Watafiti wakitoa sampuli za damu kutoka kwa sokwe mtu katika utafiti wa Ukimwi huko Gabon. Picha ya Mtandao
|
Watafiti katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Temple,
Marekani wamegundua dawa ya kuangamiza Virusi Vya Ukimwi (VVU) ambayo ni ya
uhakika zaidi ukilinganisha na zilizowahi kupatikana katika tafiti za awali
duniani.
Dawa yao inaweza kutumika
kwa tiba ya wanaoishi na VVU na kinga kwa wale ambao bado hawajaambukizwa.
Mmoja wa watafiti hao, Dk. Kamel Khalili aliwaambia waandishi wa habari juzi mjini Philadelphia, Marekani
kuwa tofauti na utafiti mwingine, wao wamegundua namna ya kukiondoa kirusi
kilichoingia kwenye kinasaba (DNA) ndani ya CD4 na kukitoa nje na hatimaye
kukiua.
Alisema dawa hiyo
inafanya kazi hiyo bila kuathiri seli za mwili wa binadamu.
Dk Khalili alisema
ugunduzi wao ni wa hali ya juu zaidi kwa sababu teknolojia ya kutengeneza dawa
hiyo ni tofauti na nyingine zilizokwisha kugunduliwa ambazo hazina uwezo wa
kupenya ndani ya seli za binadamu, bali kuathiri tu VVU vilivyopo nje yake,
ndani ya mfumo wa damu.
“Dawa yetu inakivuta
kirusi nje ya seli (CD4) bila kuiathiri seli yenyewe na kukiua. Hivyo dawa hii
itatumika kwa muda fulani na kuua virusi vyote mwilini na hakuna haja ya
kuitumia wakati wote kama ilivyo dawa ya kufubaza VVU (ARV).” Alisema
ARV huangamiza VVU
vilivyopo kwenye damu na kuendelea kuviacha hai vile ambavyo tayari vimeingia
ndani ya CD4, hivyo kufanya virusi kuzuka upya pindi mwathirika anapoacha
kutumia dawa.
Mmoja wa wataalamu katika
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Kituo cha Mbeya
(NIMR-MMRC), Clifford Majani ameuelezea utafiti huo kama mwanga mpya katika
teknolojia ya kukabili VVU,
“Kama imepatikana
teknolojia ya kukiondoa kirusi ndani ya seli ni hatua nzuri ya kukabili VVU kwa sababu hili
lilionekana kuwa gumu sana mwanzoni,” alisema Majani.
Alisema imekuwa vigumu
kuua kirusi kikiwa ndani ya seli na hata baadhi ya wanasayansi wamejaribu
kutengeneza dawa itakayotambua seli zilizoathirika ili ziuawe lakini hilo
likawa gumu.
“Inaweza ikapatikana dawa
ya namna hiyo (inayoua seli zilizoathirika) lakini ikawa inaathiri vitu vingine
ndani ya mwili, hilo halikubaliki. Kikubwa katika ugunduzi huo ni dawa kuweza
kukifuata kirusi kinakojificha na kukiondoa, jambo ambalo dawa nyingi
zimeshindwa zikiwamo ARV,” alisema.
Hata hivyo, Majani
alisema changamoto ambayo inaweza kujitokeza katika majaribio ya dawa hiyo ni
usalama wakati wa matumizi.
No comments:
Post a Comment