Inaelezwa kuwa, hata yule mtangazaji mwenye sauti yenye mvuto
wa aina yake Fatuma Hassan ‘Dj Fetty’ naye yupo kifungoni muda mrefu kabla ya
akina B12 ingawa taarifa hizo hazijathibitishwa rasmi.
Katika mkumbo wa akina B12, mtangazaji mwingine wa
Kipindi cha Ala za Roho, Loveness Malinzi 'Diva Loveness Love' naye
amesimamishwa.
Uamuzi wa kuwasimamisha B12 na Mchomvu ulifikiwa na
uongozi wa Clouds kupitia Mkurugenzi wa Vipindi na Utafiti wa Kampuni ya Clouds
Media Group, Ruge Mutahaba kwa maelezo kwamba, wamekwenda kinyume na utaratibu
wa kazi ambao unaonesha vizuri kwenye mikataba yao.
Pigo hilo limekuwa nafasi ya kutoka jumla kwa kijana
Raymond Mshana ambaye kwa hakika anatumia nafasi hiyo vizuri sana. Raymond
hutangaza Kipindi cha Top 20 kinachoruka hewani kila Jumapili kituoni hapo.
Kama ni msikilizaji wa Kipindi cha XXL kinachoruka hewani
kupitia redio hiyo kila siku (kuanzia Jumatatu – Ijumaa) tangu mishale ya saa 7
mchana hadi saa 10 alasiri, utakubaliana nami kuwa jamaa anajua anachokifanya.
Jambo la msingi kwa Raymond ni kufahamu kuwa uwezo anao,
aongeze bidii zaidi ili aweze kupata nafasi kubwa zaidi ya kuonyesha uwezo
wake. Watu wanaweza kuona shoo zinapwaya kwa namna ama nyingine lakini si kwa
ubora wa kazi – ni mazoea ya sauti za kila siku.
Sishabikii akina B12, Dj Fetty na Mchomvu kuwa nje ya
vipindi hivyo na ni matarajio yangu kuwa watarejea hivi karibuni lakini iwe
changamoto kwa Mshana mwenyewe, kuendelea kukaza ili azidi kuwa matawi ya juu.
Wengi hawamfahamu japo kwa ufupi. Hapa nitakueleza japo
kidogo sana ili upate kumfahamu Raymond.
NI NANI HASA?
Anaitwa Raymond Mshana (25), mzaliwa wa Same,
Kilimanjaro. Raymond ni Mpare, moja ya makabila maarufu sana nchini. Wapare
hutaniana na Wachaga ambao wote ni kutoka mkoani humo. Katika utani wao,
Wachaga wamekuwa wakiwatania Wapare kuwa ni wabahili sana! Tehe...
Elimu yake ya msingi aliipata katika Shule ya Msingi
Olimpio (Dar) na baadaye alikwenda kujiunga na Shule ya Sekondari Marangu
iliyopo mkoani Kilimanjaro ingawa alichaguliwa kujiunga Azania Sekondari kabla.
Kidato cha tano na sita alisomea katika Shule ya
Sekondari
Mbezi Beach. Alipohitimu kidato cha sita, alibahatika
kupata kazi kwa muda mfupi (miezi saba) katika Benki ya NMB kabla ya kujiunga
na Chuo cha Usimamizi wa Fedha ‘IFM’.
UTANGAZAJI
Kituo chake cha kwanza katika utangazaji kilikuwa ni
Runinga ya C2C ambapo aliona matangazo yakihitaji watu wanaojiamini kuwa
wanaweza kutangaza, alipokwenda zali likawa upande wake.
Katika usaili huo uliokuwa na watu wengi, walifanikiwa
kushinda watu wanne; yeye, Zamaradi Mketema, Mussa ‘Kipanya’ George na
Aboubakar.
Baada ya kupata uzoefu kituoni hapo, alibahatika kupata
mchongo wa kazi Clouds FM mwaka 2010, ambapo aliendelea kupiga mzigo hadi sasa,
ingawa hakupata nafasi ya kusikika sana lakini alipokabidhiwa mikoba ya Kipindi
cha Top 20, sauti yake ya dhahabu ikatoka jumla!
HUYU HAPA RAYMOND MSHANA
Raymond Mshana alizaliwa Julai 29, 1987, akiwa na asili
ya Kabila la Kipare. Ni mcheshi, bachela anayeishi Mbezi Beach jijini Dar es
Salaam. Ndoto zake ni kumiliki kampuni au kiwanda kikubwa ambacho hakueleza ni
cha nini.
No comments:
Post a Comment