18 March, 2011

Dereva, konda, abiria nani kiongozi wa basi?


NI muda mwingi huwa natafakari kuhusiana na mwelekeo wa taifa letu na mwenendo mzima wa maisha ya Mtanzania wa kawaida na viongozi kwa jumla.
Najiuliza kati ya makundi haya matatu ni nani aliye kiongozi wa basi? Mwingine ataniambia ni dereva kwa sababu ndiye mshika usukani na mwingine anaweza kuniambia ni kondakta kwa sababu ndiye anayemwambia dereva vituo vya kusimama.
Kwa mtazamo wangu, nasema abiria ndio kiongozi wa basi kwa sababu ndiye anataka pa kushushwa.
 
Pia kwa sababu serikali yetu ni ya kidemokrasia, wananchi ndio wanaopaswa kuwa na sauti na maamuzi katika taifa.
Tukiangalia tafsiri iliyotolewa na Abraham Lincolin aliyekuwa rais wa Marekani ni kwamba serikali ya kidemokrasia ni ya watu, inaundwa na watu na kwa ajili yao .
Kwa tafsiri hii ni dhahiri kuwa wananchi ndio wenye mamlaka ya kutaka nini kifanyike na nini kisifanyike katika taifa wanamoishi, japo katika taifa letu ni kama hatujaweza kufikia hatua hiyo ya wananchi kutoa maamuzi ya mwisho.
Imekuwa kwamba mtu anapochaguliwa kuwa kiongozi anakuwa mtu maalumu, asiyetaka kuchangamana na wananchi waliomweka mahali alipo.
Si vizuri kuwapuuza wananchi waliokuweka madarakani na wenye haki, ni nini kifanywe kwa ajili yao na nini kisifanywe kwa sababu ndio wanaohitaji kulingana na matatizo yao .
Mwananchi ndiye mwenye haki ya maamuzi ya taifa, inapotokea kiongozi kuwa na maamuzi ya mwisho ni matumizi mabaya ya madaraka kwani nchi yenye demokrasia ya kweli serikali ni ya wananchi, kwa ajili ya watu walio wengi, ambapo mwananchi ndiye anapaswa kuwa na uamuzi.
Wananchi wanakosa madaraka waliyonayo, wamekosa kuzifahamu haki zao na hata malengo yao yanafifia.
Wananchi hawa wakiwa kama abiria, basi walilolichagua limeshindwa kufika kule wanakotaka kufika; na wengine wamevushwa vituo vyao walivyotaka kushuka na hawana namna ya kufika walikotarajia.
Ni shida, mateso na mihangaiko kwa ndugu na jamaa zao.
Awali matangazo yalionyesha kuwa basi ni jipya na kwamba lina kasi nzuri kumbe sivyo ilivyo, halina mwendo japo halikufungwa spidi gavana, lilipakwa rangi kwenye mabati chakavu, mwendo wake haueleweki tena.
Abiria wanajuta kuangalia rangi ya basi pasipo kulikagua na hivyo kulazwa wasikotarajia.

Makondakta wa basi wamekuwa adui zao, hawataki kusikia habari zao ni kwa sababu abiria wanawaeleza matatizo yao .
Makondakta wamesahau kuwa anayefanya basi kuondoka kila siku kwenda sehemu husika ni abiria na ndiye wa kusema anahitaji huduma ya namna gani.

   Kwa sababu ya kutojua kwao, abiria wamenyang’anywa haki zao na wanazibembeleza badala ya kuzitaka na kupewa kadiri wanavyozihitaji.
Huduma nzuri zilizoahidiwa kutolewa ndani ya basi hazipo tena. Wakati basi lilipoanza safari kila abiria aliahidiwa kupewa atakacho. Hakuna lililotekelezwa, abiria wanajuta kuchagua basi walilolipanda.
Matarajio yao yanazidi kuota mbawa kila kukicha basi linaonekana kuwa na mwisho mbaya, uaminifu kwa ndani ya basi hilo haupo tena makondakta wananyang’anyana nauli za abiria, wengine wamehamishwa viti na kushushwa kabisa.
Hawana pa kwenda wao na watoto wao, hawajui hatima ya kesho, usalama wao uko mashakani wakilala wakiamka wanamshukuru Mungu wao.
Wakati basi linakaribia kupaki huku makondakta wakiwa wameanza kukatisha nauli kwa ajili ya safari nyingine huku abiria waliomo ndani ya basi wakiwa hawajui hatima yao na ya watoto wao. Ni nani atawafungulia mlango makondakta wamekwishashuka kabla ya basi kusimama?
Makondakta na dereva wanahitaji ruti nyingine huku abiria waliokuwa nao hawajui hatima yao , wameshindwa kuwafikisha walikotaka kufika, wameanza kulipaka basi rangi nyingine iitwayo “Mapinduzi ya kijani” ili abiria walione kuwa ni tofauti.
Inafaa tufahamu, tumwambie dereva atuonyeshe ratiba ya safari yaani atakavyotekeleza ahadi zake kabla ya kukata tiketi yaani kufanya uchaguzi.

La sivyo tutabaki na manung’uniko yetu na kukosa utatuzi wa shida zetu. Ifahamike pia kuwa mwananchi ndiye muamuzi katika kuchagua kiongozi bora kwa ajili ya maendeleo yake.
Imeandaliwa na Amos Nyaigoti

No comments:

Post a Comment

UKIONDOA DIPLOMA, DEGREE AU PHD ULIYONAYO, KICHWA CHAKO KINABAKI NA NINI?

Horace Mann - Binadamu wa kwanza kugundua wazo la elimu Albert Einstein aliwahi kuulizwa akili ni nini? What is intellect? Akasema akili ni ...