TAMKO KUHUSU YANAYOENDELEA CHADEMA

MH. MKONO KUMPATIA MH. ZITTO MAGARI MAWILI

Nimesikitishwa na jinsi Chama kikuu cha upinzani ambavyo kwa siku za hivi karibuni kimeingia katika migogoro ambayo inaathari kubwa kwa ustawi wa demokrasia hapa nchini.

Nimesoma kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mimi Mh. (Nimrod Mkono) kumpatia Zitto Kabwe (MB) magari mawili (Land Cruiser pamoja na Nissan Patrol).

Kwanza napenda ifahamike kwamba sijawahi kumpatia Zitto magari. Isipokuwa kuhusu hiyo Land Cruiser; nilitoa msaada wa kuwanusuru kule Tarime kwenye msiba wa marehemu Chacha Zakayo Wangwe (MB) Tarime. Wakiwa wanatishiwa kupigwa (Freeman Mbowe pamoja na Zitto Kabwe) nilijitolea gari langu lenye bendera ya Bunge, liwachukuwe na kuwapeleka Mwanza wakiwa salama, na ilifanyika hivyo. Baada ya kufika Mwanza, Mhe. Zitto aliwasiliana na mimi, kuhusu ununuzi wa gari hilo, nami kupitia kwa wakala wangu Africariers; nilimuuzia Zitto hilo gari.

Kuhusu hilo gari la pili: (Nissan patrol) Mhe. Zitto Kabwe alilikodi, na mpaka sasa anaendelea kulipa vizuri tu; lakini pia ifahamike kwamba hata nyaraka za gari hilo bado ninazo mimi kama mmiliki halali na sijawahi kuhamisha umiliki wake (Transfer of ownership)

KUHUSU KUTOA FEDHA KWA CHADEMA

Nimesikitishwa na ninataka kuweka wazi kwamba, sijawahi kuongea na Tundu Lissu kama inavyodaiwa kwa masuala yoyote binafsi isipokuwa tukiwa kwenye kamati ya Katiba na Sheria.

Ikumbukwe kwamba, nimepita bila kupingwa kwa vipindi vitatu mfululizo (2000, 2005 na 2010). Ni historia ya aina yake; lakini pia uchapakazi wangu kwenye jimbo la Musoma vijijini. Ushindi wangu wa kupita bila kupingwa kwa kiwango kikubwa umekuwa unatokana na bila shaka umahiri wangu kwa kufanya kazi za wananchi kwa kiwango kikubwa.
Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono ametoa ufafanuzi juu ya uhusiano wake na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe.

Hatua hiyo ya Mkono imekuja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kumtuhumu kuwa aliwahi kumpa Zitto magari mawili.

Katika taarifa yake aliyoitoa jana, Mkono alisema kuna magari mawili yanayohusishwa na Zitto na kuyataja kuwa ni Toyota Land Cruiser na Nissan Patrol.

“Sijawahi kumpatia Zitto magari, isipokuwa kuhusu hiyo Land Cruiser, nilitoa msaada wa kuwanusuru Zitto na Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe), kule Tarime kwenye msiba wa marehemu Chacha Wangwe (aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Chadema), kwani walikuwa wakitishiwa kupigwa.”

Alisema alitoa gari hilo lililokuwa na Bendera ya Bunge liwachukue Mbowe na Zitto na kuwapeleka Mwanza... “Walipofika Mwanza, Zitto aliwasiliana na mimi kuhusu ununuzi wa gari hilo na kupitia wakala wangu nilimuuzia,” alisema Mkono.

Kuhusu Nissan Patrol, Mkono alisema lilikodishwa kwa Zitto na mpaka sasa bado analipa gharama za kulikodisha...

“Hata nyaraka za umiliki wa gari hili ninazo mimi mwenyewe kama mmiliki halali. Ninamiliki magari mengi tu hata wewe mwandishi ukitaka Vogue (aina ya gari) nitakukodisha tu,” alisema Mkono.

Alisema wanafahamiana kwa siku nyingi hata kabla ya Zitto kuwa mbunge na kwamba aliwahi kufanya mazoezi kwa vitendo katika ofisi yake (Mkono), alipokuwa mwanafunzi.

Kuhusu tuhuma kwamba anawahonga wapinzani wake wajitoe katika uchaguzi ili apite bila kupingwa alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, 2005 na 2010 alipita bila kupingwa kutokana na uchapakazi wake wa kiwango kikubwa.

Mkono pia alijibu tuhuma zilizotolewa na Zitto jana kwamba Mbowe alipewa mamilioni ya fedha na Mkono kwa nyakati tofauti na kusema hajawahi kutoa fedha zozote kusaidia Chadema.

Zitto akana

Katika hatua nyingine, Zitto ameitaka Chadema kumwandikia mashtaka mapya yaliyoibuliwa na Lissu ili aweze kujitetea.

“Mashtaka yangu ni yale tu ya waraka na kugombea uenyekiti na shtaka moja la masuala ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Kwa kuwa hawakuniandikia mashtaka hayo kinachobakia ni majungu tu, masuala ya kuhongwa magari ni tuhuma zinazorudiwarudiwa bila ushahidi wowote,” alisema na kuongeza:

“Mkono ananihonga ili nimpe nini? Yeye mbunge na mimi ni mbunge pia. Hiyo hongo tunabadilishana na nini? Katika kumaliza Shahada yangu ya Uzamili ya Sheria na Biashara nilifanya `internship’ (mafunzo kwa vitendo) kwa Mkono na hivyo kuna uhusiano wa kikazi wa baba na mtoto.”

Zitto alisema kuwa Mkono ni kama mzee wake na suala la kumpa chochote kile si hoja.

Kitila amruka Slaa

Aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dk Kitila Mkumbo amesema kauli zilizotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbrod Slaa kuwa alikiri kwamba Zitto alikuwa akiujua waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013, ni za kutunga.

Juzi, wakati akieleza uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kuwafukuza uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Dk Kitila, Dk Slaa alisema wakati akihojiwa na Kamati Kuu, Dk Kitila alisema Zitto alikuwa akiujua waraka huo.

“Siyo kweli. Hata siku moja sijawahi kukiri kwamba Zitto alikuwa akiufahamu waraka, kilichosemwa na Dk Slaa ni uongo.”

Mwigamba afafanua

Mwigamba alisema hakuhojiwa na Kamati Kuu kwa sababu yeye ni Msabato na Siku ya Sabato, hairuhusiwi kufanya jambo lolote zaidi ya kumwomba Mungu.

“Waliniita Ijumaa (Januari 3) ili nihojiwe lakini mpaka saa 12 jioni sikuwa nimehojiwa na niliwaeleza kuwa jua likizama sitakubali kuhojiwa kwa sababu itakuwa imeanza Siku ya Sabato,” alisema.

Alisema kikao cha Kamati Kuu kiliendelea Januari 4, mwaka huu, pia hakuweza kwenda kuhojiwa kwa sababu ilikuwa Sabato, pia alikuwa kanisani, “Niliwaambia kuwa nipo tayari kuhojiwa Jumapili, hawakunijulisha kama wameridhia.”


CHANZO:
Mwananchi - Jan 07, 2014