Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ametangaza rasmi
kuungana na umma mpana, kupinga rasimu ya Katiba Mpya inayopendekezwa na
Bunge Maalum la Katiba (BMK).
Hatua hiyo
isiyotarajiwa, inafuatia Bunge Maalum la Katiba kukamilisha rasimu hiyo
Jumatano iliyopita, ikitarajiwa kupigiwa kura mapema wiki ijayo.
Akizungumza
kwenye adhimisho la miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), Aidha, Jaji Warioba, alisema Bunge hilo
limeondoa mambo ya msingi yaliyopendekezwa na wananchi yakiwa ni kiini
cha kupatikana kwa Katiba Mpya.
Adhimisho
hilo lilitumika pia kumkumbuka muasisi wa LHRC, marehemu Dk. Sengondo
Mvungi, ambapo kitabu kinachoelezea maisha yake, kinachoitwa ‘Sengondo
Mvungi, breathing the Constitution’ ikimaanisha, ‘Sengondo Mvungi, pumzi
ya Katiba’, kilizinduliwa.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, rasimu ya Katiba inayopendekezwa na BMK ni mfano wa ile iliyopo sasa ikiwa imewekewa viraka.
“Bunge
limeacha mawazo ya wananchi na kuingia katika mikakati na misimamo yao,
walioona rasimu yetu siyo, watatoka bungeni watakutana nasi mitaani,
tutatetea maoni ya wananchi na wao watoke waje kutetea mawazo yao,”
alisema.
Jaji
Warioba, alitoa mfano wa mambo ya msingi yaliyotokana na maoni ya
wananchi, yakaondolewa na BMK kuwa ni maadili, tunu za taifa,
mgawanyiko wa madaraka, miiko ya uongozi na Muungano.
MAADILI
Jaji
Warioba, alisema wananchi waliotoa maoni walisisitiza masuala yanayohusu
maadili kwa taifa yaingizwe kwenye Katiba Mpya, lakini hali hiyo
haikukubalika kwa BMK.
Kadhalika,
alisema tunu za Taifa ambazo ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi,
uwajibikaji na lugha ya taifa zilizopendekezwa na wananchi, rasimu hiyo
ya bunge imezipunguza na kubaki nne tu.
Alizitaja zilizowasilishwa na rasimu ya bunge kuwa ni lugha ya Kiswahili, muungano, utu na udugu na amani na utulivu.
“Tunu za
taifa zilizopendekezwa na wananchi, na siyo vyama vya siasa wala tume
zimeondolewa, Bunge linasema eti ni hiyo ni misingi ya utawala,”
alisema.
Aliongeza, “mimi siwaelewi kabisa kusema hizo siyo tunu za kitaifa, siwaelewi kabisa,” alisema.
Alisema, sura ya tatu ya rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Tume yake, ilihusu miiko ya uongozi.
Jaji
Warioba, alisema sura hiyo ilieleza kuwa kiongozi wa umma hapaswi kuwa
na akaunti ya benki nje ya nchi na kutangaza mali na madeni yake.
Pia,
ilieleza kiongozi huyo anapaswa kuwasilisha kwenye ofisi za umma zawadi
anazopewa, kutotumia mali za umma kwa mambo binafsi, kukomesha rushwa na
ufisadi.
Alisema, miiko ya uongozi ilifanikisha kukabiliana na kadhia kama Ufilipino, Kenya, Namibia na Afrika Kusini.
“Tunajua
ufisadi na rushwa ndiyo chanzo cha hayo yote, watu wanapewa zawadi
wanasaini mikataba ya hovyo, lakini tunapokuwa na miiko yeyote
atakayebainika amepokea zawadi au ana akaunti nje ya nchi
atawajibishwa… kwenye haya wameniita mimi ni shida,” alisema.
MADARAKA YA NCHI
Jaji
Warioba, alisema wananchi walipendekeza kumuondoa Mwakilishi
asiyewajibika kwao, kuwapo ukomo wa ubunge na muundo wa serikali tatu,
lakini vimeondolewa na BMK.
“Wananchi
walisema baadhi ya wabunge ni watalii kwenye majimbo yao, wakataka
wapate mamlaka ya kuwaondoa, cha ajabu wenyewe wamejipa mamlaka ya
kumfukuza mbunge asiyeshiriki kikao kimoja, na vyama vya siasa vimejipa
madaraka ya kuwaondoa wabunge wao, kwa nini mwananchi anyimwe hili,”
alihoji.
MGAWANYO WA MADARAKA
Alisema,
Tume ilipendekeza kuwa kutokana na mwingiliano uliopo kati ya Bunge na
Serikali, ipo haja ya kuwapo mgawanyo wa madaraka kwenye Katiba Mpya.
Alitoa mfano
namna ushawishi wa Rais ulivyofanikishwa kurejeshwa bungeni kwa Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kukutana na viongozi wa upinzani.
Aliongeza,
“hata sasa, wakati rasimu yao inasema Katiba itaitwa ya mwaka 2014, Rais
anasema haiwezi kupatikana mwaka huu hadi 2016. Huu ni muingiliano wa
madaraka, ndio maana tume tuliona kila mhimili ujitegemee.”
MUUNGANO
Jaji
Warioba, alisema muundo wa serikali tatu ulipendekezwa na wananchi na
kwamba ndani ya Tume, kila mjumbe alikuwa na maoni yake.
“Mfano
Baregu (Profesa Mwesiga Baregu) alitaka serikali mbili, Joseph Butiku
alitaka moja, Awadhi Said alikuwa muumini wa Muungano wa mkataba, mimi
ni serikali mbili kwenda moja,” alisema.
AZIPONDA KURA ZA MTANDAO
Jaji
Warioba, alisema pamoja na kasoro iliyopo kupigia kura ibara badala ya
sura za rasimu ya Katiba inayopendekezwa, alipinga pia utaratibu wa
kuruhusu wajumbe wasiokuwapo bungeni kupiga kura.
“Kusaka kura
kwa mtandao hakuwezi kutuletea Katiba ya maridhiano na mimi nimeanza
kukata tamaa, ninachoona mchakato huu utarudiwa mara baada ya
kupatikana kwa Rais mpya,” alisema na kuongeza:
LHRC BILA DK. MVUNGI
Mkurugenzi
Mtendaji wa LHRC, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema endapo angekuwapo Dk.
Mvungi, angeshangaa kuona maslahi ya taifa yanatupwa na yale ya itikadi
yanapewa kipaumbele.
Pia, alisema
angeshangaa kuondolewa kwa vipengele kama kuwajibishwa wabunge, ukomo
wao na jinsi mchakato ulivyokiuka maoni ya wananchi.
Mjane wa Dk.
Mvungi, Anna Mvungi, alisema baada ya kuteuliwa katika tume, moja ya
kauli zake (Dk. Mvungi) ilikuwa ni ‘nimetimiza nia yangu’.
Mwenyekiti wa ukoo wa Mvungi, Adrian Mvungi, aliiasa LHRC kuondokana na woga na kuendeleza mapambano ya kutetea haki za watu.
Mmoja wa
wahariri wa kitabu hicho, Profesa Chris Maina, alisema Dk. Mvungi
alikuwa ni Profesa kutokana na makala 20 alizoziandika kwa wananchi na
shauri kuhusu wanyonge na matatizo wanayoyapata. Kuhusu Tume ya Warioba,
alisema pamoja na `madongo’ wanayoyapa wamekuwa imara kutokana na yote
waliyosimamia waliyaamini.
“Jinsi
tunavyopata vioja vya Dodoma tunazidi kuvumbua ubora wa tume hii,
wananchi wanajua mchele na pumba historia haifutwi na FFU,” alisema.
Mwenyekiti
wa chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia, alisema kuna mazungumzo
yanayoendelea yakivihusisha vyama vya siasa hususani vyenye wabunge, ili
kuinusuru Katiba Mpya.
“Yapo
mazungumzo yanayoendelea yanahusisha vyama vyote vyenye wawakilishi
bungeni CCM, Chadema na NCCR-Mageuzi, tunataka Tanzania isifike mahali
tukamwaga damu kwa sababu ya ubinafsi wa watu wachache,” alisema.
KITABU CHA DK. MVUNGI
Katika
kitabu hicho zipo makala mbalimbali za wanataaluma, familia na wanafunzi
na walimu wake, wananchi na wanahabari ambazo zimemuelezea jinsi
alivyofanya kazi za utetezi wa wanyonge.
Kitabu hicho
ambacho kimepambwa na picha 157 kina sura kumi ambazo waandishi wake
wametumia lugha mbalimbali kufikisha ujumbe ambazo ni Kiswahili,
Kingereza, Kijerumani na Kipare kilichokuwa lugha ya Dk. Mvungi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment