Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bi. Terezia
Mmbando (kulia) akitoa taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU na Ukimwi katika
jiji la Dar es salaam kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi
(TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho alipotembelea maeneo mbalimbali ya jiji hilo
kuangalia hatua zilizofikiwa katika kupambana na ugonjwa huo katika ziara yake
ya siku nne.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bw. Raymond Mushi akitoa tathmini ya hali ya maambukizi
ya VVU katika jiji la Dar es salaam na hatua zinazochuliwa na serikali kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali kukabiliana na janga hilo mara baada ya
kupokea ugeni kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi.
Meya wa Manispaa ya Ilala Mh. Jerry Silaa ambaye pia
ni diwani wa kata ya Gongolamboto akitoa ufafanuzi kwa Mwenyekiti wa Tume ya
Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho kwa kuhusu
hatua iliyofikiwa na mikakati ya manispaa ya Ilala katika kukabiliana na
maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.
Meya wa Manispaa ya Ilala Mh. Jerry Silaa akifurahia
jambo na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma
Mrisho (kulia) na Diwani wa Viti maalum Ilala Mh.Batuli Mziya (katikati) wakati
wa ziara ya viongozi wa TACAIDS kata ya Gongolamboto.
Mmoja wa wanachama wa Asasi ya Vijana ya St. Camilus
inayojihusisha na utoaji wa elimu kuhusu VVU na Ukimwi kwa vijana kupitia sanaa
mbalimbali Bi. Aquila Mawenya akisoma taarifa ya utendaji kazi wa asasi hiyo
kwa Mwenyekiti wa wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Dkt. Fatma
Mrisho alipokutana na wanachama wa Asasi hiyo Kiwalani jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti
Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho (katikati) akiwa na baadhi ya wanachama
Asasi ya Vijana ya St. Camilus inayojihusisha na utoaji wa elimu kuhusu VVU na
Ukimwi kwa vijana kupitia sanaa mbalimbali alipowatembela eneo la Kiwalani
jijini Dar es salaam.
Baadhi ya viongozi wa manispaa ya Ilala wakiongozwa
na Meya wa Manispaa hiyo Mh. Jerry Silaa (katikati) wakiwa na Mwenyekiti wa
Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Dkt. Fatma Mrisho (wa tatu kutoka kulia)
alipotembelea Kata ya Gongolamboto kuangalia hatua zilizofikiwa katika
kupambana na ugonjwa huo katika ngazi ya kata.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi
(TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho akizungumza na viongozi na wakazi wa
kata ya Gongolamboto jijini Dar es salaam alipotembelea eneo hilo kuangalia
hatua zilizofikiwa katika kupambana na ugonjwa huo katika ngazi ya kata.
Katibu wa mtandao wa Vikoba vya watu wanaoishi na
VVU (IDINEPA VICOBA) kata ya Kiwalani Bw. Shaban Mwasa Wamikole akimkabidhi
risala ya kikundi hicho Mwenyekiti wa wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti
Ukimwi Dkt. Fatma Mrisho alipokutana na wanachama wa kikundi hicho katika kata
ya Kiwalani jijini Dar es salaam.
====
=======
MAAMBUKIZI
YA VVU JIJINI DAR ES SALAAM YAPUNGUA.
Na. Aron
Msigwa –MAELEZO.
18/6/2014.
Dar es salaam.
Licha ya
kukabiliwa na changamoto mbalimbali za udhibiti wa maambukizi mapya ya Virusi vya
Ukimwi na Ukimwi, Jiji la Dar es salaam limefanikiwa kupunguza kiwango cha
maambukizi kutoka asilimia 9.8 za mwaka 2007/2008 hadi kufikia asilimia
6.9 kutokana na jitihada zilizofanywa na serikali zikiwemo za uundaji wa
kamati shirikishi za mkoa kudhibiti maambukizi hayo.
Hayo
yamebainishwa katika taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU na Ukimwi
iliyotolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bi. Terezia Mmbando kwa
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho
alipotembelea maeneo mbalimbali ya jiji hilo kuangalia hatua zilizofikiwa
katika kupambana na ugonjwa huo.
Akisoma
taarifa hiyo leo jijini Dar es salaam Bi. Mmbando ameeleza kuwa janga la Ukimwi
ni tatizo la dunia nzima na limekuwa kikwazo cha maendeleo ya jamii hapa nchini
na kuongeza kuwa jitihada za kudhibiti maambukizi ya Ukimwi jijini Dar es
salaam zimechukuliwa kupunguza maambukizi ikiwa ni pamoja na uanzishaji rasmi
wa kamati za kuratibu na kusimamia shughuli za kudhibiti Ukimwi kuanzia ngazi
ya mkoa, halmashauri, ngazi ya kata na mtaa.
Amesema
jiji la Dar es salaam linakabiliwa na changamoto ya ongezeko la kubwa la watu
ikilinganishwa na mikoa mingine hali inayochangia mwingiliano wa
tamaduni, shughulim mbalimbali, masuala ya kijamii,kimila na kiuchumi na
kuongeza kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2012 idadi ya watu
imefikia 4,364,54, wanaume wakiwa 2,125,786 na wanawake 2,238,755
sawa na ongezeko la asilimia 5 kwa mwaka.
Hali ya VVU
na Ukimwi mkoa wa Dar es salaam. Hali ya
maambukizi ya Ukimwi katika jiji la Dar es salaam kwa mujibu wa matokeo ya
utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuhusu viashiria vya Ukimwi na
Malaria mwaka 2011/2012 inaonesha kuwa kiwango cha maambukizi ya VVU kitaifa ni
wastani wa asilimia 5.1 ambapo maambukizi kwa wanawake ni asilimia 6.2 na wanaume
ni asilimia 3.8.
Sababu za
maambukizi. Miongoni
mwa sababu zinazochangia kuendelea kuwepo kwa maambukizi mapya ya VVU katika
mkoa wa Dar es salaam ni pamoja na kasi ya ukuaji wa jiji na shughuli za
kibiashara hali inayosababisha mwingiliano wa watu na mahusiano ya kimapenzi
pia baadhi ya wakazi kutobadili tabia licha ya kupatiwa elimu ya kujikinga na
maambukizi ya ya ugonjwa huo.
Sababu
nyingine ni hali ngumu ya uchumi hususani maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa
wakazi wa kipato cha chini,kuongezeka kwa vitendo vya ngono isiyo salama
hususani maeneo yenye nyumba nyingi za kulala wageni, kumbi za starehe,
madangulo na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi ya madereva wa magari ya
masafa marefu.
Aidha,
ngoma za usiku zinazokesha hasa maeneo ya pembezoni mwa jiji
zinazoambatana na unywaji wa pombe kupita kiasi na uwepo wa makundi
maalum ya watu wanaofanya biashara ya ngono na wale wanaotumia dawa za kulevya
hali inayowafanya washindwe kutoa maamuzi sahihi ya kujikinga na VVU ni miongoni
mwa sababu zinazochangia maambukizi mapya ya VVU.
Hatua
zilizochukuliwa kudhibiti maambukizi. Mkoa kwa
kushirikiana na halmashauri za manispaa na wadau mbalimbali pamoja na mambo
mengine umeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na
maambukizi ya VVU,kuhamasisha upimaji wa hiari wa VVU pia kuongeza nguvu katika
mapambano ya kuzuia maabukizi kutoka mama kwenda kwa mtoto kupitia kliniki za
afya ya uzazi.
Hatua
nyingine ni utoaji wa huduma za tiba na virutubisho kwa wagonjwa, kuwahudumia
watoto yatima na wale wanaoishi mazingira hatarishi pia kutoa mafunzo ya
ujasiriamali na kuhamasisha uundaji wa vikundi vya ujasiriamali kwa wanaoishi
na VVU ili waweze kumudu gharama za maisha na uundaji wa vikundi vya sanaa vya
vijana kwa ajili ya kutoa elimu ya VVU na Ukimwi kwa vijana walio katika
mazingira hatarishi ya maambukizi katika jiji la Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment