Hoteli
ya Singita Grumeti Reserves.
HOTELI
ya Singita Grumeti Reserves, iliyopo Serengeti, Mara, Tanzania, inathibitisha
kufuru ya utajiri uliopo Tanzania.
Singita
ndiyo hoteli nambari moja duniani, ikichukua tuzo hiyo kwa mwaka wa pili
mfululizo. Tuzo hizo hutolewa kila mwaka na taasisi maarufu ya
Marekani, US Travel + Leisure ambayo ‘hudili’ na viwango vya biashara ya utalii
duniani.
Hoteli hiyo, inathibitisha kwamba thamani ya Tanzania ipo juu
mno, ndiyo maana mwekezaji kutoka Afrika Kusini, Luke Bailes, aliamua kufanya
uwekezaji wa hali ya juu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Matokeo hayo, yaliandikwa
Agosti mwaka huu kwenye jarida maarufu kwa kuchapisha matukio ya biashara za
utalii, linaloitwa T+L Magazine. Jarida hilo linamilikiwa na Taasisi ya US
Travel + Leisure.
Tangu kufunguliwa kwake,
Singita Grumeti imekuwa kivutio cha viongozi, matajiri na watu maarufu ambao
mara kwa mara hutinga kujivinjari, vilevile kujionea vivutio vya utalii
vilivyopo nchini.
Kwa mujibu wa US Travel +
Leisure, sababu ya kuipa Singita hadhi ya kuwa hoteli namba moja duniani,
inatokana na muundo wake, huduma zinazotolewa, kuwa ndani ya mbuga kubwa kabisa
ya wanyama duniani (Serengeti), vilevile wageni mashuhuri inaopokea.
Inaelezwa kwamba Singita
Grumeti ndiyo hoteli inayoongoza kwa sasa duniani kwa kupokea wageni wenye
hadhi ya daraja la kwanza, wakiwemo marais, matajiri, wanamichezo, wasanii,
viongozi mbalimbali maarufu ulimwenguni na kadhalika.
HAWA WANATAJWA
KUJIVINJARI SINGITA
Marais wa 42 na 43 nchini
Marekani, Bill Clinton na George W. Bush, kwa nyakati tofauti wamefikia kwenye
hoteli hiyo baada ya kuvutiwa na sifa zake zinazotikisa duniani.
Bilionea wa Kirusi
anayemiliki Klabu ya Chelsea ya Uingereza, Roman Abramovich, alipotembelea
nchini Septemba 2009, inaelezwa kwamba alilala kwenye hoteli hiyo.
Bilionea wa Kihindi,
Mukesh Ambani ambaye kwa sasa ni tajiri namba 19 duniani, alifika nchini mwaka
jana na kufikia kwenye hoteli hiyo.
Wakati alipowasili
nchini, Mekesh alikuwa tajiri namba nne duniani. Ripoti ya mwaka 2011, ilimtaja
kuwa tajiri namba tisa na sasa anashika nafasi ya 19.
Mke wa zamani wa
mwanasoka anayechezea Chelsea ya England, Ashley Cole, Cheryl, alipofika nchini
miaka miwili iliyopita, inaelezwa pia kwamba alifikia kwenye hoteli hiyo.
Mwanamitindo aliye pia
mcheza sinema maarufu wa Hollywood, Marekani, Angelina Jolie na mumewe Brad
Pitt, waliripotiwa kufika nchini na moja kwa moja makazi yao yakawa Singita
Grumeti.
Wengine ambao wanatajwa
kuwahi kupumzika kwenye hoteli hiyo ni mwanamuziki wa Marekani, Sean Carter
‘Jay Z’, mwanasoka Thierry Henry, Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda.
Hata hivyo,
inaelezwa kuwa orodha ya wageni wanaofikia Singita ni kubwa mno, tatizo
hufanywa siri kwa sababu watu wengi mashuhuri ulimwenguni huwa hawapendi
ijulikane kama wamefikia kwenye hoteli hiyo kwa sababu za kiusalama.
SIFA ZA HOTELI HIYO
Ni hoteli yenye eneo
kubwa, kutoka ‘loji’ moja hadi nyingine, inabidi utumie usafiri maalum.
Imegawanywa kwenye ‘loji’
mbili, moja inaitwa Ebony na nyingine ni Boulder.
Hoteli hiyo, pia inaundwa
na ‘loji’ nyingine inayoitwa Castleton Camp ambayo inaweza kuhamishwa kutoka
sehemu moja hadi nyingine.
Bei ya chini kabisa kwa
mtu kulala kwenye hoteli hiyo ni shilingi 2,000,000 na bei hiyo hutegemea na
msimu.
Bei zimetofautiana kati
ya ‘loji’ moja hadi nyingine na mtu kulala kwenye Castleton Camp, inaweza
kugharimu mpaka shilingi milioni 23 kwa siku moja.
Singita Grumeti ni moja
kati ya hoteli za Singita za nchini Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment