MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) imesema
dawa za Dicloper na Diclofenac zilizopo nchini ni
salama kwa matumizi ya binadamu. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, msemaji wa mamlaka hiyo, Gaudencia
Simwanza, alisema Tanzania haijapiga marufuku
dawa hizo. “Hapa nchini dawa aina ya Dicloper na Doclofenac
hazijapigwa marufuku… bado matumizi yake
hayana athari kwa binadamu, ni dawa salama kwa
matumizi,” alisema Gaudencia. Kauli ya msemaji huyo ni mwanzo wa utaratibu wa
serikali kuzitaka idara, wizara na taasisi zake
kuzungumza na vyombo vya habari kila siku
kueleza utekelezaji wa shughuli zao. Alisema matokeo ya uchunguzi yanayofanywa na
maabara ya TFDA yapo kwenye ngazi za kimataifa
baada ya maabara hiyo kufanyiwa ukaguzi na
Shirika la Afya Duniani (WHO) na kubainika kwamba
inakidhi viwango vya kimataifa. “Kwa sababu hiyo, tumepata ithibati kwa kiwango
cha ISO/IEC 17025:2005 na kupata kibali cha
kuhudumia kutoka taasisi ya nchi zilizo kusini mwa
Afrika (SADCAS). “Pia maabara yetu ni moja kati ya maabara nne
zilizopata ithibati kati ya 12 zilizopo Afrika,”
alisema Simwanza na kuongeza kuwa maabara
nane zilikosa udhibiti. Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
Nsachris Mwamaja, alisema mwaka 2012/2013
serikali imeajiri watumishi 8,869 wa kada
mbalimbali za afya. Mwamaja alisema wengi wa madaktari
walioajiriwa ni waliokuwa wanajifunza kwa
vitendo kwenye hospitali mbalimbali nchini,
ambao walishiriki katika mgomo wa madaktari
uliofanyika kati ya Mei na Juni mwaka jana. “Wengi kati ya waajiriwa hawa hususan madaktari
ni wale waliogoma mwaka jana ambao usajili wao
ulisitishwa kwa muda wakaenda kwenye baraza
lao, huko waliadhibiwa na kurejeshewa usajili
wao,” alisisitiza. Awali, msemaji wa wizara hiyo, alibainisha
mgogoro uliopo kati ya serikali na Kampuni ya
Tanzania Pharmaceutical Industries (TPI) Ltd
inayochunguzwa kwa kina, hivyo aliwataka
wananchi kusubiri matokeo ya uchunguzi huo. Mwamaja alisisitiza kwamba Bohari ya Dawa (msd)
iliuziwa dawa bandia za kupunguza makali ya
ukimwi aina ya TT-VIR 30 toleo Na.0C.01.85 kwa
mujibu wa nyaraka zilizopo na kwamba zilibainika
kuwa ni feki.