Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemhukumu
kifungo cha miaka sita jela, Melkiad Kabunduguru (28) baada ya
kupatikana na hatia ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na
kukutwa na noti bandia.
Kabunduguru ambaye ni mwanafunzi wa
Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) atatumikia kifungo hicho baada ya Mahakama
kuridhika na ushahidi uliotolewa dhidi yake.
Katika shtaka la kwanza la Kabunduguru
atatumikia kifungo cha miaka minne baada ya kupatikana na hatia ya
kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu huku shtaka la pili la kukutwa
na noti 50 za bandia za Sh5000 mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka
miwili.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Juma
Hassani alisema mshtakiwa atatumikia vifungo hivyo kwa pamoja baada ya
Mahakama kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Juma
Hassani alidai kuwa mshtakiwa huyo atatumikia kifungo hicho ili iwe
fundisho kwa vijana wengine wenye tabia za wizi.
Kabla ya kutoa hukumu hiyo, upande wa
Jamhuri ukiongozwa na Mwendesha mashtaka, Felista Mosha uliiomba
mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa vijana
wengine wenye tabia za udanganyifu.
“Mheshimiwa hakimu naiomba mahakama hii
tukufu kutoa adhabu kali dhidi ya mtuhumiwa huyu kutokana na kushamiri
kwa vitendo vya udanganyifu na kujihusisha na matumizi ya noti bandia
wakati akijua kuwa ni kosa la kisheria,” alidai Mosha .
Baada ya Hakimu Hassani kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, alimuhukumu Mwiganyi kifungo cha miaka sita jela.
Awali, Wakili wa Serikali, Felista
Mosha alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari
29, mwaka huu katika Barabara la Ally Hassan Mwinyi katika mashine ya
kutolea fedha (ATM) ya NMB iliyopo Chuo cha Biashara (CBE) na kujipatia
Sh100,000 kutoka kwa Expedith Mtisi kwa madai kuwa angemrejeshea lakini
hakufanya hivyo.
Katika shtaka la pili, mshtakiwa alikutwa na noti bandia 50 za Sh5000.
No comments:
Post a Comment