Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Alhamisi, Septemba 26, 2013, ametembelea Ubalozi wa Kudumu wa Kenya Umoja wa Mataifa(UN), New York, Marekani na kutia saini Kitabu cha Rambirambi kufuatia vifo vya watu 69 na mamia kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi mjini Nairobi mwishoni mwa wiki.
Rais Kikwete amewasili kwenye Ubalozi wa Kudumu wa Kenya Umoja wa Mataifa, Jengo 866 UN Plaza, kiasi cha saa 8:30 kamili baada ya kutembea kwa mguu na walinzi wake kutoka Makao Makuu ya UN yaliyoko karibu kwenda Ubalozini ambako alipokelewa na Balozi Koki Muli Grignon, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya UN kwa niaba ya Balozi Macharia Kamau ambaye yuko nje ya Marekani.
Baada ya kuwa ametia saini Kitabu cha Rambirambi, Rais Kikwete alizungumza kwa ufupi na wafanyakazi wa Ubalozi huo na kupiga nao picha akisema kuwa amekwenda kwenye Ubalozi huo kuelezea majonzi na hasira yake kufuatia vifo vya watu hao pamoja na kujeruhiwa kwa mamia ya watu katika shambulio la kigaidi lilitokea Jumamosi, wiki iliyopita, katika Kituo cha Maduka cha Westgate, eneo la Westlands, Nairobi.
“Siku ile ya tukio nilikuwa natokea Canada kuja Marekani na nililiona tukio hilo kwenye televisheni, bado nikiwa Canada. Nilimpigia simu Rais Kenyatta na kuzungumza naye. Nilimweleza masikitiko yangu na hasira yangu kwa shambulio hilo dhidi ya watu wasiokuwa na hatia na raia wasiokuwa na ujuzi wowote wa kupigana,” Rais Kikwete amesema na kuongeza:
“Nilimweleza Rais Kenyatta masikitiko na hasira yangu kuhusu kitendo hicho. Nilimwelezea utangamano wa Watanzania na Wakenya katika tukio hilo. Nilimwambia kuwa wananchi wa nchi zote mbili wako pamoja katika kipindi hiki kigumu, ni majirani na watu wale wale. Nilimwambia kuwa tutaendelea kushirikiana katika kupambana na ugaidi kwa sababu wakati wa tukio hilo la Septemba mwaka 1998, Nairobi na Dar ES Salaam wote waliathirika.”
Ameongeza: ”Nilimwambia Rais Kenyatta kuwa Tanzania iko tayari kusaidia katika kuchangia mawazo na raslimali kutafuta suluhisho la tukio hili kama msaada wetu ungehitajika. Nilimtakia yeye na wananchi wa Kenya kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.”
Naye Balozi Koki Muli Grignon amemwambia Rais Kikwete: “Kwa niaba ya wafanyakazi wote wa Ubalozi wa Kenya Umoja wa Mataifa, nataka kukuelezea kuwa umetupa heshima kubwa sana kwa kuja hapa, umetupa hamasa na ari. Pamoja tutapambana kukomesha ugaidi katika eneo letu la Afrika Mashariki. Ujio wako umetushangaza, umemshangaza kila mtu kwenye Ubalozi. Hatukutarajia kabisa. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais.”
Chanzo: Kibonde

No comments:
Post a Comment