BARAZA
la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), limetangaza
kuunga mkono operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta (Ukuta)
iliyotangazwa hivi karibuni na Kamati Kuu ya chama hicho.
Aidha,
Bavicha wamemjibu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwamba
hana mamlaka ya kuzuia operesheni hiyo kwa kuwa wanaifanya kisheria na
yeye siyo msajili wa vyama vya siasa.
Makonda
aliagiza Jeshi la Polisi kuzuia maandamano ya Ukuta, Ijumaa wakati
akizungumza na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) katika kambi ya Ukonga.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa
Bavicha, Patrobas Katambi, alisema maandalizi ya kuunga mkono operesheni
hiyo yamekamilika kwa nchi nzima.
“Kauli
ya Mkuu wa Mkoa (wa Dar es Salaam) ya kusema kwamba polisi wahakikishe
Ukuta haujengeki, haitekelezeki kwa sababu yeye hana mamlaka ya kufanya
hivyo na wala si msajili wa vyama vya siasa hadi atoe kauli hiyo,” alisema Katambi.
“Zipo kesi nyingi zinazoonyesha wakuu wa mikoa kufanya kazi ambazo haziwahusu, hivyo kauli yake tutaipima kisheria,” alisema na kuongeza:
“Yeye
akitaka aendelee kusema chochote akijisikia, lakini sisi tunamwambia
kwamba mikutano yetu iko pale pale na tutaifanya nchi nzima.”
Katika
mazungumzo yake na FFU, Makonda alisema askari wanafahamu sheria, hivyo
wasisubiri mtu yeyote kuja kuwakumbusha juu ya jambo hilo.
Aidha,
aliwataka polisi hao kutosubiri maelekezo mengine kwa kuwa Amiri Jeshi
Mkuu ambaye ni Rais John Magufuli ameshaagiza kutofanyika kwa maandamano
ya Ukuta yaliyopangwa kuwa Septemba mosi.
Makonda
aliliagiza jeshi hilo kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa na kusiwapo
kitu kinaitwa Ukuta ili wananchi waendelee na kazi zao kama kawaida.
Lakini Mwenyekiti wa Bavicha jana alisema: “Tunamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, ajiandae kutuma jeshi lake kulinda mikutano yetu.”
Kuhusu
onyo la Rais Magufuli aliloitoa akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani
Singida kwamba Chadema isimjaribu kwa Ukuta, Katambi alisema chama hicho
hakimjaribu.
Alisema
Chadema itafanya maandamano nchi nzima kwa sababu kwa njia hiyo
wanamsaidia kutoa mawazo yao kama vyama vya siasa kwa ajili ya kumsaidia
kuendesha shughuli zake vizuri zaidi.
“Hatuna
shida ya kumjaribu Rais, na wala si kwamba tunamchukia, na wala hatuna
sababu ya kupinga uwapo wake, na hata ukiulizwa sasa kwamba Rais wako ni
nani, lazima useme ni John Magufuli,” alisema Katambi.
“Tunapotoa dosari na kasoro tunamsaidia kuendesha nchi yake na watu walio chini yake.”
“Sisi
kama vyama vya siasa tuna haki, tunajua yeye ndiye Rais, kama sisi
hatukuweza kupata nafasi ya hiyo, haimaanishi kwamba ni vita, isipokuwa
kupitia vyama vyetu, tuna sehemu ya kutoa mawazo yetu katika
kuifanikishia serikali yake kuongoza vema pamoja na watu wake wa chini
tena kwa mujibu wa sheria na inamsaidia yeye kuwa bora zaidi.
“Kwa hiyo kauli ya Rais sisi hatuna tatizo nayo.”
Katambi alisema taratibu zote za kisheria katika kutekeleza mikutano hiyo zitafuatwa.
Kamati Kuu ya chama hicho ilisema lengo la operesheni hiyo ni kuzuia matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia nchini.
No comments:
Post a Comment