Mgombea wa urais kupitia Chadema, Edward
Lowassa ameituhumu CCM kuwa ni hodari wa kuiba kura hivyo akawataka
wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili hata sehemu ya kura hizo
ikiibiwa, Ukawa ishinde kwa kishindo.
Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani aliuambia umati wa wafuasi wa
Ukawa uliojitokeza jana kumpokea katika ofisi za makao makuu ya CUF
yaliyopo Buguruni kuwa ili kufanikisha ushindi wa kuwawezesha kuingia
ikulu hawana budi kushikamana, kushawishiana kupiga kura kwa wingi na
kuzilinda Oktoba 25.
Kauli hiyo ya Lowassa ambaye amelelewa kisiasa na CCM tangu alipojiunga
akiwa mdogo mwaka 1977, inaendeleza tuhuma ambazo hutolewa na vyama vya
upinzani kuwa chama hicho huchakachua matokeo wakati wa uchaguzi.
Hata hivyo, Lowassa hakuwa na vielelezo wala kuthibitisha kuhusu tuhuma hizo dhidi ya chama chake cha zamani.
“Tukiwa na umoja, tukiwa na mshikamano tutawaondoa Jumapili asubuhi
sana. Tutahitaji mshikamano, tatahitaji ushawishi wa kupiga kura tupate
angalau asilimia 90 ili wakiiba asilimia 10 tuwasamehe,” alisema Lowassa
katika hotuba yake iliyokuwa inakatishwa na kushangiliwa na na salamu
ya CUF ya “Hakiii” na kujibiwa “kwa wote.”
“Hodari sana wa kuiba CCM kura. Sasa tupate kura nyingi za kutosha hata
wakiiba kura hausikii na kuna usemi wa Chadema unaosema ‘piga kura,
linda kura’ na sisi CUF ni hodari sana wa mambo hayo.”
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipotafutwa kwa simu
kuhusu madai hayo, alijibu kwa ujumbe wa maneno kuwa asingeweza
kuzungumza bali atumiwe ujumbe, na alipotumiwa ujumbe huo hakujibu.
Lubuva: Aeleze wanaibaje
Akizungumzia madai hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
Jaji mstaafu, Damian Lubuva alisema Lowassa angeeleza jinsi wanavyoiba
kura.
“Ili kutoa majibu ya uhakika naomba tufanye utafiti wa kutosha juu ya
tuhuma hizo, lazima tujue ni njia zipi watu wanaiba, vinginevyo
nitaeleza kitu ambacho sina ufahamu nacho. Yeye (Lowassa) kama mtu
aliyekuwa serikalini lazima ana ufahamu walikuwa wanaiba vipi,
angeeleza.”
Tume huwa inaendesha uchaguzi kwa mujibu wa taratibu na sheria na iwapo
kuna mtu anasema kura zinaibwa ajitokeze aeleze kinagaubaga ili ofisi
yake ifanye utafiti wa kina.
“Naomba nieleweshwe kura huwa zinaibiwa vipi? Hii imekuwa ni hisia,
wengine wanasema tutaibiwa kura zetu wakati upande mwingine unasema hawa
wataleta fujo kwa visingizio vya kuibiwa kura,” alisema Jaji Lubuva.
Lowassa ambaye alihamia Chadema siku 11 zilizopita na baadaye kuteuliwa
kugombea urais kwa mwamvuli wa Ukawa kupitia Chadema, alisema safari ya
Ikulu itafanikishwa kwa kupiga kura na siyo maandamano, hivyo Watanzania
watunze shahada za kupigia kura. Hata hivyo, hakuendelea kueleza undani
kuthibitisha ni namna gani CCM huiba kura.
Kiongozi huyo aliyeonekana mwenye furaha, aliwataka wanawake nao
kujitokeza kwa wingi siku ya upigaji wa kura huku wakiwa wameshapika
vyakula majumbani mwao ili nao wapate fursa za kupiga na kulinda kura.
Lowassa alisema ameingia Ukawa ili kuandika historia ya nchi kukuza
uchumi na kuondoa umaskini na kutekeleza kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere ya “mabadiliko ya kweli yatapatikana nje ya CCM.”
Ukawa kutoyumba
Mbunge huyo wa Monduli anayemaliza muda wake, alisema Ukawa ipo imara
haitayumbishwa kirahisi na wafitini, licha ya baadhi ya watu kujipitisha
kwa viongozi wa juu na kutaka kuwarubuni ili umoja huo utetereke.
“Wanakuja kupitisha hela na kuhongahonga lakini viongozi wapo
imara…hawahongeki hawa! Wanapita na maneno kwenye magazeti ya ufukuzi
ufukuzi, nawaambia muwapuuze,” alisema Lowassa bila kuwataja wahusika.
Alisema kuna baadhi ya watu wanaleta propaganda kuwa Ukawa ikiingia
madarakani nchi haitatawalika kiasi cha kuwatisha wafanyabiashara
kukimbiza fedha zao nje ya nchi, jambo ambalo si la kweli.
“Waongo wakubwa hao…nchi itatawalika kuliko awali, Ukawa ikiingia
madarakani nchi itatulia tuli, wasiwadanganye mkimbize hela zenu..tupo
imara,” alisema.
Juma Duni afafanua
Mgombea mwenza wa urais wa Ukawa, Juma Duni Haji alisema hajahamia
Chadema kutafuta vyeo kwa kuwa ameondoka akiwa Makamu Mwenyekiti wa CUF
na waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na hatua yake hiyo
ni kutimiza za kuing’oa CCM madarakani.
“Ni vizuri mkaelewa kwamba tutafanya kosa kubwa tusipofika ikulu mwaka
huu, tutahitaji kusubiri miaka 50 zaidi maana jamaa hawa wakija kutulia
balaa yao ni mara 100 ya wanayoyafanya. Wanaoleta mabadiliko ni vijana
siyo wazee,” alisema Duni Haji.
Alisema Ukawa wanatakiwa kushirikiana kwa dhati na Watanzania kwa ujumla
kwa kuwa mwaka huu ni wa mageuzi na kila mmoja ana wajibu wa kufanya
kampeni ya kuiondoa CCM ili kutafuta hatima bora ya nchi.
Kauli ya Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuna nguvu nyingi
zinatumika kuivunja Ukawa lakini umoja huo utabaki kuwa imara na
kutimiza malengo yake ya kushika dola mwaka huu kwa nguvu za Mungu.
Alisema vyama vya upinzani vimefanya siasa zao kwa shida kwa miaka 25
huku baadhi ya makada wakifungwa, kufukuzwa kazi, ndoa kuparaganyika,
kufungwa au kufunguliwa kesi mahakamani lakini miezi minane iliyopita
imekuwa migumu zaidi kutokana na baadhi ya watawala kupatwa na hofu
baada ya Ukawa kujiimarisha.
“Safari yetu imebaki kidogo tufike tunakoelekea. Sasa akitokea kiongozi
mmoja wetu bila kujali ni wa chama gani akaona kwamba malengo yetu siyo
ya muhimu kuliko fursa binafsi, huyo hatufai,” alisema Mbowe na
kushangiliwa.
Alisema maandamano ya leo kumsindika Lowassa kuchukua fomu yataanzia CUF
na kupitia ofisi za Makao Makuu ya NCCR-Mageuzi Ilala hadi NEC kabla ya
kurudi ofisi za Chadema Kinondoni.
Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi aliwataka wafuasi wa Ukawa
kujitokeza kwa wingi kumsindikiza mgombea wa urais kupitia umoja huo na
ikiwezekana kila mfuasi apeleke watu 10.
Mbatia amvaa JK
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema Ukawa itaendelea
kuhubiri amani siku zote ili CCM na vyombo vya dola visipate sababu ya
kuwatuhumu na kwamba Uchaguzi Mkuu utafanyika kwa amani.
Alisema Rais Jakaya Kikwete alihubiri chuki dhidi ya wapinzani kwa
kuwaita maadui siku alipozungumza na wafuasi wa CCM baada ya kumpokea
mgombea wa urais kupitia chama hicho, Dk John Magufuli alipotoka
kuchukua fomu za kuwania.
“Sikuamini kama Rais Kikwete angesema maneno yale eti anawaambia
wana-CCM wana mikakati ya kila aina ya kushinda na kwamba ‘msiogope
kujihadhari na nguvu za adui’. Yaani sisi wapinzani ni adui? Ukianza
kuwaita wenzio adui wakati wewe ni amiri jeshi mkuu, nchi hii unaipeleka
wapi?” alihoji Mbatia.
Malim Seif apongeza
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, aliwashukuru wafuasi wa
Ukawa waliojitokeza kumpokea Lowassa wakati wa ziara ya kutembelea ofisi
zao na kwamba moyo huo uendelee hadi Oktoba 25 siku ya kupiga kura.
“Hakuna silaha kubwa kuliko umoja, ushirikiano na mshikimano.
Tukishirikiana tukawa wa kweli wa nafsi zetu bila shaka Lowassa
anasubiri kuapishwa tu na sisi Zanzibar tumeshamaliza kazi,” alisema
Maalim Seif na kushangiliwa na umati wa wafuasi hao.
Hali ilivyokuwa
Mapema kabla ya Lowassa hajawasili Buguruni wafuasi wa CUF walianza
kujikusanya taratibu saa 4 asubuhi kwa kuzunguka na ngoma barabara za
Uhuru na za mitaa kuingia ofisi za chama hicho.
Baadaye umati huo uliongezeka kiasi cha kufunga barabara ya Uhuru kwa
muda wakati Lowassa anaingia saa 6:20 mchana na kupokelewa na Maalim
Seif, Makaidi, Mbatia na viongozi waandamizi wa Ukawa.
Idadi hiyo ya watu iliwapa kibarua maofisa usalama wa Ukawa walioonekana wakihaha kutengeneza njia ili viongozi hao wapite.
Baada ya viongozi hao kuwahutubia wafuasi hao, waliingia katika ukumbi
wa Mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi saa 7:15 mchana na kufanya
mazungumza ya takriban saa moja na baadaye viongozi kutoka nje ya CUF
kuondoka.
Nafasi ya Lipumba
Kikao cha Baraza Kuu kilijadili nafasi ya mwenyekiti iliyoachwa na
Profesa Lipumba na suala hilo liliachiwa Mkutano Mkuu wa chama ambao
utaitishwa baada ya miezi sita kwa kuwa ndio wenye uwezo wa kufanya
uchaguzi huo kwa mujibu wa katiba ya CUF.
Akitoa taarifa ya kikao hicho, Maalim Seif alisema Baraza Kuu limeunda
kamati maalum ya watu watatu itakayofanya kazi na katibu mkuu kwa miezi
sita kabla ya Mkutano Mkuu kukaa na kumchagua mwenyekiti na makamu wake,
nafasi ambazo ziko wazi.
Waliochaguliwa kwenye kamati hiyo ni Twaha Taslima ambaye ni mwenyekiti
na wajumbe wawili ambao ni Aboubakary Khamis Bakary (Waziri wa Katiba na
Sheria Zanzibar) na Sererina Mwijage (mbunge mstaafu wa viti maalumu.
No comments:
Post a Comment