bila
hivyo hatutaweza kuipinga,” anasema Mnyaa.
Alisema: “CUF itakuwa nanyi bega kwa bega katika
hili kwani tulitarajia kupata Katiba bora lakini imekuwa kinyume chake
na hili halina ubishi kwani mlijionea ninyi wenyewe yaliyokuwa
yanaendelea kuwa bungeni Dodoma.”
Profesa Lipumba aliwaomba wananchi waiunge mkono
CUF kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu na akawashukuru kwa jinsi
walivyokiunga mkono chama hicho kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliomalizika hivi karibuni.
“Wananchi wametuamini na kutuchagua sasa kazi ni
kwetu kuwatumikia kwa weledi na kuonyesha tofauti yetu na walio
kuwapo... Ongozeni kwa misingi ya chama kwa haki sawa kwa wote,”
anasema.
Anaongeza: “Harakati za kuiondoa CCM madarakani
imefika. Utakapofika wakati wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la
wapiga kura hakikisheni mnajitokeza kwa wingi ili muwe na fursa ya
kuchagua na kuitupilia mbali CCM.”
Profesa Lipumba anasema, “Mabadiliko ya nchi hii
yatafanywa na sisi wenyewe kama tutaamua. Dalili tayari mmeanza
kuzionyesha mabadiliko kupitia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Endeleeni
hivyo hivyo kwani CCM imeshindwa na sasa haina uwezo tena wa kuendelea
kutuongoza.”
Zitto na Escrow
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, ambaye ni mbunge
kupitia Chadema, alieleza kwenye mkutano huo jinsi kamati yake
ilivyofichua uozo katika sakata la escrow.
Anasema wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta
Escrow ulikuwa ni Sh306 bilioni na kusisitiza ni lazima zirejeshwe
ingawa Rais Jakaya Kikwete wakati akiongea na wazee wa Mkoa wa Dar es
Salaam Desemba 22 mwaka jana alisema siyo mali ya umma bali ni za IPTL.
“Serikali lazima ichukue hatua mara moja
kuhakikisha fedha zilizokuwamo kwenye akaunti ya Tegeta Escrow Anarudi,
uamuzi wa mahakama ya kimataifa unatekelezwa na fedha za umma
zinarejeshwa Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) na zile za binafsi
zinalipwa kwa wamiliki halali.
“Tanzania haiwezi kuwa nchi ya kubariki utapeli wa kimataifa na
kuchafua sura ya nchi yetu mbele ya jamii ya kimataifa,” alisema Zitto.
“Waliohusika wachukuliwe hatua, maazimio nane ya
Bunge yatekelezwe. hakuna mijadala ya kuwachunguza mara mbili mbili
wengine suala lipo wazi na linafahamika.” anasema Zitto ambaye pia ni
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema).
“Kinachoendelea kufanywa na Serikali ya CCM
kitaigharimu katika Uchaguzi Mkuu ujao kwani ni ishara kwamba
kimeshindwa kuwatumikia wananchi wake na badala yake wachache ndiyo
wanaendelea kuneemeka na rasilimali za taifa huku shule na zahanati
huduma zikiwa bado ziko chini.”
Mtwara, Lindi iko nyuma
Zitto anasema Mtwara ni mkoa ambao kwa miaka zaidi
ya 25 baada ya uhuru ulibaki kuwa ngome imara dhidi ya mabeberu wa
Kireno na waasi wa nchi jirani ya Msumbiji.
Wakati mikoa mingine ikisonga mbele katika
maendeleo ya kiuchumi na kijamii, anasema Mtwara na Lindi zilibaki nyuma
kwa sababu ya kulinda heshima ya mipaka ya nchi.
“Hii ni historia muhimu sana ambayo vijana wetu inabidi waijue na waithamini,” alisema Zitto.
Mkutano huo ulihudhuriwa na halaiki ya watu na
mara nyingi walikuwa wakishangilia. Pamoja na mamia ya wananchi
waliojitokeza katika mkutano huo. Swali ni je, watawaunga mkono
wapinzani na kuwafanya wafaulu katika karata zao mbili; kupiga kura ya
hapana dhidi ya Katiba Inayopendekezwa na kuhakikisha wagombea wa Ukawa
wanashinda uchaguzi mkuu 2015?
Imekuwa kawaida mikutano ya vyama vya upinzani
kufurika watu, lakini unapofika wakati wa chaguzi CCM bado wanashinda
licha ya mikutano yao kutokuwa na misisimko. Je, yawezekana
wanaohudhuria katika mkutano hiyo hawana sifa za kupiga kura? au
wapinzani havawana uwezo wa kushika dola? Majibu ni Kura ya Maoni na
Uchaguzi Mkuu. Oktoba.
No comments:
Post a Comment