07 August, 2015

SIMULIZI HII IMENISISIMUA. UKIPATA MUDA ISOME NA WEWE USISIMKWE..... NIMEITOA HUKOOOOOO KWENYE GROUP LA WHATSUP


Nipo kwenye wakati mgumu sana.
Nafanya kazi zangu bila uhuru wala
utulivu wa akili. Namuwaza mtoto
wangu ambaye anasoma ‘kindagaten’.
Kila siku nakatiza muda wa kazi, mzee
mzima narejea nyumbani kumlea
mwanangu.
Asubuhi kabla ya kwenda kazini, inabidi
nimwamshe mtoto,nimuogeshe,
nimwandalie kifungua kinywa kisha
nimwandae kwa ajili ya shule.
Baada ya
hapo hutoka pamoja kwenda stendi
nikisubiri gari la shule, akishapanda
nami ndiyo nakwea daladala kuwahi
kazini.
Kila siku mchana natoroka kazini
kuwahi kumpokea mtoto
anaporudishwa na gari la shule.
Namlea mwanangu, namlisha, nacheza
naye, namwogesha, akishalala ndipo
nami napumzika. Sina muda wa
kutosha kufanya kazi zangu, ajira yangu
ipo shakani.
Mateso yote haya yamesababishwa na
housegirl wangu ambaye alitoroka miezi
miwili iliyopita
Nahangaika kutafuta
dada mwingine wa kazi, wamekuwa
adimu kwelikweli. Taarifa za mikoani
mpaka ‘intiria’ kabisa, naambiwa wale
akina dada waliokuwa wanapatikana
kwa urahisi, nao wameadimika.
Wamekwenda wapi jamani?
Eti
wamechepukia kwenye siasa!
Hata housegirl wangu Mwanabolibo
alipotoroka aliacha ujumbe nyumbani
kwamba anakwenda kugombea
ubunge.
Nilishangaa sana! Ubunge
Mwanabolibo atauwezea wapi? Elimu
yake darasa la saba tu, na hayo
majukwaa ya kisiasa atayawezea wapi?
Wiki moja kabla Mwanabolibo
hajatoroka, alikuwa na kawaida ya
kuniuliza maswali mengi sana.
Hivi sifa
ya kugombea ubunge ni nini?
Mshahara
wa mbunge ni shilingi ngapi?
Kama
kiinua mgongo cha safari hii ni shilingi
milioni 238, miaka mitano ijayo si
itakuwa shilingi milioni 400?
Kila nilipokuwa namjibu alikuwa
anaandika kwenye karatasi, sikujua
alichokuwa anakiandika.
Maswali mengi;
Hivi yule Wema Sepetu, ana sifa
gani ya kuwa mbunge?
Au kwa sababu
alishakuwa mpenzi wa Diamond
Platnumz?
Au ni kwa vile vigogo wengi wanamshobokea?
Au ni kwa kuwa
alishakaa kinyumba na yule kigogo wa
Ikulu, sijui anaitwa CK? Eeh Kiondo!
Housegirl wangu alikuwa mtata sana,
aliniuliza;
Yule mjane wa Sajuki,
anaitwa nani vile?
Nikamjibu kwa
mtindo wa kumuuliza, unamaanisha
Wastara?
Eeh, huyohuyo, naye ana CV
gani?
Au kwa sababu alikwenda India?
Ikabidi nami nimuulize kwa nini?
Akaniambia, eeh, maana ukiachana na
sifa aliyojizolea ya kumuuguza Sajuki
kwa upendo na uaminifu mpaka India,
sioni sifa nyingine aliyonayo.
Nikamuuliza anachokusudia kukisema,
akanijibu;
Eti Wastara naye anataka
ubunge, wakati baada tu ya Sajuki
kufariki dunia, ndipo tukaanza
kushuhudia udhaifu wake,
mara yupo
na yule kijana anaitwa Bondi,
ghafla
Wastara akawa mke mwenzake Aunty
Lulu ambaye alishakiri kujiuza.
Mke
mwenza wa Aunty Lulu kweli awe
mbunge?
Kabla sijajibu, Mwanabolibo akaendelea;
Unajua Thea nilikuwa namheshimu
sana, lakini aliniacha hoi kwa ile tabia
yake ya kubinua maziwa juu wakati
alikuwa anajitangaza kuwa ameokoka.
Kwa mfano akishaingia bungeni, si
itakuwa kituko na huo mwendo wake
wa ‘kubusti’ maziwa?
Ila nina siku
sijamuona, sijui kama ameacha!
Mwanabolibo akanishangaa;
Halafu
baba inaonekana wewe unachukulia
haya mambo kuwa ya kawaida sana.
Hivi kweli Steve Nyerere awe mbunge,
si itakuwa balaa jamani?
Huyo Steve si
ndiye yuleyule aliyetibuana na wenzake
Bongo Movie, wakamtimua. ‘Kagrupu’
ka wasanii wasiozidi 10 kalimshinda,
itakuwa ubunge wa jimbo lenye wakazi
zaidi ya laki nne?
Usingizi ulikuwa umenikamata ila hoja
za Mwanabolibo zilifanya uyeyuke,
nikawa namsikiliza; Baba, kwa hiyo
baada ya Oktoba 25 mwaka huu, yule
Uwoya tutasikia anaanza kuitwa
mheshimiwa Irene Uwoya.
Jamani,
kweli ubunge hapa Tanzania ni rahisi
sana.
Huku nikimtolea macho,
nilimuuliza, kwa nini?
Akatiririka mtoto wa kike; Sasa zaidi ya
kuanguka jukwaani Miss Tanzania
2006, akawa mpenzi wa H-Baba,
akachangamka na vigogo fulanifulani,
kisha akamtia umasikini yule aliyekuwa
mume wake,
Hamad Ndikumana
‘Kataut’, akamfanya mpaka ashindwe
kucheza mpira,
Je kuna kuna lingine la
kumuongezea CV ya ubunge Uwoya?
Badala ya kumjibu hilo swali, nilibaki
namshangaa Mwanabolibo, kweli
Mwanabolibo ni zaidi ya nimjuavyo.
Naye hata hakungoja jibu langu,
akaendelea; Ila Uwoya ana dhambi
jamani yule mwanamke, kaka wa watu
alikuwa mcheza soka mkubwa,
anacheza Ulaya, tena tegemeo la Timu
ya Taifa ya Rwanda, Amavubi!
Uwoya
alimpukutisha kipaji chote na fedha
zote, jamaa akageuka baba wa
nyumbani ndani ya Jiji la ‘Darisalama’
mpaka alipoamua kurudi kwao Rwanda.
Mwanabolibo alikuwa ameshika rimoti
ya TV, mara wimbo wa Nana wa
Diamond aliomshirikisha Mr. Flavor wa
Nigeria, ukapigwa,
aliongeza sauti, naye
akaanza kuimba kwa kung’atang’ata
maneno, kilipofika kipande cha
“sankoro…. Sankoro…. Kama Ronaldo”,
sauti yake ilitoka barabara.
Wimbo ulipoisha tu, Mwanabolibo
akaendelea; Tena hili liwimbo
limenikumbusha kitu, Uwoya akiwa mke
wa mtu kabisa si alitembea na
Diamond?
Hivi mwanamke anayeweza
kumdhalilisha mume wake kwa kiwango
ambacho Uwoya alimfanyia mumewe
anawezaje kuwa mbunge?
Tena
mwakilishi wa wanawake, akina sisi
tujifunze nini?
Bila kutafuna maneno, niliuona ukweli
katika maneno ya Mwanabolibo, ila
sikutaka kumkubalia, maana ningempa
kichwa angejiona anajua sana.
Unajua
housegirl mfanye abaki kuwa dada wa
ndani, akijiona ana uelewa mkubwa
ataanza kuzingua.
Sikutaka nimpe sifa.
Mwanabolibo naye wala hakuhitaji
nimfagilie, akasema; Najua tatizo lipo
wapi, inaonekana watu wengi
wanaojiheshimu hawajitokezi
kugombea ubunge, ndiyo maana
tunaona hawa watu wanavamia viwanja
ambavyo siyo ‘saizi’ yao.
Kwa jinsi
mimi ninavyotimiza wajibu wangu
ipasavyo kama dada wa nyumbani,
naamini nina uwezo mzuri wa
kuwasemea wanawake kuliko hao akina
Wema, Thea, Wastara, Uwoya na wengineo.
Sikumbuki hata tuliagana vipi, ila kesho
yake nilipoamka nilikuta Mwanabolibo
ametoroka.
Akaacha ujumbe kwamba
anarudi kwao kugombea ubunge kwa
sababu anajiona yeye ana sifa nyingi
kuliko hao mastaa wa Bongo Movie.
Akasema yeye ana uwezo mkubwa wa
kusinzia na kuitikia “ndiyooo”, kuliko
wabunge wengi ambao wamemaliza
muda wao na kiinua mgongo cha
shilingi milioni 238.
Nikanukuu sehemu ya barua yake:
“Usijali baba nikiwa mbunge
nitakusaidia mambo mengi kwa sababu
na wewe umekuwa mtu mzuri kwangu.
Najua ubunge ni pesa tu, nami naenda
kuuza mashamba ya baba na babu,
nikahonge nipate ubunge.
Kama ni
uwezo wa kujenga hoja, siku hizi
ubunge siyo hoja wala kuuliza maswali
ya kuibana serikali, ni uwezo wako wa
kusinzia ndani ya mjengo, kuitika
‘ndiyooo’,
kupiga umbeya, vyote hivyo
mimi naviweza kuliko waliopita, na
kuliko hao akina Uwoya.
“Hivi baba, kwa ile sauti ya Wema,
anaweza kuitika ndiyo kunizidi,
anaweza kugonga meza kunizidi?
Wewe baki salama na mdogo wangu,
ngoja na mimi nikapambane niwe mbunge, nami
nipate milioni 15 kila mwezi,
shilingi350,000 kila siku za kusinzia tu bungeni
huku nikingoja kiinua mgongo shilingi
milioni 400 mwaka 2020.”
Baada ya housegirl wangu kutimka,
nasikia nyumba nyingi pia
wamekimbiwa na akina dada wa kazi.
Wamekwenda kuwania ubunge,
wengine udiwani, siasa ndiyo dili la kisasa,
kujua kusoma na kuandika tu!
Kisha unaitwa mheshimiwa!
Leo kinyozi nimenyolewa mwenyewe,
housegirl ameninyoa.
Nami nimtakie
kila heri, kweli akifanikiwa, housegirl
wangu nitakuwa na
muita
mheshimiwa
Mwanabolibo.

No comments:

Post a Comment

UKIONDOA DIPLOMA, DEGREE AU PHD ULIYONAYO, KICHWA CHAKO KINABAKI NA NINI?

Horace Mann - Binadamu wa kwanza kugundua wazo la elimu Albert Einstein aliwahi kuulizwa akili ni nini? What is intellect? Akasema akili ni ...