JANA taifa
lilisimama saa nne kwa Watanzania kuelekeza masikio na macho kwenye
runinga kusikiliza ufafanuzi wa wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, juu ya upotoshaji wa viongozi waandamizi wa serikali kuhusu
mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya katiba mpya.
Wajumbe wa
Tume hiyo wakiongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba, waliwataja
viongozi hao kuwa ni Stephen Wassira, William Lukuvi, Anna Tibaijuka na
Mwigulu Nchemba katika mdahalo wa katiba mpya uliofanyika Ukumbi wa
Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, uliondaliwa na Taasisi ya Mwalimu
Nyerere na kurushwa na runinga ya ITV.
Jaji
Warioba, alianza kwa kuweka hadharani namna watu wenye propaganda za
mfumo wa serikali mbili wanavyopotosha maana nzima ya rasimu ya pili ya
tume hiyo inayoelekeza mfumo wa serikali tatu.
Alisema
watetezi wa serikali mbili, wamejikita kuelezea upungufu wa serikali
tatu huku wakiacha mazuri ya muundo huo pamoja na udhaifu wa serikali
mbili za sasa.
Jaji
Warioba, alikanusha kauli iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera na Bunge, William Lukuvi, kuwa kuna maoni mapya
yamewasilishwa serikalini.
Alisema
hajabadilika katika msimamo wake wa kutetea serikali tatu kama wananchi
walivyotaka, na kwamba kinachofanywa na wanaoeneza maneno hayo ni uzushi
wenye malengo maalum.
Alifafanua
kuwa kilichofanywa na wao ni kupeleka serikalini yale mambo ambayo
waliyachuja na ambayo yasingekuwa na nafasi katika Serikali ya Muungano
zaidi ya kusubiri Katiba ya Tanganyika.
“Sijabadilika,
na jambo la msingi ni kwamba yale tuliyoyachuja badala ya kutupa
tulisema tukakabidhi serikalini kwa ajili ya kusaidia kuwa kumbukumbu
kwao pale watakapoona wanakwama, lakini muhimu hayo wanayosema
tumepeleka kuonyesha kuwa tumebadilika ni vema waweke hadharani,”
alisema Jaji Warioba.
Alisema bado
kuna haja ya viongozi kuendelea kuvumiliana na kutafuta maridhiano
yatakayozaa katiba bora ya Watanzania, huku akibainisha kuwa hata wao
walikuwa na tofauti zilizomalizwa kwa kuangalia maslahi ya taifa badala
ya makundi waliyotoka.
Kwamba kabla
ya Bunge la Katiba kuanza, aliwashauri viongozi wa vyama vya siasa
kukutana na kukubaliana baadhi ya mambo, na kwamba viongozi hao
hawakuweza kufanya jambo hilo, hali iliyozalisha matokeo ya sasa ya
mchakato ulipofikia.
Jaji Warioba
alikataa dhana ya wanasiasa na wachambuzi mbalimbali wanaotaka Bunge
hilo liahirishwe kwa muda kuchagua baadhi ya mambo yatakayofanyiwa
maboresho huku yakitajwa kuwa ni kuboresha Tume ya Uchaguzi na kutoa
fursa kwa mgombea binafsi.
Alisema, haafiki mambo hayo kuwa kipaumbele na kuachwa kwa mambo muhimu ya wananchi.
Aliyataja
baadhi ya mambo muhimu ya kujadiliwa mbali na masuala ya uchaguzi, kuwa
ni pamoja na suala la uwazi na uwajibikaji, kwa madai kwamba huwezi kuwa
na utawala bora kama hakuna uwazi na uwajibikaji.
Pia, alisema
suala la maadili na tunu ya taifa ni mambo ambayo wananchi
walizungumzia sana na haki za binadamu ambako walitaka kuwekwa kwa
utaratibu wa utekelezaji kwa kuwa hata zilizopo hazitekelezeki.
Aidha, Jaji
Warioba aliwashangaa wale wanaohangaika na takwimu, lakini akasisitiza
kuwa itambulike wajumbe wa tume ndio waliozunguka mikoani na kuzungumza
na wananchi na kuna mengi yalisemwa kwa uwazi kabisa ambayo wengi
hawayajui.
Paramagamba aonya
Kwa upande wake, Profesa Paramagamba Kabudi akichangia katika mjadala huo, aliasa kuzingatia utu na kuheshimu mawazo ya wengine.
Alisema kwa
upande wake, hawahofii Wazanzibar kwa kuwa wao wanayo mambo yao na
yanayojulikana, na kwamba Watanganyika mambo yao wameyaficha mioyoni,
jambo aliloeleza kuwa ni hatari kama hawatapatiwa mahitaji yao mapema.
Alisema
kwamba ni wakati muafaka hivi sasa Watanganyika wakapewa serikali yao
wakiwa wanaidai kwa amani, badala ya kusubiri waongezeke na kuidai kwa
nguvu.
“Ni busara
kuwapa Watanganyika serikali yao wakati wanaiogopa, badala ya kusubiri
waidai wakati wakiwa wengi na muda wa kuwaongoza ukiwa haupo,” alisema
Profesa Kabudi na kutoa mfano wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ambaye
wakati wa mchakato wa taifa kuingia mfumo wa vyama vingi miaka ya 90
mwanzoni, licha wakati ule waliokuwa wakitaka vyama vingi walikuwa
wachache, alivikubali, kwani alijua ni bora kuliko waliokuwa wakiunga
mkono wangepuuzwa na kuja kuvidai kwa nguvu.
Kuhusu
muundo wa rasimu, Profesa Kabudi alisema inatoa fursa ya rais wa
muungano kushitakiwa kwa uhaini kama atakiuka mambo yaliyoamuliwa na
mahakama ya muungano.
Alisema
tatizo kubwa lililopo, ni kwa watu waliojivika upumbavu kushupalia kila
jambo hata kama hawana uwezo nalo, wakiamini nguvu zitawalinda huku
akisisitiza kuwa, hakuna aliye mkubwa juu ya sheria.
Butiku amshangaa rais
Mwenyekiti
wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, kwa upande wake alieleza
kuwa Rais Kikwete alipokubali mchakato wa katiba na kuunda tume, hakuwa
na mamlaka ya kuiingilia tena.
Alisema
jambo la msingi ni wahusika kufuata kile kilichokusanywa kwa wananchi na
kuheshimu, badala ya yale wanayoyakwaza kwenda kupata ushauri ndani ya
chama.
“Ninyi
simamieni kile mnachoamini kilichokusanywa na tume, hapa hakuna nani
wala nani, hata Wassira hayupo, watu wanasema tume imesema uongo, lakini
tunajua namna umri wetu ulivyo, tutasema uongo kwa ajili ya nini, huu
mchakato ni wa wananchi,” alisema Butiku.
Alisema
katika mazingira ya sasa wanapoamua kusema wanaitwa wachochezi, na
kwamba wananchi wanapaswa watafakari kwanini baadhi ya vitabu
walivyokusanyia maoni vimefichwa na tovuti ya tume imefungwa.
Aliongeza
kuwa Jaji Warioba anaficha baadhi ya mambo, ikiwamo kueleza wazi kuwa
kutungwa kwa katiba ya Zanzibar ya 2010 kulivunja uwepo wa muungano.
Alipoulizwa
kama hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa bungeni iliharibu mchakato mzima
wa Katiba Butiku, alisema nchi ina Rais na anaheshimiwa sana na kwamba
heshima ina pande mbili huku akizitaja kuwa njia mojawapo ya kumheshimu
rais ni kutokuficha ukweli na kwamba upande wa pili ni heshima ya
kuficha ukweli.
Alisema mtu
atakayeficha ukweli atakuwa hamuheshimu rais, na kwamba kitendo cha
kusema hakushauriana na tume kinapaswa kifikiriwe kwa makini kwa kuwa
wao walishauriana nae vya kutosha.
Butiku
alisema rais anapaswa kuheshimiwa na hata eneo alilotolea kauli hiyo
linapaswa kuheshimiwa, na kwamba muhimu Watanzania wajue kuwa
walishauriana kwa kina.
Polepole afichua siri
Aliyekuwa
mjumbe wa tume hiyo, Humphery Polepole, alisema wakati wakikusanya
maoni, viongozi mbalimbali wa kiserikali waliojitokeza mbele yao
walitaka muundo wa serikali tatu na hata tasisi wanazozisimamia
zilibainisha umuhimu wake.
Alizitaja
taasisi hizo kuwa ni Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Tume ya Makatibu
na Viongozi wa Serikali ya Zanzibar, pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Alisema
anapowaona baadhi ya viongozi waliotoa maoni ya serikali tatu
wanavyotumia nguvu ya kutaka serikali mbili wakiwa hadharani, anashindwa
kuwaelewa wana dhamira gani kwa Watanzania.
Kuhusu
gharama za Serikali ya Muungano, Polepole alisema hakuna gharama kubwa
zaidi ya kupunguza matumizi na kubainisha kuwa haziwezi kuzidi sh
trilioni 2.
Awadh Said ashangaa madai ya gharama
Mwanasheria
Awadh Said ambaye naye alikuwa mjumbe wa tume hiyo, alisema anashangazwa
na watu wanaokimbilia takwimu na gharama katika suala zima la rasimu
huku wakishindwa kuainisha idadi ya wabunge watakaopungua kwa kupatikana
serikali tatu.
Alisema
muundo mzima wa wabunge wote wa muungano kwa sasa una watu 434 na kwamba
katika Serikali ya Muungano iliyopendekezwa idadi hiyo itapungua kwa
wabunge 100.
Kwamba tume haikuelekezwa ichukue takwimu bali uzito wa hoja, na kwamba hoja zilizotolewa ndizo zimezaa rasimu iliyopo.
“Nashangaa
wengine wanajiita wachumi huku wakishindwa kuona namna gharama
zitakavyopungua katika muundo wa serikali tatu, lakini katika hali ya
sasa wanapaswa watuambie ni wizara gani inayofanya kazi yake Zanzibar
ukiacha zile za muungano na sana sana ile ya Mambo ya Ndani,” alisema
huku akihoji kama Wizira ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewahi kwenda
kusimamia maendeleo ya ardhi Zanzibar.
Aliongeza
kuwa kwa sasa Zanzibar inajisimamia kwa masuala mbalimbali, ikiwamo
ardhi, hivyo kusema uwepo wa serikali tatu ni gharama ni kuudanganya
umma.
Awadh
alisema suala la muungano kwa bahati mbaya linazungumziwa na watu
wasiolielewa au hawapendi kufuatilia mambo, zaidi ya kutengeneza
propaganda na vitisho.
CREDIT: TANZANIADAIMA: TUME YA WARIOBA YAIVUA NGUO SERIKALI
No comments:
Post a Comment