Waziri Mkuu Mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim amesema
hakutarajia kusikia kauli za Rais Jakaya Kikwete alizozitoa bungeni
kukosoa Rasimu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa sababu walikuwa wanampa
taarifa kwa kila hatua waliyokuwa wanafikia kabla ya kutoa rasimu hiyo.
Dk Salim alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam wiki iliyopita.
“Hatukutarajia kama hali ingefikia hatua iliyofikia,” alisema
Dk Salim na kuongeza: “Lakini Rais ana uamuzi wake na anazingatia mambo
mengine mengi.”
Akilihutubia Bunge maalumu la Katiba Machi 21, mwaka huu Rais
Kikwete aligusia mambo saba ya msingi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba
na kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha kuwa mengine hayawezekani
kutekelezeka. Miongoni mwa mambo hayo ni muundo wa Serikali. Alipinga
waziwazi pendekezo la serikali tatu lililopendekezwa na Tume na kuegemea
katika muundo wa serikali mbili na idadi ya watu walioupendekeza
akionyesha kuwa ilikuwa ni ndogo.
Pia alisema ni vigumu kutenganisha uwaziri na ubunge kama
ilivyokuwa imependekezwa na Tume kwa maelezo kuwa mawaziri wanatakiwa
kuwepo bungeni ili kujibu hoja za Serikali.
Jambo lingine alilokosoa katika Rasimu ni pendekezo la mtu
kupoteza ubunge kwa sababu ya kuugua kwa miezi sita mfululizo huku
akisema baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo
mengi ambayo hayapaswi kuwamo katika Katiba, bali katika sheria
zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Katika mahojiano hayo maalumu, Dk Salim alisema baada ya
kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume aliacha kuhudhuria vikao vya chama chake
ili aweze kufanya kazi hiyo kwa usahihi na alimtaarifu Mwenyekiti wa CCM
ambaye ni Rais na katibu mkuu wake na walimwelewa.
Alipoulizwa anaitazama vipi Tanzania iwapo Katiba Mpya
haitapatikana, Dk Salim alisema ana wasiwasi kwa kuwa suala hilo
limeingizwa siasa na Bunge Maalumu limegeuka la kisiasa hivyo linaweza
kuleta matatizo.
“Tuko katika hali ambayo si nzuri inayohitaji uongozi
thabiti, viongozi wote watambue umuhimu wa zoezi hili kwa lengo la
kulinda amani na utulivu wa nchi yetu,” alisema.
Alisema kunahitajika ufumbuzi wa kudumu na hicho ndicho
kipimo cha uongozi kwa CCM, Chadema na wengine kwa kutafakari masilahi
ya Watanzania wa leo, kesho na keshokutwa.
Nini kifanyike?
Dk Salim alisema jambo muhimu sasa ni pande mbili
zinazoshindana kuhusu idadi ya Serikali kutumia mwezi ujao wa Julai
kukaa pamoja na kumaliza tofauti zao ili Bunge la Katiba liendelee bila
misuguano.
“Mwezi huu wa Julai ni muhimu sana, ni mwezi pekee uliobaki
wa kuwaweka pamoja wanaotofautiana. Kila jitihada zinatakiwa kufanyika
ili kuhakikisha Bunge Maalumu linakutana tena Agosti na wapinzani
waliosusa wanarejea ili kumaliza kazi hiyo kabla ya kutoa rasimu ya tatu
kwa ajili ya kura za maoni,” alisema na kuonya kuwa kuendelea na katiba
ya sasa kunaweza kuleta matatizo.
Neno ‘wasaliti wa Mwalimu Nyerere’ lamchefua
Aidha, Dk Salim ameeleza kusikitishwa na kukatishwa tamaa na
kauli za baadhi ya wanasiasa dhidi yake na wajumbe wenzake wa Tume kwa
kuwaita wasaliti na hasa kitendo cha kutilia shaka uzalendo wao.
“Inakatisha tamaa sana. Mimi nina umri wa miaka 72, kati yake
zaidi ya miaka 30 nimeitumikia nchi yangu, haiingii akilini katika umri
huu wa mwisho nianze kuisaliti nchi yangu, inasikitisha sana kusikia
eti hawa wasaliti wa Mwalimu Nyerere,” alisema.
Dk Salim ambaye ni Mwenyekiti wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere
(MNF), alisisitiza kuwa wajumbe hao wamekuwa wakishutumiwa na watu wenye
malengo yao, akitolea mfano kuwa hata Dk Mwesiga Baregu aliwahi
kushutumiwa na chama chake na kutakiwa ajitoe kwenye tume hiyo
iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Itakumbukwa kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekuwa
ikishutumiwa na wanasiasa hasa kutoka CCM kutokana na mapendekezo yake
ya mfumo wa Muungano wa serikali tatu badala ya mbili zinazoungwa mkono
na chama hicho.
Kutokana na tofauti hiyo, wajumbe walio wengi wa Bunge
Maalumu la Katiba kutoka CCM waliamua kubadili baadhi ya vifungu vya
rasimu.
“Ni bahati mbaya sana binadamu unapotukanwa, unatupiwa
madongo, tunaonekana wapuuzi kwa kazi ya kukusanya maoni ya wananchi,
inaumiza sana,” alisema.
Kama ambavyo Jaji Warioba amesema mara nyingi, Dk Salim
aliitetea Rasimu ya Katiba, akisema kilichopendekezwa ndiyo picha halisi
ya maoni ya Watanzania.
Alisema Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi yenye hoja
nzito yakieleza hasa matatizo yao katika nyanja mbalimbali kama afya,
elimu, ardhi na mengine, ingawa hoja kuhusu muundo wa Serikali ndizo
zinaonekana kushikiwa bango na wanasiasa.
Alisema ushahidi wa watu waliohojiwa upo katika maandishi,
sauti na picha za video na idadi yao inatosha kuwakilisha Watanzania
wote.
“Wanasema hatukuhoji watu wengi, waliohojiwa ni
representative sample (sampuli), huwezi kuhoji Watanzania wote milioni
45,” alisema Dk Salim.
Alisema ni jambo la kushangaza kuwa mchakato umetekwa nyara
na wanasiasa lakini Katiba inastahili kuwa ya kitaifa ya Watanzania
wote, wenye vyama na wasio na vyama vya siasa.
Alisema hata kwenye tume, walikuwapo wajumbe zaidi ya 12
ambao hawatokani na CCM, wakitoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na
wote walikuwa na mawazo tofauti lakini waliamua kuyaweka kando na kutoa
rasimu inayotoa taswira ya mawazo na masilahi ya wananchi.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment