Mtu
mmoja amekamatwa mkoani dodoma na maburungutu ya fedha hotelini,
inasemekana alikuwa na lengo la kuwahonga wajumbe wampitishe mmoja wa
gombea uteuzi..nani kamtuma?
Ilikuwa
kama sinema wakati mabegi matatu yaliyokuwa yamesheni mamilioni ya
fedha yalipokamatwa katika hoteli ya St. Gaspar mjini hapa, fedha
zinazodaiwa kuwa zimetolewa na Mfanyabiashara Yusufu Manji, kwa nia ya
kuhonga wajumbe wa vikao vya maamuzi vya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Fedha
hizo zilikamatwa jana katika hoteli hiyo iliyopo eneo la Kisasa, zikiwa
mikononi mwa mfanyakazi wa Kampuni ya Quality Group (T), Amit
Kevaramani, akiwa na hati ya kusafiria M1470774 ya nchini India.
Quality Group (T) inamilikiwa na Yusuf Manji.
Kiasi
cha fedha kilichokamatwa hakijaweza kuthibitika mara moja, ila
waliohusika katika kamata hiyo na baadaye kushuhudia polisi waliofika
eneo la tukio baada ya kuitwa kuhesabu, walisema zinafikia Sh.
725,2050,000.
Mbali
na polisi, maofisa wengine wa vyombo vya usalama walioshuhudia rundo
hilo la fedha za noti za Sh. 5,000 na 10,000 zikiwa zimefungwa kwa
mabunda ya Sh. milioni 10 kila moja, ni maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Usalama wa Taifa.
Waliomkamata
na fedha hizo walishtukia mwenendo wa mfanyakazi huyo, aliyeonekana
akihamisha mabegi makubwa moja baada ya jingine kupeleka kwenye gari
lililokuwa limeegeshwa nje ya hoteli hiyo likiwa na namba za usajili
T687 ANQ Toyota Land Cruiser.
Katika
hoteli hiyo ambayo kulikuwa na wajumbe wengi wa Mkutano Mkuu, na
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM inadaiwa kuwa mamilioni hayo
yalikuwa yanapelekwa kwa kambi ya mmoja wa wagombea watano waliopitishwa
na Kamati Kuu, juzi usiku.
Katika
simu ya mkononi ya mtuhumiwa huyo, ilipokaguliwa na waliomkamata
zilikutwa jumbe fupi za maandishi (SMS) zilizotumwa kwake kutoka kwa
mfanyabiashara (Manji) zikimueleza watu wa kuwapeleka fedha hizo.
Mfanyakazi
huyo akizungumza kwa Kiingereza na Kiswahili cha kubabaisha,
alipogundua kuwa amekamatwa, alijaribu kumhonga mwanamke mmoja begi moja
lenye fedha, lakini alikataa na kuwaita watu wengine kushuhudia tukio
hilo.
Katika
simu yake, miongoni mwa waliotakiwa kupewa fedha ni Mbunge mmoja wa
jimbo lililopo Dar es Salam ambaye alitakiwa kupewa milioni 10 kama
mkopo na alitakiwa asaini vocha ya malipo.
Wengine walionufaika na mgawo huo, ni manaibu waziri wawili, mmoja milioni 15 na mwingine milioni 10.
Aidha, kwenye simu hiyo kulikuwa na orodha ndefu ya watu waliotakiwa kupewa fedha hizo.
Mbali
na mfanyabiashara huyo kukamatwa na polisi, dereva kutoka kampuni ya
Ngatuni Traders, Rashid Nkungu, ambaye alikodishwa na mfanyakazi wa
Manji, aliwaambia waandishi wa habari kuwa alitumwa kwenda kuwapokea
katika uwanja wa ndege wa Dodoma juzi asubuhi majira ya saa 1:30.
Alisema mfanyakazi huyo alikuwa amefuatana na wenzake watatu, wote wenye asilia ya Asia.
“Mimi
hawa Wahindi wamekodisha gari katika ofisi yetu, mimi ni dereva
nimewapokea uwanja wa ndege nikawaleta hapa St. Gaspar, walikuwa na
mabegi yao kutoka uwanja wa ndege mpaka hapa walikuwa wanne,” alisema
Nkungu.
Aidha,
alisema kati ya abiria hao wanne, aliweza kumtambua mmoja wao ambaye ni
Yusuph Manji na baadaye aliwatoa hotelini hapo na kuelekea Benki ya
CRDB tawi la Dodoma.
Alisema aliwapeleka benki watatu na baadaye akawarudia wawili mmoja wao akabaki benki.
Walipofika hotelini abiria hao walimchukua mwenzao mmoja kisha wakaelekea uwanja wa ndege Dodoma.
“Hakuna
Mswahili hata mmoja aliyekuja kuwapokea wote walikuwa Wahindi na hakuna
mtu aliyekuja kuwapokea zaidi yangu mimi, kuna mmoja nilimtambua ambaye
ni Manji,” alisema Nkungu.
Alisema
baada ya kuwapeleka uwanja wa ndege, Nkungu alisema kuwa alipita benki
kumchukua aliyebaki huko, alitakiwa aingize gari kwenye uzio wa benki,
kisha alitoka mfanyakazi huo akiwa na begi.
“Baada
ya kuwarudisha hapa nikalipwa hela kiasi cha Shilingi laki tatu
nikaondoka, kurudi zangu nyumbani na tukaagana vizuri na leo asubuhi
(jana) akanipigia tena nimfuate nimpeleke airport namba yake sikuwa
nakumbuka inaishia namba 24,” alisema Nkungu.
Hata
hivyo, alisema baada ya kufika na kumsubiri nje mfanyakazi huyo alitoka
na kupakia kwenye gari begi la kwanza na kumtaka dereva huyo asikae
ndani ya gari na pia akarudi kupakia begi la pili na kumwambia aendelee
kusubiri nje, lakini baadaye akaona mtu anakuja na kupiga picha gari
mbele na kuchukua ufunguo na kuzima gari.
Kwa
upande wake, Meneja wa Hoteli hiyo, Denis Johannes, alisema mgeni huyo
alipokelewa juzi katika hoteli hiyo akidai kuwa alitumwa na ubalozi wa
India na kulazimika kumpatia chumba kimoja.
“Sisi
kama hoteli mgeni tunamsikiliza na tuna uhusiano mzuri sana balozi zote
Tanzania, Balozi yeyote yule akikosa nafasi tunampa kipaumbele, na
walipoingia walisema wao wametumwa na balozi ya India, na kuangalia
alivyo walisema wamekosa vyumba katika hoteli ya Moreno wakasema kwa
hiyo wamekuja hapa,” alisema Meneja huyo.
Alisema
awali aliwajibu kuwa hana taarifa za kuwapo kwa chumba kwa ajili yao,
lakini kwa kuzingatia ushirikiano na balozi zilizopo wakaamua kumpatia
chumba kimoja.
Hata
hivyo, baada ya kukagua nyaraka za kujisajili kulala hotelini hapo,
aligundua kuwa maelezo binafsi ya mteja huyo ni tofauti na alivyojieleza
awali.
*Imeandikwa na Godfrey Mushi, Editha Majura, Jacqueline Massano na Agusta Njonji,
DodomaCHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment